August 18, 2020

Bei elekezi, mfumo mpya wa usajili vyakwamisha miradi vijiji vya USMJ

Mwekahazina wa Kikundi cha Wakata Mkaa Happiness Mapunda akielezea waandishi wa habari namna wanavyotumia msiti kwa njia endelevu.

Waandishi na wanakijiji wa Kijiji cha Kitunduweta wakiwa ndani ya msitu wa kijiji unaohifadhiwa kwa njia USMJ.
Ofisa Sera na Majadiliano wa MJUMITA, Elida Fundi akielekea msituni katika kijiji cha Kitunduweta kujionea namna uhifadhi unavyotekelezwa.

 

Na Suleiman Msuya

 

WANAVIJIJI wanajishughulisha na Usimamzi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (UMSJ), wamesema bei elekezi iliyotolewa na Serikali katika biashara ya mkaa na kubadilika kwa mfumo wa usajili kuhusu biashara hiyo umechangia miradi mingi kusimama.

Kauli hizo zimetolewa mbele ya waandishi wa habari hivi karibuni na wanavijiji ambao wanajihusisha na uvunaji endelevu wa rasilimali misitu katika vijiji vya Msolokelo, Matuli, Ulaya Mbuyuni na Kitunduweta vilivyopo wilaya za Morogoro, Mvomero na Kilosa mkoani Morogoro

Waandishi wa habari kutoka vyombo vya habari mbalimbali walitembelea vijiji hivyo kujionea namna USMJ kupitia Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS) chini ya uratibu wa Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) na Mtandao wa Usimamizi wa Misitu ya Jamaii Tanzania (MJUMITA) kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswis (SDC).

Jumanne Omary Mkazi wa Kijiji cha Msolokelo wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, alisema mradi wa TTCS umeweza kubadilisha maisha ya wananchi na kijiji kupata maendeleo hivyo unapaswa kuendelezwa ila changamoto anayoiona ni mfumo mpya wa usajili ili kupata kibali cha kuvuna mazao ya misitu.

Omary alisema mbaya zaidi mabadiliko hayo ya uvunaji yamekuja bila kuwashirilisha jambo ambalo limekwamisha mipango yao mingi.

"Sio kwamba tunapinga mfumo mpya ila kusema kweli haukuwa shirikishi hali ambayo imesimamisha mipango yetu ambayo tulijiwekea kwa mwaka 2019/2020, nadhani wahusika wanatakiwa kutafakari upya," alisema.

Alisema mwanya huo wa kuwanyima kupanga mipango ya uvunaji katika ngazi ya kijiji inaweza kuchochea uharibifu mkubwa wa misitu hivyo ni vema mamlaka husika kurejea mfumo wa zamani.

Omary alisema pamoja na manufaa ambayo wamepata bado kuna changamoto ambazo zinasababishwa na vijiji jirani vya Digarama, Masimba na Gonja ambao wanavamia misitu yao na kuharibu.

Alisema iwapo hakutakuwa na hatua za haraka kudhibiti wavamizi na kubadili mfumo vijiji vyao havitahusika na uchumi wa kati unaozungumziwa.

Kwa upande wake Sadick Kondo wa Kijiji cha Matuli, Kata ya Matuli wilayani Morogoro, alisema mfumo huo umesimamisha shughuli za uvunaji jambo ambalo linawarudisha nyuma kimaendeleo.

Kondo alisema mwamko wa ulinzi na usimamizi wa misitu ya asili kijijini unaanza kushuka baada ya mabaliko hayo ya mfumo wa usajili na bei elekezi.

"Tulishajenga imani moja kuwa misitu ni uhai wetu, tuitunze, tuitumie kiendelevu lakini kwa hali ilivyo naona dalili mbaya tunapaswa kuchukua hatua mapema," alisema.

Naye Happiness Mapunda Mwekahazina wa Kikundi cha Wakata Mkaa Kitunfuweta, Kata ya Muhenda wilayani Kilosa, alisema  dhana ya usawa iliashaanza kuonekana kijijini kwao lakini inaweza kurejea kwa kuwa wananchi watakosa nguvu ya usimamizi wa misitu kwa kuwa hawana mamlaka kupanga matumizi na bei.

Kulangwa Ganda Katibu wa Kikundi cha Wakata Mkaa kijiji cha Kitunduweta, Kata ya Muhenda wilaya ya Kilosa alisema haoni sababu ya Serikali Kuu kuchukua jukumu la kupanga bei kwani wanaoumia ni wao.

Ganda alisema kupanga bei moja kwa nchi nzima kutanufaisha baadhi ya waandishi huku kundi kubwa likiathiriwa. 

"Sio ni mantiki ya kupanga bei elekezi ya mkaa kuwa shilingi 12,500 nchini kote wakati kuna changamoto za usafiridhaji na zingine nyingi ambazo zinahitaji ufumbuzi kwanza," alisema

Wakizungumzia mfumo na bei elekezi Maofisa Misitu na Maliasili wa wilaya hizo walisema zipo faida na hasara hivyo wao watajikita kwenye hasara ili kuenda sawa na wanavijiji wanaotekeleza USMJ kwa vitendo.

John Mtimbanjayo Ofisa Maliasili wa Wilaya Kilosa, alisema utulivu wa wilaya ya Kilosa ni moja ya matunda chanya ya USMJ hivyo watahakikisha wanapigania changamoto hizo zinapata majibu sahihi.

Naye Edward Kimweri alisema Jamii inapaswa kujikita kwenye uhifadhi matokeo makubwa na kuachana na hasara ambazo zimekuwa zikiwakwamisha.

Ofisa Uhusiano wa TFCG, Bettie Luwuge alisema wao wameamua kujikita kwenye uhifadhi wakiamini kwa ni eneo rahisi kuchochea maendeleo.

Luwuge alisema mradi wa mkaa endelevu kuhakikisha kuwa Misitu ipo salama ma mazingira kwa kila jambo.

No comments:

Post a Comment

Pages