July 20, 2020

MAAGIZO YA RAIS DKT MAGUFULI YAENDELEA KUTEKELEZWA

Bwawa la Kidete lililolalamikiwa na wananchi wa Kilosa Mkoani Morogoro wakati wa ziara ya Rais Dkt Magufuli Wilayani humo limebainika kusababisha maafa ya watu 17 kwa mwaka huu pekee huku yakikata huduma ya maji safi ya kunywa pamoja na kuharibu na kusomba mazao ya wananchi wa eneo hilo la Kidete na kusababisha mafuriko katika mji wa Kilosa.

Adha hiyo imebainika baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kupokea malalamiko ya wananchi na kuagiza viongozi wa serikali kufika eneo hilo la Kidete na kujionea athari zinazolalamikiwa ambapo wananchi hao wamesema Bwawa la Kidete limegeuka kuwa kero badala ya fursa baada ya kingo za Bwawa hilo kuharibika

Mara baada ya wananchi hao kutoa malalamiko yao, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi aliyeambatana na Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba kwa lengo la kutekeleza agizo la Rais, amesema malalamiko ya wananchi wa Kidete ni dhahiri na yana mashiko baada ya kujionea mwenyewe na kuwaomba wananchi hao kuwa na subira wakati serikali ikiangalia utaratibu wa kutatua kero hiyo.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba, amesema ni kweli Bwawa hilo kingo zake zimebomoka na kusababisha maafa na kuwataka wananchi hao kuitumia changamoto hiyo kama fursa pale Bwawa hilo litakapojengwa upya ili liweze kutumika kwa shughuli nyingine za uzalishaji kama vile uvuvi na kilimo cha umwagiliaji

Bwawa la Kidete lilijengwa na wakoloni wa kijerumani wakati wa ujenzi wa reli ya kati kwa lengo la kupunguza mafuriko kutoharibu miundo mbinu ya reli hiyo na kuharibika miaka ya 1990 na tangu wakati huo halijafanyiwa ukarabati jambo ambalo limesababisha maafa na adha kwa wananchi wa eneo la Kidete Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro hadi pale wananchi hao walipolalamika kwa Rais Dkt Magufuli na kuagiza ufuatiliaji wa kero hiyo ufanyike.

No comments:

Post a Comment

Pages