August 31, 2020

Taasisi ya Uongozi yazindua mafunzo, Viongozi vijana watakiwa kuacha tabia ya kujiona wanajua kila kitu


Washiriki wa mafunzo ya uongozi ngazi ya cheti yanayotolewa na Taasisi ya Uongozi, wakiwa katika ufunguzi wa mafunzo hayo.


Washiriki wa mafunzo ya uongozi ngazi ya cheti yanayotolewa na Taasisi ya Uongozi, wakiwa katika picha  ya kumbukumbu.

 

NA JANETH JOVIN

VIJANA walioshika nafasi mbalimbali za uongozi nchini wametakiwa kuacha tabia ya kujiona wanaelewa na kujua kila kitu badala yake wametakiwa kujishushe ili iwe rahisi kwa watu wengine kwenda kuwashauri.

Hayo yamebainishwa leo Agosti 31,2020 jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Dk. Laurean Ndumbaro wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya uongozi ngazi ya cheti yanayotolewa na Taasisi ya Uongozi kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Aalto Executive Education cha nchini Finland.

Dk. Ndumbaro amesema kiongozi anaejiona anaelewa kila kitu si mtu ambaye anajiamini na kuongeza kuwa tabia hiyo ufanya baadhi ya watu kushindwa kuwashauri.

"Kiongozi mzuri anapaswa kujishusha na muda wote awe mtu wa kujifunza ili iwe rahisi watu wengine kufika ofisini kwake na kumshauri, pia anapaswa kutambua jamii nyingi ni maskini hivyo asifanye mambo yatakayomfanya ashindwe kujua  wananchi wake wanashida gani," amesema

Hata hivyo Dk. Ndumbaro amesema kiongozi anapaswa kujiamini lakini atakuwa hivyo kama atafahamu  changamoto za wananchi wake na mambo anayotaka kuyafanya kwa maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Naye Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Uongozi, Profesa Penina Mlama amesema bado nchi anakabiliwa na changamoto ya wanawake kutoshika nafasi za juu za uongozi hivyo ni wajibu wa vijana waliopata nafasi za uongozi kushirikiana kuhakikisha wanalitatua tatizo hilo.

"Tutaweza kulitatua tatizo hilo kama wanawake waliopata nafasi za uongozi watatoa fursa kwa wenzao ili kuwepo kuwa uwiano sawa  na kujiuliza kuwa watafanya nini kuhakikisha wanawainua wanawake wenzao, nina imani mambo haya yatawezekana na kwa pamoja tutalijenga taifa letu," amesema.

Awali akifungua mafunzo hayo, Katibu Mkuu Ikulu, Dk. Moses Kusiluka amesema mafunzo hayo ni ishara ya kuunga juhudi za maendeleo nchini.

Amesema mafunzo hayo amefahamishwa kuwa  yanalenga kuimarisha uwezo wa viongozi katika  
Kufanya maamuzi ya Kimkakati, kuongoza rasilimali watu na nyingine, na
Kujenga Sifa Binafsi za Kiongozi.

"Bila shaka haya ni maeneo muhimu katika safari yetu ya kuimarisha utawala bora ili kuleta maendeleo endelevu nchini.Nawaomba mtakaopatiwa mafunzo haya mjitathmini vyema na kutumia programu hii kujijenga pale mnapopungukiwa," amesema

Naye Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Kadari Singo amesema mafunzo hayo ni progamu ya miezi sita yenye moduli tatu na yanawalenga viongozi chipukizi na waandamizi wanaofanya kazi katika taasisi mbalimbali barani Afrika.

"Programu hii inatoa fursa kwa viongozi hususan wanawake ya kurudi nyenzo mpya za kiuongozi, kupata mbinu za uongozi wa kimkakati na kuwa mawakala wa mabadiliko," amesema Singo

Aidha amesema asilimia 54 ya washiriki waliopo kwenye programu hiyo ni wanawake waliopo katika ngazi mbalimbali za utawala na uongozi na kuongeza kuwa mafunzo hayo yatatolewa kwa njia ya mtandao.

"Fursa ya mafunzo kwa njia ya mtandao imeiwezesha Taasisi ya Uongozi kutumia njia za kiufundi zinazohakikisha mafunzo yanatolewa na kuwafikia walengwa na masafa marefu, taasisi imeongeza kasi katika mkakati wake wa mapinduzi ya kidijitali ili kuwafikia wateja na wadau wengi ndani na nje ya nchi kwa njia za kisasa," amesema

No comments:

Post a Comment

Pages