July 11, 2020

TAASISI YA HAWA YAWAHASISHA WANAWAKE KUJITOKEZA KUGOMBEA NAFASI KWENYE UCHAGUZI MKUU

Mkurugenzi wa Taasisi ya Haki za Wanawake (HAWA) Joyce Kiria akizungumza na Waaandishi wa Habari (Hawapo pichani ) wakati akitoa wito kwa wanawake kujitokeza katika kugombea nafasi mbalimbali wakati wa uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu.


Na Dixon Busagaga

Mkurugenzi wa taasisi ya Haki za Wanawake (Hawa) Joyce Kiria amewataka wanawake kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi mkuu.

Amesema kwa mfumo ambao umetengenezwa sasa na serikali ya awamu ya tano, mchakato wa kugombea umeondolewa urasimu hivyo kutoa nafasi hata watu wasio na fedha kuwania na kuchaguliwa.

Kiria alisema endapo wanawake wengi watajitokeza na kuchaguliwa itasaidia utungwaji wa sera na sheria  zitakazosaidia kukabiliana  na changamoto zinazozikabili kundi hilo.

Alisema chini ya uongozi wa awamu ya tano jitihada kubwa zimefanyika kuhakikisha inaboresha sekta ya afya kwa kujenga vituo vya afya, dawa hatua iliyochangia kupunguza vifo vya wanawake na watoto.

“Ile dhana ya kwamba wanawake ni wapiga kampeni na kuwanadi wagombea tuachane nayo. Tujitokeze kwa wingi kugombea na kuchaguana. Rais John Magufuli ameondoa urasimu kabisa hivyo sasa hivi sio lazima uwe na fedha nyingi ndio upate nafasi ya kugombea. Ametutengenezea mazingira mazuri ya kuingia kwenye mchakato.

Twendeni tukagombee, tukachukua hizo nafasi ili tumsaidie rais ambaye ameonyesha jitihada kubwa katika kutukwamua wanawake. Amewaamini wanawake wengi na wamefanya kazi nzuri iliyotukuka,”

Kiria alisema uwepo wa wanawake wengi kwenye ngazi za maamuzi utasaidia utungwaji wa sheria na sera zitakazoondoa ukandamizaji wa kundi hilo na kuwakwamua katika nyanja mbalimbali.

No comments:

Post a Comment

Pages