August 18, 2020

ACT-Wazalendo watambulisha timu ya ushindi

Mwenyekiti wa timu ya kampeni ya ACT–Wazalendo, Joram Bashange.
 Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.

 
Na Mwandishi Wetu

CHAMA Cha ACT-Wazalendo leo kimetambulisha rasmi viongozi wa timu ya kampeni ya kitaifa kuelekea uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28/2020.

Timu hiyo ya ushindi imetambulishwa na Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe leo Agosti 18, 2020 jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari.

Katika kikao chake na waandishi wa habari katika Ofisi za chama, Magomeni Dar es Salaam, Zitto aliwataja wajumbe wa timu hiyo ni Mwenyekiti wa Timu ya kampeni ya ACT–Wazalendo kuwa ni Joram Bashange ambaye  ni Naibu Katibu Mkuu Bara pamoja na Mjumbe wa Kamati Kuu, Wakili Emmanuel Lazarus Mvula ambaye  atakuwa Meneja wa kampeni Taifa.

Pia katika mkutano huo na waandishi wa habari, kiongozi wa chama amezungumzia matukio ya utekwaji, kupigwa na kujeruhiwa kwa wanachama na wagombea waliotia nia katika nafasi ya ubunge na udiwani ndani ya chama cha ACT- Wazalendo katika Jimbo la Ruangwa mkoani LIndi.

Aliwataja wahanga wa matukio hayo kuwa ni Said Ally Nangendekwa ambaye alipigwa na kujeruhiwa nyumbani kwake Agosti 9 2020.

"Mwingine ni Joakim Ng’ombo ambaye alitekwa, kupigwa Agosti 12 na kuokotwa wilayani Mkuranga mkoani 
Pwani Agosti 13 akiwa na hali mbaya ambapo awali alitibiwa katika Hospitali ya Temeke na sasa amehamishiwa Hosptali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) baada ya hali yake kuzidi kuwa mbaya zaidi.

Mtu wa tatu ni Bakari Abdallah Nanyambo ambaye ni mgombea udiwani wa ACT- Wazalendo alishambuliwa kwa mapanga na watu wasiojulikana ambapo hivi sasa anaendelea na matibabu katika Kituo cha Afya Mbekenyera mkoani Lindi," alisema.

Alisema matukio haya yote yameripotiwa katika vituo vya polisi mkoani humo.

Zitto alisema kutokana na matukio hayo,  anaomba yafuatayo yazingatiwe: Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ifuatilie kwa karibu na kutolea ufafanuzi matukio haya kama ni ya kisiasa basi ikemee na kuchukua hatua.

Aidha, amewataka wanachama wa ACT- Wazalendo wachukue hatua za kujilinda, kulinda viongozi wao na mali za 
chama.

"Chama kinawaagiza wanachama wote kufuata taratibu za kisheria wakati wote kuelekea Uchaguzi Mkuu na pale wanapoona haki zao au haki za wengine zinavunjwa watetee na kuzuia uvunjwaji  wa haki kwa kuripoti matukio hayo mahali panapohusika," alisema.

No comments:

Post a Comment

Pages