July 21, 2020

Wengi wapendezwa na kura za wazi kila mtu apewe zake

Na Bryceson Mathias
WATANZANIA wengi nchini wamependezwa na utaratibu wa kura za wazi kila mtu kupewe zake uliotumika kwenye zoezi la kupiga na kuhesabu kura za maoni, wakidai ukitumika kwenye uchaguzi wa ubunge mwaka huu uchaguzi utakuwa huru na haki.
Sababu za kupendezwa na utaratibu huo zinatokana na kuonekana hauna figisufigisu za wizi wa kura au mizengwe ya aina yoyote inayopelekea wagombea na wapenzi wao kuwa na malalamiko yanayoweza kuibua uvunjifu wa Amani dhidi ya uchaguzi huo.
Aidha wakihojiwa kuhusiana na mchakato huo wananchi wengi waliohojiwa kwa nyakati tofauti kutoka katika Kata na Majimbo mbalimbali wamekiri kwamba utaratibu huo ni mzuri kama utaendana na kauli na vitendo kama alivyosema, Rais John Magufuli, kwamba wananchi wasiwe na wasiwasi Uchaguzi wa 2020 utakuwa huru na haki.
Mwanachama wa Chama cha ACT-Wazalendo mkoani Morogoro, Juma Abdalah, alisema, “Kama Kauli ya Magufuli kwamba Uchaguzi wa Oktoba 2020 utakuwa Huru na Haki alilenga kutumia utaratibu huu! Ni Hakika na hakuna ubishi uchaguzi utakuwa huru na Haki, na kutakuwa hakuna mizengwe, Malalamiko na uvunjifu wa Amani.
“Binafsi ninaamini! adha, maafa na vifo vilivyotokea huko nyuma kwenye chaguzi ndogondogo na kubwa na zilizosababisha uvunjifu wa amani, zitabaki kuwa historia na simulizi za Adamu na Hawa”. alisema Abdalah ambaye hakusita kudai uharibifu wa maisha ya wananchi.
Kada wa CCM wilayani Mvomero, Khadija Said, alisema “kwenye kura za maoni tuliona haki na usawa vikitendeka, na zama za vigogo, wakubwa na majina ya wenye uwezo, viliwekwa Kando tukashuhudia Uwanja sawa wa ushindani, na ikiwa hivyo kwenye uchaguzi Mkuu, tutaishangaza dunia”.alisema Khadija.
Mbobezi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kata ya Mvomero, Lazaro Lufunyo, ikitokea kukawa na Usawa sawa wa Ushindani wa Siasa, na Kura zikapigwa kwa Uwazi uliooneshwa na Washindani wetu CCM kwa Amani hiyo, “Basi Mwana Simba na Mwana Ng’ómbe watakuwa wananaweza kulala Zizi moja”.alisema Lufunyo akidai ni jambo litakalo washangaza walimwengu bila kufafanua.

No comments:

Post a Comment

Pages