July 20, 2020

WAZEE KILIMANJARO WAJIPANGA KUMPA TUZO NA KUMUOMBA RADHI RAIS MAGUFUL

Mwenyekiti wa kamati inayoratibu tuzo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tazania kutoka kwa wazee na jamii ya watu wa mkoa wa Kilimanjaro,Yunusi Mmari akizungumza wakati wa kikao cha maandalizi kilichofanyika katika ukumbi wa Kili Home mjini Moshi . 
Katibu wa kamati ya maandalizi ya tukio hilo Joseph Msele akizungumza katika tukio hilo.
Mzee Akili Kawishe akifurahia jambo na baadhi ya wajumbe wa kikao hicho.
Mzee Akili Pendael Kawishe ni mzee mwenye umri wa miaka 102 akiwa na mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya tukio hilo Yunusi Mmari wakati wa kikao kilichofanyika mjini Moshi .
Baadhi ya Vikundi vya ngoma za asili vikionesha namna vilivyoanza maandalizi kwa ajili ya tukio hilo linalotaraji kufanyika mwezi ujao mkoani Kilimanjaro.


Na Dixo Busagaga, Moshi

WAZEE katika mkoa wa Kilimanjaro wakiwemo viongozi wa Mila ,Machifu na Malaigwanani wameanza mchakato wa kumpongeza na kumpa Tuzo Maalumu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi aliyofanya katika kipindi cha miaka mitano.

Katika tukio hilo wananchi wenye asili ya kanda ya kaskazini wanakusudia pia kumuomba radhi Rais Magufuli kutokana na maamuzi waliyofanya wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kwa kumpa kura chache.

Mwenyekiti wa kamati inayoratibu tuzo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tazania kutoka kwa wazee na jamii ya watu wa mkoa wa Kilimanjaro,Yunusi Mmari alisema maandalizi ya tukio hilo tayari yameaza huku yakishirikisha wazee kutoka wilaya zote za mkoa wa Kilimanjaro.

“Kusudio la tukio hili ni kuwakutanisha Wazee kutoka wilaya zote za mkoa wa Kilimanjaro na mikoa ya jirani wakiwemo Wazee wa mila kama Machifu na Malaigwanani ambao watakuwa na ujumbe maalumu wanaotarajia kuufikisha kwa Rais Dkt Magufuli”alisema Mmari .


Kwa upande wake katibu wa tukio hilo Joseph Msele alisema watu wengi wamejiandaa kushiriki huku kamati kwa kushirikiana na vyombo vingine vya serikali vikiangalia eneo kubwa zaidi la kufanyika kwa tukio hilo.

“Watu wengi wamejiandaa kushiriki katika tukio hilo ,tulikua tunafikiria kulifanyia uwanja wa Ushirika lakini kwa hesabu ambazo mpaka sasa tunazo tunaona uwanja wa ushirika mpaka sasa umejaa,hautoshi .

“Tunaendelea kuwasiliana na vyombo husika ili kuweza kuona ni eneo gani walau linaweza likakidhi hiyo population inayotarajiwa ni watu wengi san asana ,wanasubiri kwa hamu.”aliongeza Msele .

Kuhusu Shauku ya watu wa Kanda ya Kaskazini kuonana na Rais Magufuli ,Msele alisema:
“Ni kweli imekua kiu ya wengi kutamani kumpatia Mh Rais Dkt John Pombe Magufuli tuzo na sisi kazi yetu kama kamati ni kuratibu tu hayo mawazo ya wengi ili kuyafikisha kwenye kilele hicho.”alisema Msele .

Alisema wapo wazee wenye umri  zaidi ya miaka 100 wao pia wamekuwa na shauku ya kumpongeza Rais Dkt Magufuli huku akitoa rai kwa vyombo vya usafiri yakiwemo Mabasi ,Treni ,Ndege kujipanga kusafirisha wakazi wa mikoa ya kaskazini kuhudhuria tukio hilo.

“Niwaombe pia viongozi wa taasisi mbalimbali za kiserikali na ambazo sio za kiserikali wawaruhusu wakazi wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini wahudhurie tukio hili watakapo pata taarifa ya tukio hili .”alisema Msele.

Miongoni mwa Machifu walioshiriki katika kikao cha maandalizi ni pamoja na Mangi Frank Mareale pamoja na Akili Pendael Kawishe mzee wa miaka 102 wakazungumzia juu ya tukio hilo.

Tukio la Pongezi na utoaji tuzo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli linataraji kupambwa na vikundi vya ngoma za asili ambavyo vimekuwa  sehemu ya maandalizi ya tukio hilo.

No comments:

Post a Comment

Pages