August 22, 2020

NDONDO CUP YAZIDI KUPAA

*KCB Bank yamwaga udhamini mnono

*Sasa kuonekana mubashara kimataifa kupitia PlusTV ndani ya DStv

 

Dar es Salaam – Ijumaa Agosti 21, 2020; Michuano maarufu ya mpira wa miguu – Ndondo Cup ambayo imeanza kutimua vumbi mwezi huu imechukua sura mpya baada ya benki maarufu nchini KCB kutangaza kudhamini mashindano hayo.

 

Akizungumza wakati wa kutangaza udhamini huo ambapo benki hiyo inatoa shilingi milioni 50, Mkurugenzi Mtendaji wa KCB Cosmas Kimario  amesema kuwa benki hiyo imeamua kudhamini mashindano hayo kwani yamekuwa ni chimbuko la vipaji vya wanasoka vijana hapa nchini. Amesema kuwa kutokana na mafanikio ya mashindano hayo katika kukuza na kuibua vipaji ndiyo sababu wameamua kudhamini mashindano hayo ili yaweze kuwa ya kiwango cha juu zaidi na hatimaye kuweza kuzalisha wachezaji wazuri na mahiri ambao wanaweza kuchezea timu kubwa za ndani nan je n ahata timu ya taifa.

 

“Tumeona jinsi ambavyo mashindano haya mbali na kuwa burudani kwa wakazi wa Dar es Salaam, lakini pia limekuwa chimbuko la wachezaji wenye vipaji. Kwa hiyo tumeona kuwa tukishirikiana na waandaaji, tunaweza kuyafanya mashindano haya kuwa makubwa na bora zaidi na hivyo kuleta faida kubwa kwa soka la Tanzania” alisema Kimario

 

Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa KCB Bank imekuwa mbia muhimu katika michezo hapa nchini na wanatarajia kuwekeza zaidi ili kuongeza mchango wao kwa maendeleo ya jamii. “Mbali na biashara yetu ya msingi ambayo ni kutoa huduma bora za benki kwa watanzania, pia tumewekeza sana kwenye miradi ya kijamii ikiwemo  kukuza michezo hapa nchini”.

 

Huu ukiwa ni mwaka was saba tangu kuanza kwa mashindano hayo yanayoandaliwa na Clouds Media Group, tayari Ndondo Cup imekuwa na mafanikio makubwa ikiwemo kutoa wachezaji zaidi ya 100 ambao wameingia mikataba na vilabu vya kimataifa huku wengine wengi wakicheza hapa nchini katika ligi mbalimbali ikiwemo ligi kuu.

 

Mratibu wa michuano hiyo Shafi Dauda amesema kutokana na udhamini huu wa KCB na kwakuwa sasa michuano hiyo inaonekana mubashara kuitia PlusTV ndani ya kisimbuzi cha DStv, bila shaka umaarufu wa mashindano hayo utaongezeka kwani sasa yataonekana hadi nje ya nchi ambapo DStv inaonekana.

 

“Kwa kweli udhamini huu wa KCB Bank pamoja konyeshwa kwa michuano hii mubashara kwenye DStv kupitia PlusTV kutayafanya yaonekana kwenye nchi mbalimbali hivyo kuongeza wigo wa wachezaji wetu kuonekana na kuongeza uwezekano wa wachezaji kupata fursa za kuchukuliwa na vilabu vikubwa ndani nan je ya nchi. Hiki ni kitu kikubwa sana hususan kwa ukuaji wa soka hapa nchini” alisema Dauda.

 

Mkurugenzi wa PlusTV Ramadhani Bukini, amesema wamejipanga vizuri kuwapa watanzania na Ulimwengu kwa ujumla burudani ya Ndondo Cup. “Tunaona fahari kubwa sana kuwa wabia wa mashindano haya na kama mnavyojua, Plus TV tunaonekana katika mataifa mengi ya Afrika kupitia DStv hivyo tunawapa fursa wapenda soka kushuhudia michuano hii mubashara” alisema Ramadhani.

 

Mkurugenzi Mtendajiwa wa MultiChoice Tanzania Jacqueline Woiso amesema kwa muda mrefu mashindano ya hapa nchini yamekuwa hayaonekani nchi za nje kitendo ambacho kinazorotesha ukuaji wa michezo hapa nchini. “tunafahamu wazi kuwa wachezaji wakiwa uwanjani ni sawa na kuwa sokoni kuuza uwezo na vipaji vyao, sasa kama michezo hiyo haionekani kimataifa, watu wan je wataonaje na kujua uwezo wa wachezaji wetu?”

 

Jacqueline amesema kwa michuano hiyo kuonekana kupitia PlusTV ndani ya DStv ni suala la watanzania kujivunia kwana halitatangaza soka la Tanzania tu, bali pia kuitangaza nchi kwa ujumla. “Kitendo cha soka letu la Tanzania kuonyeshwa nje ya nchi yetu kupitia chanel yetu ya Tanzania ni kitu cha kujivunia na bila shaka kutokana na hatua hii pamoja na udhamini huu wa KCB Bank , sasa michuano hii itakuwa na hadhi kubwa zaidi na itavutia watazamaji na mashabiki kutoka kote barani Afrika” amesisitiza Jacqueline.

 

Michuano ya Ndondo Cup 2020 itaendelea kwa miezi miwili na inashirikisha timu 34 ambazo zitacheza katika mzunguko wa kwanza, kisha timu 16 zitaingia mzunguko wa pili kabla ya kuingia robo fainali timu 8, nusu fainali timu 4 na fainali itakayowakutanisha wababe wa ndondo cup 2020.

 

Michuano hii imekuwa na muamko mkubwa sana ambapo maelfu ya washabiki huhudhuria michezo hiyo inayojumuisha timu kutoka maendeo yote ya jiji la Dar es Salaam. Michezo hiyo huchezwa katika viwanja vya Mwalimu Nyerere, Urafiki na Bandari.

 

No comments:

Post a Comment

Pages