August 18, 2020

Benki ya NMB yatangaza neema kwa wachimbaji wadogo

 Benki ya NMB imetenga shilingi bilioni 32 kwa ajili ya mikopo kwa wachimbaji wadogo nchini. Akizungumza jijini
Mwanza wakati wa kongamano la wafanyabiashara ‘NMB Business Club’, Mkuu wa idara ya Biashara wa Benki
hiyo - Alex Mgeni alisema kutolewa kwa mikopo hiyo ni matokeo ya maboresho ya sheria na sera kwenye sekta ya
madini yanayofanywa na serikali kwa lengo la kuongeza tija.


 “Mikopo hiyo ambayo imeanza kutolewa tangu Januari, mwaka huu inahusisha gharama za kununua vifaa vya uchimbaji ikiwemo mitambo na magari ya kubebea mchanga wa madini migodini,” alisema Alex.

Mkuu wa Idara ya Biashara wa Benki ya NMB - Alex Mgeni, akizungumza kwenye kongamano la biashara (NMB Business Club) Jijini Mwanza lililoratibiwa kwa ajili ya kuwafunda wafanyabiashara zaidi ya 200 kuhusu huduma za kifedha na faida za kutumia huduma za benki hiyo.
 

Kuhusu madhara ya janga la corona kwa sekta ya biashara, Mgeni alipongeza juhudi za Serikali zilizofanikisha kutokomezwa kwa ugonjwa huo uliosababisha changamoto katika mfumo wa biashara na uwekezaji. Alisema kutokana na mifumo ya biashara kupata changamoto, NMB iliwasaidia wateja wake ambao biashara zao ziliathirika zaidi, hasa wale wa sekta ya utalii.


“Kila mfanyabiashara aliyepata changamoto na kutifikia tulizungumza naye kutafuta namna ya kumsaidia. Wapo waliopunguziwa viwango vya marejesho na wengine marejesho yao yalisimamishwa kwa muda, hasa wale wa sekta ya utalii walioathirika zaidi,” alisema. 

Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa - Baraka Ladislaus, akipata maelezo kutoka kwa msindika mvinyo - Rose Stephen, kwenye kongamano la wafanyabiashara Jijini Mwanza.


Akizungumzia NMB Business Club, Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa - Baraka Ladislaus alisema kongamano hilo
linatoa fursa kwa benki kusikiliza, kupokea na kufanyia kazi hoja za wateja.


“Kupitia hoja na mrejesho kutoka kwa wateja wetu wakiwemo wafanyabiashara, NMB tunapata fursa ya kuboresha huduma na bidhaa zetu,” alisema Ladislaus.


Mfanyabiashara, Contilda Magweti wa jijini Mwanza alisema licha ya kuwakutanisha pamoja wafanyabiashara, kongamano hilo la kila mwaka katika maeneo mbali mbali nchini pia huwapa fursa ya kukutana na kujadiliana uso
kwa uso na viongozi na watendaji wa Benki.


“Kwa kukutana pamoja tunapata fursa ya kujadiliana na kubadilishana uzoefu kibiashara; NMB iangalie
uwezekano wa kongamano hili kufanyika angalau mara mbili kwa mwaka,” alisema Magweti.


Aliwashauri wafanyabiashara na wajasiriamali wenzake kuendelea kusaidiana maarifa ya kutafuta masoko ya
bidhaa zao kwa pamoja.

No comments:

Post a Comment

Pages