July 11, 2020

TSB YASEMA ZAO LA MKONGE LATUMIKA KUTENGENEZA BIDHAA MBALIMBALI NCHINI

Na Janeth Jovin

BODI ya ya Mkonge Tanzania (TSB), imesema asilimia nne tu ya mazao ya mkonge ndio yanatumika kutengeneza bidhaa mbalimbali hapa nchini,huku asilimia 96 ikipotea kutokana na ukosefu wa teknolojia za kisasa za kutengeneza bidhaa bora.

Akizungumza kwenye mkutano wa Ana kwa Ana (B2B)wa wafanyabiashara kwenye Maonesho ya 44,ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF), yanayoendelea Afisa Mipango na Utafiti wa TSB,Frederick Sospeter amesema zao la mkonge lina faida nyingi lakini bado mazao yake hayatumiki kwa kiwango stahiki.

"Mazao ya mkonge yana faida nyingi na yanatumika kwenye sekta mbalimbali kama vile viwanda,kilimo, viwanda vya kutengeneza dawa ,kwenye meli,ndege na magari ambapo nyuzi za mkonge hutumika na bidhaa nyingine  ya zao hilo hutumika kama chakula cha mifugoo na mbolea,ila hapa kwetu bado tuko nyuma kwa sababu ya teknolojia duni,"amesema Sospeter.

Amesema pamoja na changamoto hiyo ya teknolojia duni lengo la bodi hiyo ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 wanazalisha tani 120,000 za zao la mkonge kwani hivi sasa zao hilo linazalisha kiasi cha tani 40,000 tu.

Akizungumzia hatua walizofanya kuhakikisha wanapata wawekezaji kwenye sekta hiyo Sospeter amesema juhudi zinaendelea za kuwapata wawekezaji ili kuwekeza kwenye zao hilo na kuwa na teknolojia ya viwanda vitakavyotumika kuchakata mazao hayo kupata bidhaa mbalimbali zenye ubora na kupata fedha nyingi kuliko kuendelea kuzalisha malighafi ambayo haina thamani kubwa ukilinganisha na bidhaa zake.

"Utaona bidhaa za mazao ya mkonge yana thamani kubwa kuliko kuzalisha malighafi ya mkonge ambayo thamani yake ni ndogo,tunaendelea kutafuta wawekezaji ili waje na teknolojia bora ya kuwa na viwanda vitakavyojengwa na kutumia malighafi hizi kutengeneza bidhaa za mkonge zenye fedha zaidi,"amesema Sospeter.

Akichangia kwenye mkutano huo wa uliowashirikisha wadau mbalimbali wa masoko wakiwemo Soko la Mazao Tanzania (TMX) amesema kuanzia Desemba mwaka huu wataanza kuuza mazao ya mkonge ya wakulima wadogo kama njia mojawapo ya kuinua sekta hiyo.


Kwa mujibu wa taarifa kutoka TMX wanazungumza na bodi ya vyama vya msingi vya mazao (AMCOS),ili kukamilisha baadhi ya taratibu ili ifokapo Desemba mwaka huu waanze kuuza mazao ya mkonge ya wakulima wadogo kwa mfumo wa kieletroniki.

"Tutaanza nwishoni mwa mwaka huu kuuza mazao ya mkonge ya wakulima wadogo wa zao hilo tutayaweka kwenye soko letu ambalo ni la wazi ili yapate wateja,"alisema Mkurugenzi wa Mwendeshaji wa TMX,Augustino Mbulumi.

No comments:

Post a Comment

Pages