NA ASHA MWAKYONDE
CHAMA cha Wananchi CUF kimezindua mpango maalumu wa kukisaidia chama hicho ambapo kila mwanachama atachangia Sh.100 lengo likiwa ni kukidhi mahitaji ya kampeni katika kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Agasti 29, Mgombea wa Urais na Mwenyekiti wa Chama hicho Profesa Ibrahimu Lipumba amesema fedha zitakazopatikana zitasaidia katika kampeni za madiwani, wabunge, urais pamoja na kuwalipa wakala wao.
Prof. Lipumba amesema ruzuku inatotoka serikali haiwezi kukidhi mahitaji hivyo kila mwanachama achangie kiasi cha Sh. 100 kila siku kwa kipindi cha miezi miwili.
"Hiki ni chama cha wananchi na kinategemea wananchi wenyewe, tunatafuta ukombozi na ni sisi ndio tutakao leta ukombozi," amsema Prof. Lipumba.
Ameongeza kuwa wanaingia katika uchaguzi huo kwa lengo la kushinda kiti cha urais 2020 na kupata serikali ambayo ina haki na usawa kwa watu wote.
Awali akiwasilisha mpango huo Mkurugenzi wa uchumi na mpango Taifa wa chama hicho Juma Kilagai amesema chama kinahitaji rasilimali watu ili kiweze kukidhi mahitaji yake.
"Kwa sasa mapato ya chama ni madogo kwa sababu chanzo chake ni kimoja tu amacho ni ruzuku inayotolewa na serikali kupitia msajili wa vyama vya siasa ni ndogo ikilinganishwa na mahitaji ya chama," amesema.
Aidha amewaomba wananchi kujitolea zaidi kuchangia chama hicho ili kiweze kufanikisha azima yake ya kushika dola.
No comments:
Post a Comment