HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 03, 2020

WAZIRI MKUU AFUNGUA MAONESHO YA 44 YA BIASHARA

*Asema Serikali itaendelea kuviwezesha viwanda vidogo, vya kati
 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe kufungua Maonyesho  ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Nnee ya Dar es Salaam, Barabara ya Kilwa jijini Dar es salaam, Julai 3, 2020.Wengine pichani kutoka kushoto ni Naibu Waziri wa Biashara na Viwanda, Mhandisi Stella Manyanay, Waziri wa Biashara na Viwanda, Innocent BashungwaNaibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro na kuliani Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza wakati alipofungua Maonyesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya  Dar es Salaam, Barabara ya Kilwa jijini Dar es salaam, Julai 3, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama mashine ya kuranda na kuweka urembo kwenye mbao wakati alipotembelea banda la Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogovidogo (SIDO) kabla ya kufungua Maonyesho  ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya  Dar es salaam , Barabara ya Kilwa jijini Dar es salaam, Julai 3, 2020. Kulia ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa na wa tatu kulia ni Kaimu Mkurugenzi  wa Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogovidogo (SIDO), Shoma Kibende. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki na wezeshi ili kuviwezesha viwanda vidogo sana, vidogo na vya kati kukua na kufanya kazi kwa tija zaidi.

Ametoa kauli hiyo leo jioni (Ijumaa, Julai 3, 2020) wakati akifungua rasmi Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (44TH DITF) yaliyoanza Julai mosi, 2020 kwenye viwanja vya Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu ambaye amefungua maonesho hayo kwa niaba ya Rais, Dkt. John Pombe Magufuli amesema ili nchi iweze kuwa na mafanikio makubwa, taasisi za kifedha hazina budi kuweka mikakati ya kutoa huduma ya mikopo rafiki ili kuwezesha ukuaji wa viwanda kwa kuzingatia viwanda vidogo na vya kati ikiwemo vinavyoratibiwa na SIDO katika kila mkoa.

“Taswira hii ya maendeleo ya sekta ya viwanda inafanana na taswira ya maendeleo ya viwanda katika nchi karibu zote duniani. Kwa mfano, Japan, viwanda vidogo sana, vidogo na vya kati vinachukua takribani asilimia 99 ya sekta ya viwanda; Kenya asilimia 98; Malaysia asilimia 97.3; Indonesia asilimia 99.9; Canada asilimia 98 na Ujerumani asilimia 99.”

Amesema Serikali inaendelea kuimarisha sekta ya biashara na viwanda nchini ili kuchochea maendeleo ya nchi kwa ujumla. Akielezea mafanikio ya Serikali katika kipindi cha miaka mitano, Waziri Mkuu amesema: “Jumla ya viwanda vipya 8,477 vimejengwa na kuchangia kuzalisha ajira mpya 482,601… mchango wa sekta ya viwanda katika Pato la Taifa kwa mwaka 2019 ulikua kwa asilimia 8.5 ikilinganishwa na asilimia 8.05 mwaka 2018, sawa na ongezeko la asilimia 0.45.”

Amesema mchango huo, ni matokeo ya kuongezeka kwa shughuli za uzalishaji wa bidhaa viwandani nchini ambao unaendelea kuimarika na kukua vizuri. Akitoa mfano, Waziri Mkuu amesema mwaka 2019, bidhaa za viwanda zilikuwa na thamani ya sh. trilioni 10.2 ikilinganishwa na sh. trilioni 9.6 mwaka 2018 ambao ukuaji wake ni sawa na asilimia 5.8.

Kuhusu viwanda vidogo na biashara ndogo, Waziri Mkuu amesema sekta hiyo inaendelea kutoa mchango mkubwa katika pato la taifa wa wastani wa asilimia 35 kwa mwaka. “Kwa mwaka 2019/2020, jumla ya miradi 304 inayohusiana na ujenzi wa viwanda imesajiliwa ambayo inatarajiwa kuongeza jumla ya ajira 11,793.”

Amesema SIDO imeratibu na kuhudumia viwanda vidogo vipya 1,400 vinavyotoa ajira 4,200. “Sekta hii muhimu imeajiri Watanzania zaidi ya milioni tisa ikiwa ni ya pili kwa sekta za kiuchumi katika kutoa ajira baada ya sekta ya kilimo,” ameongeza. 

Amesema maendeleo ya uwekezaji katika sekta ya viwanda nchini yameongeza uzalishaji wa bidhaa mbalimbali ikiwemo bidhaa za chuma, saruji, vigae, nguo na mavazi, ngozi na bidhaa za ngozi, kusindika nyama, chakula, mbogamboga na matunda, maziwa, mafuta ya kula, sukari, vifungashio, mbolea, dawa za binadamu, sabuni na sigara pamoja na ubanguaji wa korosho.  

Kwa upande wa biashara, Waziri Mkuu amesema utekelezaji wa Blueprint for Regulatory Reform to Improve Business Environment umewezesha maboresho ya tozo 173 ambapo kati ya tozo hizo, tozo 163 zimefutwa na tozo kero 10 zimepunguzwa viwango.

“Kati ya tozo zilizofutwa, 114 ni za sekta ya kilimo na mifugo, tano ni za Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), 44 za Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka za Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), utalii, maji, uvuvi na iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).”

Amesema tozo zilizopunguzwa za GCLA, zimewezesha kuhamisha jukumu la usimamizi wa masuala ya chakula kutoka iliyokuwa TFDA kwenda TBS ili kuondoa muingiliano wa majukumu. “Maboresho hayo yamesaidia kuondoa urasimu na kupunguza gharama za kufanya biashara,” amesisitiza.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa maonesho hayo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa alisema kati ya mwaka 2015 na 2019, viwanda 8,477 vilianzishwa katika maeneo mbalimbali nchini ambapo kati ya hivyo, viwanda 201 ni vikubwa, 460 ni vya kati, 3,406 ni vidogo na 4,410 ni vidogo sana.

“Uwepo wa viwanda vyetu vya ndani, ulitusaidia hata wakati wa janga la corona tuliweza kutengeneza barakoa, mavazi ya watoa huduma, vitakasa mikono na bidhaa nyingine nyingi.”

Akisisitiza matumizi ya bidhaa zinazozalishwa nchini, Waziri Bashungwa amesema: “Hakuna soko endelevu na lenye uhakika kama soko la ndani. Kwa hiyo, wazalishaji wa ndani wazalishe bidhaa zenye ubora, na Watanzania wapende kununua bidhaa za ndani. Kwa njia hiyo, tutaimarisha soko la ndani na kulinda viwanda vyetu,” alisisitiza.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TanTrade, Dkt. Ngw’anza Kamata alisema kutokana na changamoto ya COVID 19, mwaka huu idadi ya washiriki imepungua kiasi. “Washiriki wa ndani wamepungua kutoka 3,250 hadi 2,837 wakati wa washiriki wa nje nao wamepungua kutoka 520 hadi 43,” alisema.  

No comments:

Post a Comment

Pages