July 18, 2020

UJENZI BWAWA LA UMEME JULIUS NYERERE; HATUA ZOTE 8 ZA UJENZI WA MRADI ZINAKWENDA KWA KASI

Mashine zikichoronga mlima na malori yakibeba kifusi kwenye bonde la mto Rufiji eneo la mradi wa ujenzi wa bwawa la umeme la Julius Nyerere (JNHPP-MW2115) Julai 17, 2020.


Na Mwandishi Wetu, JNHPP
HATUA zote nane (8) za utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa bwawa la kufua umeme wa maji la Julius Nyerere (JNHPP-MW2115) kwenye bonde la mto Rufiji unaendelea kwa kasi inayohitajika, Mhandisi mkazi wa mradi huo Eng. Mushubila Kamuhabwa amewaambia waandishi wa habari kwenye eneo la mradi Julai 17, 2020.
Eng. Kamuhabwa ametaja hatua hizo kuwa ni ujenzi wa njia kubwa ya ardhini ya mchepuko wa maji (diversion tunnel), sehemu ya kufua umeme (power house), ukuta utakaotengeneza bwawa, eneo la kupokelea umeme unapozalishwa (Switch yard), power intake, barabara na madaraja, saddle dams nne na kuchakata mawe yanayotumika kutengeneza zege na mahitaji mengine.
“Mradi huu wa JNHPP una miradi mingi ndani yake na yote iko katika hatua mbalimbali na hatua hizo kama nilivyozitaja kwa pamoja ndiyo zinajenga mradi mmoja wa Julius Nyerere Hydro Power Project Megawati 2115 katika hilo ujenzi unaendelea katika maeneo yote hayo, mafundi wako kazini na wanaendelea na ujenzi kwa kasi kubwa kama inavyohitajika.” Alisema Eng. Kamuhabwa.
Alisema jambo la kufurahisha tayari mradi umeanza kuchangamsha uchumi wa nchi na kutolea mfano wakati wakiweka zege kwenye njia ya kuchepusha maji (diversion tunnel, zaidi ya tani 200 za nondo zimetumika hii inafaidisha viwanda vyetu hapa nchini lakini pia wananchi wanaokaa vijiji vinavyozunguka eneo la mradi wanafaidika kwa namna mbalimbali ikiwwemo miundombinu wezeshi kama vile umeme unaotoka Morogoro kuja hapa umepitia kwenye vijiji kadhaa natayari baadhi yao wameanza kufaidika na umeme huo.” Alisema na kuongeza…Lingine zaidi ya vijana wa Kitanzania wapatao 4,000 kutoka maeneo mbalimbali nchini hususan yale yanayozunguka eneo la mradi wameajiriwa na wanashiriki katika mradi kwa ari kubwa.
“Tunatarajia idadi hiyo ya ajira ikaongezeka hadi kufikia watu 6,000 mradi utakapofikia hatua ya juu peak.” Alisema Eng. Kamuhabwa.
Kwa upande wao baadhi ya wanakijiji wa Kisaki kilomita 60 kutoka eneo la mradi wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Magufuli kwa kuwaletea mradi huo kwani tayari manufaa yake wameanza kuyaona.
“Kisaki inakuja juu, tuna uhakika mradi ukimalizika Kisaki itakuwa kama Morogoro, kwa sasa biashara inakuwa kwa kasi sana tofauti na hapo awali, mfano mchele tunauza kwa kilo shilingi 1,600/= tofauti na hapo awali tulikuwa tunauza shilingi 500/= bei ya juu kabisa shilingi 1,000/=, watu wameongezeka sana.” Alisema mwanakijiji wa Kisaki Ali Matumbo na kuongeza…umeme nao tayari umefika kijijini kwetu, shule imepata umeme kwa hivyo tunafuraha sana kwa ujio wa mradi huu na tunampongeza sana Rais wetu Magufuli.
Naye mwanakijiji mwingine Bi. Asha Said alisema, anauhakika hata barabara nzuri itajengwa kutokana na mradi huo na anafurahi kuona wageni wengi wanafika Kisaki na hivyo biashara zao zimechangamka.
Naye mwanakijiji mwingine Hassan Mohammed Ngozi alisema, anayo matumaini makubwa kwa hali anavyoiona hivi sasa hapo Kisaki, mradi utakapokamilika watakuwa na Kisaki mpya.
“Kwetu sisi ongezeko la watu hapa Kisaki limekuwa na faida kubwa………..watu wakienda kufanya kazi huko kwenye mradi wanakuja hapa kijijini wananunua bidhaa zetu na sisi tunapata pesa haya ni manufaa makubwa kwetu.” Alisema Bw. Ngozi.

No comments:

Post a Comment

Pages