July 08, 2020

TUTAFUFUA VYUO NA VITUO VYA UTAFITI WA KILIMO-MAJALIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama maziwa yanayotokana na korosho wakati alipotembelea  Taasisi ya Utafiti wa Kilimo, Naliendele, Mtwara, Julai 7, 2020. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Taasisi  ya Utafiti wa Kilimo Naliendele, Dk. Fortunus Kapinga (kushoto), kuhusu utafiti wa mbegu bora za mhogo unaofanyika katika Taasisi hiyo, Julai 7, 2020. Wa pili kushoto ni Mtafiti Mkuu katikaTaasisi hiyo, Bernadetha Kimata. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
 
 
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli itahakikisha kwamba vyuo na vituo vyote vya utafiti wa kilimo nchini vinafufuliwa, hivyo Wizara ya Kilimo inatakiwa kutenga fedha za kutosha katika bajeti yake kila mwaka.

“Nataka niwahakikishie Serikali yenu imedhamiria kuimarisha kilimo pamoja na utafiti wake. Mwezi mmoja uliopita nilikuwa Mlingano mkoani Tanga kuona shughuli za utafiti wa zao la mkonge lakini miezi miwili iliyopita nilikuwa kwenye chuo kipya tulichokianzisha kule Kigoma cha utafiti cha Kihinga na nimeona kazi yake na tutapata mafanikio makubwa.”

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana (Jumanne, Julai 07, 2020) alipotembelea Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Naliendele iliyoko mkoani Mtwara kwa lengo la kujionea shughuli za utafiti wa mazao mbalimbali ya kilimo zinazoendelea kituoni hapo.

Alisema Rais Dkt. John Pombe Magufuli amefurahishwa na kazi nzuri za utafiti wa mazao mbalimbali zinazofanywa na vituo vya utafiti na matokeo mazuri ya utafiti huo kwa wakulima wa Watanzania.

Waziri Mkuu alisema “Azma ya kusimamia na kuona vyuo vya utafiti vinafanya kazi yake vizuri ni pamoja na maboresho haya kwanza wizara husika lazima itambue  kuwa vyuo vya utafiti vinamchango mkubwa, wizara kwenye bajeti zake ipeleke fedha nyingi kwenye utafiti na tuone utafiti unagundua mambo na yale yanayogunduliwa yaende yakafanyiwe kazi.”

Vilevile, Waziri Mkuu alisema idadi ya udahili wa wanafunzi katika vyuo vya kilimo itaongezwa ili wapatikane wataalamu na watafiti wengi ambao wanahitajika sana katika kufanikisha mapinduzi ya kilimo nchini.

Tasisi ya hiyo ya Kilimo ya Naliendele ni miongoni mwa vituo vya utafiti wa kilimo nchini ambavyo vimewawezesha wakulima wengi kujiongezea tija na kujikwamua kiuchumi baada ya kutumia mbegu bora zinazozalishwa kituoni hapo kama za korosho, ufuta na muhogo.

No comments:

Post a Comment

Pages