July 21, 2020

KATIBU MKUU KILIMO ASIMAMISHA SHUGHULI ZA TAASISI YA STAWISHA

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya muda mfupi uliopita; ameagiza kusimamishwa mara kuanzia leo tarehe 21 Julai, 2020 kwa shughuli za Taasisi ya Kuendeleza zao la Viazi Mviringo (STAWISHA) ya Jijini Mbeya.

Mradi wa kuendeleza viazi mviringo unaotekelezwa na Taasisi ya STAWISHA upo ndani ya eneo la Taasisi ya Utafiti wa Kilimo, Uyole (TARI – Uyole) baada ya kujiridhisha kuwa kuna dalili za ufisadi na ukiukwaji wa makubaliano ya msingi kati ya Serikali ya Tanzania na Uholanzi ya mwaka 2018.

Katibu Mkuu Gerald Kusaya ameyasema hayo muda mfupi baada ya kuongea na Wanahabari katika Ofisi za Wizara ya Kilimo Jijini Dodoma na kubainisha kuwa Watendaji wa Taasisi ya STAWISHA wamekiuka lengo kuu la makubaliano katika ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Uholanzi.

Katibu Mkuu Gerald Kusaya ameongeza kuwa Mkataba wa makubalio (MoU) kati ya Wizara ya Kilimo (Tanzania) pamoja na mbia mwenza; Wizara ya Kilimo Chakula na Maliasili ya Uholanzi ilikuwa ni kuendesha shughuli za utafiti wenye lengo la kuongeza tija na uzalishaji wa viazi mviringo lakini Watendaji wa Taasisi ya STAWISHA hawakuwa wakiendesha shughuli za utafiti.
 
“Katika MoU hakuna neno lililotaja kuhusu kampuni ya STAWISHA na kuwa eneo wanalotumia kuzalisha mazao kwa sasa ni mali ya umma. Suala la kuomba kibali cha ujenzi ndani ya eneo la TARI Uyole na kutumia jina la STAWISHA bila kibali cha Wizara ni kosa na siwezi kufumbia macho“ alisisitiza Kusaya Mambo mengine ambayo yamekiukwa na Watendaji wa Taasisi ya STAWISHA ni pamoja kuendesha shughuli za uzalishaji wa mazao ya ngano, mahindi jambo ambalo nikinyume cha lengo la msingi.
 
Jambo lingine ni pamoja na Watendaji wa Taasisi ya STAWISHA kusajili Jina la Taasisi hiyo BRELA kwa jina la STAWISHA bila kuzingatia kuwa ni huo ni wa ushirikiano kati ya Serikali hizo mbili kupitia Wizara zao za Kilimo.

Katibu Mkuu Kusaya ameongeza kuwa STAWISHA haijajiri Mtumishi yeyote wa Wizara ya Kilimo pamoja na kutotoa hesabu zake kwa Wizara ya Kilimo na kwa Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabau za Serikali kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili kwa ajili ya ukaguzi.

“STAWISHA imefungua akaunti mbili NMB Mbalizi na watia saini wote ni Watumishi wake. Maana yake Serikali haijui kiasi gani cha fedha kimeingia kwa kipindi cha tokamwaka 2018 hadi sasa na udhibiti wake upoje”. Amesema Katibu Mkuu Kusaya.
 
Katibu Mkuu ameongeza kuwa Watendaji wa STAWISHA waliomba kibali kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ndani ya eneo la TARI Uyole huku wakijua wazi kuwa katika mkataba wa makubaliano ya Serikali hizo mbili hakuna mahali ambapo Taasisi hiyo STAWISHA imetajwa.

Kufuatia maleozo hayo Katibu Mkuu Kusaya ametoa maagizo mawili kama ifuatavyo;kwanza kwa kuwa eneo hilo la ekari 70 ni mali ya serikali amemwagiza Mkurugenzi Mkuu wa TARI Dkt.Geoffrey Mkamilo kuwasiliana na Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya kubadilisha kibali cha ujenzi kutoka STAWISHA kuwa TARI Uyole ili kuepusha mgogoro siku za usoni

Pili, kuanzia leo tarehe 21.07.2020 kampuni ya STAWISHA isimamishe shughuli zote ndani ya eneo la TARI Uyole na kuondoa mabango yake haraka kwani katika mkataba uliosaini na serikali ya Uholanzi hautambua kampuni hiyo.

Tatu, Mtendaji Mkuu wa STAWISHA aandike barua NMB Mbalizi kusimamisha akaunti zote za fedha kufanya kazi hadi pale majadiliano na Seriklai ya Uholanzi yatakapokamilika kuhusu uhalali wake.

“Mimi kama Katibu Mkuu Kilimo, nataka kupata uhalali wa STAWISHA kufanya kazi ndani ya mkataba wetu na serikali ya Uholanzi.Lengo serilaki inataka kuona manufaa yaliyolengwa kupatikana kwa zao la viazi yanafikiwa huku tukidumisha mahusiano mema na serikali ya Uholanzi” Kusaya alisisitiza.

Katibu Mkuu amesema atawasiliana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo ya Uholanzi kuhusu masuala yote yanayoendelea ndani ya makubaliano ya ushirikiano na Serikali ya Uholanzi.

No comments:

Post a Comment

Pages