July 21, 2020

MAKAMU WA RAIS MGENI RASMI MBIO ZA “CRDB BANK MARATHON 2020”

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (katikati), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari wakati wa kutambulisha mbio za hisani “CRDB Bank Marathon 2020” zinazoandaliwa ili kuhamasisha uchangiaji wa fedha kwa ajili ya upasuaji kwa watoto wenye magonjwa ya moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete jijini Dar es salaam, leo. Nsekela alisema CRDB Bank Marathon inatarajiwa kukusanya shilingi milioni 200 ambapo washiriki zaidi ya 4,000 wanatarajiwa kushiriki siku hiyo tarehe 16 Agosti, 2020 jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete, Prof. Mohamed Janabi na kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Sanlam Insurance, Khamisi Suleiman.


Na Asha Mwakyonde

 
BENKI ya CRDB imeaandaa shindano la mbio za hisani lenye lengo la kukusanya fedha kwa ajili ya kusaidia upasuaji watoto 100 wenye matatizo ya moyo waliopo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete JKCI.
 
Mbio hizo zitafanyika Agosti 16, mwaka huu katika viwanja vya Oysterbay jijini Dar es Salaam, mgeni rasmi  anatarjiwa kuwa Makamu wa Rais Samia Suluhu na kwamba kauli mbiu ya mbio hizo ni 'Kasiisambazayo Tabasamu'.
 
Akizungumza jijini Dar es Salaam Julai 21,mwaka huu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, amesema benki hiyo imekuwa ikisimamia katika kuisaidia jamii yenye  kipato duni.

Mkurugenzi huyo amesema benki hiyo imekuwa ikitenga kiasi cha fedha kwa lengo la kuisaidia jamii huku ikiiunga mkono serikali kuboresha huduma za kijamii. 'Sera yetu imelenga kuisaidia jamii katika  nyanja za elimu, afya na nyingine, tumekuwa tukiwasaidia watoto wenye matatizo ya moyokufanyiwa upasuaji,'amesema Nsekela.
 
Ameongeza kuwa wanatarajia kupata washiriki wa mbio hizo zaidi ya 4000 lengo likiwa ni kukusanya Sh.milioni 200. Mkurugenzi huyo amezishukuru taasisi za Strategis, Sunlam, ARIS, Alliance, EFM, TVE, na Cool Blue kwa kushirikiana na benki hiyo.
 
Aidha amewaomba wananchi kujiokeza kulipia kiasi cha fedha 30,000 kwa kila mshiriki ili kuwasaidia watoto 100 wanaosubiri kufanyiwa upasuaji wa moyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Prof. Mohamedi Janabi amesema kuwa bado kuna watoto zaidi ya 500 wanaohitaji kufanyiwa upasuaji wa moyo waliotoka katika familia zenye kipato cha chini.
 
Prof. Janabi amefafanua kuwa kila mtoto anatumia kiasi cha shilingi milioni 2 kufanyiwa upasuaji na kwa mwaka huu taasisi hiyo imefanikiwa kuwafanyia upasuaji zaidi ya watoto  1000 wenye matatizo ya moyo.

No comments:

Post a Comment

Pages