July 17, 2020

WAKAZI WA MVUMI WALALAMIKIA KUTOZWA FEDHA

Wakazi wa eneo la Mvumi Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro wamelalamikia kitendo cha baadhi ya watu wanaohodhi mashamba makubwa kuwatoza shilingi elfu 30 ili waoneshwe mahali pa kulima mbali na kutozwa gunia moja au shilingi laki moja kwa kila heka moja baada ya mavuno.

Hayo yamebainika wakati wa ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni mjumbe Maalum katika kamati iliyoundwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli ya kufuatilia,kutathmini na kutoa mapendekezo na ushauri kwa Rais ili kumaliza migogoro ya ardhi ya muda mrefu wilayani Kilosa.


Baadhi ya wananchi hao wamesema licha ya Serikali kuwaazimisha baadhi ya mashamba kwa ajili ya kuendesha kilimo bado mashamba hayo hayakukidhi mahitaji ya ardhi kwa wananchi hao jambo linalowapa fursa baadhi ya watu wanaohodhi mashamba makubwa kutumia fursa hiyo kuwaumiza wananchi 

 Akijibu malalamiko hayo ya wananchi wa mvumi Wilayani Kilosa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi amesema baada ya kupokea malalamiko hayo na kuijonea mashamba yanayolalamikiwa hatua inayofuata ni ya kwenda kutafuta hati za shamba hilo ili kumfahamu mmiliki na kisha kumshauri Rais. 



Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Mwambambale Asajile amesema tatizo la ardhi Wilayani humo limekuwa kubwa kutokana na hulka ya wakulima hao kuuza tena mashamba hayo pale serikali inapoyafuta na kuyarudisha kwa wananchi  

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli aliunde kamati maalum kwa ajili ya kutathmini na kumpa ushauri kuhusu mashamba makubwa ambayo mengine yametelekezwa na kuwa mashamba pori ili ayafute na kuyagawa kwa wananchi ikiwa ni jitihada za kumaliza matatizo ya ardhi wilayani Kilosa ambayo yamekuwa yakisababisha maafa hususani baina ya wakulima na wafugaji.

No comments:

Post a Comment

Pages