August 31, 2020

Msajili Msaidizi BRELA na wengine wanne kizimbani kwa kudaiwa kutakatisha USD 300,000


NA JANETH JOVIN


WATU watano akiwamo Msajili Msaidizi wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Noel Shani (44), wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka mbalimbali yakiwemo ya kughushi na kutakatisha Dola za Marekani 300,000.

Washtakiwa hao walisomewa mashtaka yao leo Agosti 31,2020 katika Mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rashid Chaungu.

Akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon aliwataja washtakiwa mbali na Shani kuwa ni Mohammed Nur (48) raia wa Afrika Kusini, Umulkher Mohammed (34) raia wa Somalia , wote wafanyabiashara.

Washtakiwa wengine ni  Mfanyakazi wa Benki, Alex Ndondole (33) na mshtakiwa wa mwisho mfanyakazi wa benki Emma Chikaonda ambaye hakuwepo mahakamani.

Katika shtaka la kwanza washtakiwa wote wanadaiwa kati ya Machi 2011 na Mei 30, 2016 Dar es Salaam, walikula njama kufanya udanganyifu wa kujipatia fedha kwa udanganyifu.

Shtaka la pili mshtakiwa wa kwanza na wapili, wanadaiwa kughushi maamuzi ya bodi ya Kampuni ya Alliance Cargo Handling ltd ya February 8,2014 kuonesha Kampuni hiyo imekubaliana kufungua akaunti katika Benki ya Equity tawi la Prestige wakati si kweli.

Shtaka la tatu kughushi mshtakiwa wa kwanza na pili, Aprili 12,2015 wanadaiwa kughushi maamuzi ya bodi ya Aprili 12 2015 wakionesha kwamba bodi imekubali kufungua akaunti Benki ya Amana tawi la Nyerere Road.

Wankyo alidai shtaka la nne kwa mshtakiwa wa kwanza, anadaiwa kughushi , Aprili 18 mwaka 2011 alighushi barua kuonesha imetolewa na Brela kwa kuonesha kwamba Mohammed ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Alliance huku akijua si kweli.

Alidai katika shtaka la tano mshtakiwa wa kwanza na pili, wanadaiwa kughushi maamuzi ya bodi ya Machi 5, 2016 wakionesha Kampuni ya Alliance inabadili jina kutoka Alliance Cargo kwenda Africa Flight Service Tanzania wakati si kweli.

"Shtaka la sita Februari 8, 2014 mshtakiwa wa kwanza aliwasilisha nyaraka ya uongo ya maamuzi ya bodi kuonesha kwamba wamekubali kufungua akaunti Equity benki.

"Katika shtaka la saba mshtakiwa huyo aliwasilisha nyaraka  Amana benki kuonesha kampuni imekubaliana kufungua akaunti.

"Mshtakiwa anadaiwa kiwasilisha Brela  nyaraka kuonesha wamekubaliana kubadilisha jina la kampuni,"alidai Wankyo.

Alidai katika shtaka la tisa, inadaiwa Februari 10,2014 maeneo ya Equity Benki , mshtakiwa wa kwanza na pili kwa nia ya kufanya udanganyifu katika akaunti ya Kampuni ya Cargo iliyopo Equity , kwa udanganyifu walichukua mkopo wa Dola za Marekani 300,000.

Katika shtaka la kumi mshtakiwa wa nne na tano, wanadaiwa kushindwa kuzuia kosa kutendeka , wakiwa maafisa wa benki ya Equity.
.
Wankyo alidai shtaka la 11, mshtakiwa tatu akiwa Msajili Msaidizi Brela anadaiwa kushindwa kuzuia uhalifu, shtaka la 12 kutakatisha  linamkabili mshtakiwa 1 na 2 na Shtaka la 13 washtakiwa wote wanadaiwa kutakatisha Dola za Marekani 300,000.

Washtakiwa hawakutakiwa kujibu lolote sababu Mahakama hiyo haina Mamlaka ya kusikiliza shauri hilo la Uhujumu Uchumi.

Wankyo aliomba washtakiwa warudi Polisi kwa sababu hawajapimwa Corona, mahakama ilikubali, washtakiwa walirudi Polisi kwa ajili ya vipimo, kesi itatajwa Septemba 7 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

Pages