August 22, 2020

MKUU WA MKOA WA PWANI ATOA SIKU SABA KUKAMATWA KWA MFUGAJI ALIYEMBAKA BIBI KIZEE MKULIMA

VICTOR MASANGU, RUFIJI

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo ametoa muda wa siku saba kukamatwa kwa mfugaji mmoja kwa tuhuma za kutenda kosa la kumbaka bibi  mmoja  anayekadiriwa  kuwa na zaidi ya miaka 60 akiwa shambani kwake  nyakati za usiku kwa ajili ya kulinda mazao yake yasiliwe na mifugo  na kumsababishia maumivu  makali  kwa  kile kinachodaiwa ni kuwepo kwa migogoro  kati ya wakulima na wafugaji.

Ndikilo ametoa kauli hiyo wakati akizungumza  katika mkutano wa hadhara na baaadhi ya wananchi wa kata ya Mkongo iliyopo Wilayani Rufiji ikiwa ni katika mwendelezo wake wa ziara ya kikazi yenye lengo la kutembelea miradi mbali mbali  ya maendeleo pamoja na kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili wananchi ili kuweza kuzifanyia kazi ambapo ameambatana na kamati ya ulinzi na uslama ya Mkoa.

“Mkuu wa Polisi hiki kitendo alichofanyiwa huyu mama ni kitendo cha kinyama sana na mimi naagiza kwamba natoa muda wa siku saba tu yani wiki moja huyo mtuhumiwa ambaye amefanya kitendo cha kubaka akamatwe mara moja ili sheria iweze kufuata mkondo wake kwani haiwezekani mambo kama haya yafanyanyika na jeshi la polisi lipo tuu hakamatwe mara moja,”alisema Ndikilo.

Aidha Ndikilo alisema kwamba serikali yake ya Mkoa wa Pwani kamwe haiwezi kufumbia macho mambo kama hayo kwa wananchi kufanyiwa vitendo vya kikatili na kwmaba wale wote ambao watabainika kuhusika katika matukio mbali mbali kama hayo watakamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria ili iwe fundishi kwa wengine.

Katika hatua nyingine Ndikilo amewataka watendaji wa vijiji pamoja na wenyeviti wa vijiji ambao watakuwa wazembe katika kushughulikia migogoro ya wakulima na wafugaji kwa kipindi cha mwezi mmoja endapo akiona bado kunaendelea migogoro ya ardhi ameahidi kuwashughulikia mara moja na kuwataka wajiondoe kabisa katika nafai hizo ili wachaguliwa viongozi wengine ambao wanawajali wananchi.

Kwa upande wake Bibi huyo aliyejulikana kwa jina la Tatu Lupamba  ambaye alifanyiwa kitendo hicho cha ukatili wa  kubakwa ametoa kilio chake Kwa Mkuu wa Mkoa ambapo amedai kuwa alifanyiwa kitendo hicho mwezi wa sita mwaka huu wakati akiwa shambani kwake na mfugaji mmoja ambaye hakuweza kumfahamu kwa sura na kuiomba serikali kuingilia kati sakata hilo.

Akizungumzia kuhusu tukio hilo la ubakaji  Mkuu wa Polisi kituo cha Polisi Wilaya ya Rufiji Wilbert  Siwa amekiri mbele ya wananchi kuwa ni kweli taarifa hizo limesharipotiwa na kwamba tayari wameshafungua jalada na kwamba wanaendelea na uchunguzi ili kuweza kumbaini muhusika ili aweze kuchukulia hatua za kisheria .

“Ni kweli tukio hili Mkuu wa Mkoa la mama huyo tulilipata na kwamba tumeshaanza kulishughulikia na lilitokea tarehe 28 ya mwezi wa  sita ambapo mama huyo alikukuja kutoa malalamiko yake ya kwamba amebakwa na mtu mmoja ambaye ni mfugaji wa jamii ya kisukuma na sisi tumelichukua na  bado tunaendele na upelelezi kwa kuwa mtu anayetuhumiwa ajajuliakana,”alisema Siwa.

Pia katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Polisi alisema kwamba wataendelea kuimarisha ulinzi kwa wananchi katika maeneo mbali mbali ya Wilaya ya Rufiji na kwamba  lengo lao kubwa ni kuhakikisha wanadumisha hali ya ulinzi na usalama na kwamba mtuhumiwa aliyefanya kosa hilo bado anaendelea kutafutwa.

Wilaya ya Rufiji iliyopo Mkoa wa Pwani katika baadhi ya maeneo yake  bado yanakabiliwa na changamoto kubwa ya kuwepo kwa migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo kwa kiasi kikubwa inasababishwa na wenyeviti wa vijiji na vitongoji hali ambayo wakati mwingine inapelekea kuwepo kwa mapigano ambayo yanasababisha  hali ya uvunijfu wa amani.


Mkuu wa Mkoa wa Pwani  Mhandisi Evarist Ndikilo kushoto akizungumza na  baadhi ya wananchi wa Kata ya Mkongo iliyopo Wilayani Rufiji wakati wa mkutano wa hadhara ikiwa ni ziara yake ya kikazi kwa ajili ya kugagua miradi mbali mbali ya maendeleo pamoja na kuwasikiliza wananchi changamoto zao zinazowakabili kulia kwake ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani. (Picha zote na Victor Masangu).


Mkuu mpya wa Wilaya ya Rufiji Luteni Kanali Patrick Sawala kulia akizungumza na wananchi wa kata ya Mkongo kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo wakati wa mkutano wa hadhara ambao ulifanyika katika kituo cha afya cha Mkongo.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo (katikati), akiwa  wameketi na viongozi mbalimbali wa serikali ambapo kulia kwake ni Katibu Tawala mpya wa Mkoa wa Pwani ambapo kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Rufiji wakati wa mkutano huo wa kujadili na kuskiliza kero za wananchi.

Baadhi ya wananchi wa Wilayani Rufiji ambao wamefurika katika mkutano wa hadhara kwa ajili ya kumsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikiloi hayupo pichani katika ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi mbali mbali ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi.

Umati wa wananchi wa Wilaya ya Rufiki kutoka maeneo mbali mbali wakiwa wametulia na kumsikiliza kwa umakini Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist ndikilo hayupo pichani wakati wa mkutano wa hadhara ulioandaliwa kwa ajili ya kusikiliza kero mbali mbali za wananchi ili kuweza kuzitafutia ufumbuzi.

No comments:

Post a Comment

Pages