HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 12, 2020

Asilimia 80 ya uharibifu wa misitu hufanyika katika ardhi za vijiji

Na Ghisa Abby,Lindi

Afisa toka Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) Shaban Mafita ameeleza kuwa asilimia 80 ya uharibifu wa misitu nchini hufanyika katika ardhi za vijiji na shughuli kubwa inayofanya uharibifu huo ni kilimo cha kuhama hama ambapo hekta 17.6 milioni za misitu zilizopo kwenye ardhi hizo za vijiji bado hazijarasimishwa kisheria.

Aidha afisa huyo amesema hekta 1.4 milioni pekee ndizo zilizorasimishwa huku hekta 3 milioni kati ya hekta hizo 17.6 zipo kwenye halmashauri za serikali za mitaa.

Ameeleza hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya kuutambulisha mradi wa Haki katika Misitu awamu ya pili wenye lengo la kampeni ya misitu kwa kila kijiji na hiyo ni baada ya kuona kuwepo kwa changamoto zinazotokea kwenye usimamizi shirikishi wa misitu ambayo inasimamiwa TFCG pamoja na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA).

Mafita amesema wakati Tanzania ikiwa na hekta 48.1 milioni sawa na asilimia 54.4 ya maeneo Tanzania bara, misitu inayohifadhiwa katika ardhi za vijiji ni hekta 22 milioni.

“Shughuli za uanzishwaji wa mashamba kupitia kilimo cha kuhama ndizo zimekuwa zikifanya uharibifu wa mazingira na hii ni takwimu kwa mujibu wa ripoti ya Nafoma na kwa kiasi kikubwa zinaonyesha kuwa hekta 460,000 zinaharibiwa kila mwaka na kwa kiasi kikubwa eneo hilo linatokana na kutorasimishwa hasa maeneo ya vijiji,”amesema Mafita.

Amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine katika masuala ya Misitu lazima itoe kipaumbele kwenye misitu ambayo haijarasimishwa ili iweze kurasimishwa na vijiji vinavyofanya usimamizi shirikishi ya misitu kwa pamoja isimamiee kwani imekuwa na manufaa kwa jamii kwa kupata mapato kupitia usimamizi na uvunaji endelevu ambao unafanyika kupitia utatibu wa uvunaji wanaouanzisha katika maeneo yao, ikiwa ni pamoja na fedha wanazozipata kufanyia shughuli za maendeleo kama ujenzi wa shule,madarasa na kupata bina za afya.

“Faida hizi za misitu tunataka kupeleka mbali kuona kwamba ile misitu ya hekta 17.6 milioni na yenyewe inasimamiwa katika utaratibu ili kunusuru misitu kuendelea kuharibiwa katika namna ambayo inaonekana kama uchomaji wa mkaa, uvunaji mbao na ukataji miti kiholela,”amesema.

Mafita amesema kampeni hiyo  isiishie kwa viongozi wa kiserikali lakini viongozi wa kisiasa wana nafasi kubwa ya kuhakikisha mafanikio ya usimamizi shirikishi wa misitu yanaingizwa katika Ilani na program za serikali ambazo zitachukua hatamu hivyo kwenye miaka mitano ya utekelezaji shughuli zinazohimizwa na mafanikio yaweze kuingizwa ili jamii ziweze kunufaika na misitu yao.

Naye Afisa Uraghabishi na Mawasiliano wa TFCG Revocatus Njau amesema kwa miaka miwili 2020 – 2021 TFCG inatekeleza mradi wa Haki Misitu kwa Kanda za Kusini, Kasikazini na Nyanda za Juu Kusini na shughuli ya mradi huo ni kuhamasisha kuhusu uhifadhi wa mistu ya vijiji, na kwamba tangu kuanzishwa kwa sera na sheria ya misitu namba 14 ya mwana 2002 imeweza kuleta mafanikio kwa vijiji zilivyorasimishwa na wanajamii wamekuwa wakiitunza misitu yao kutokana na kupatikana na faida wanayoipata na hiyo imeleta hamasa ya kuendelea kuhifadhi misitu.

“Lakini hii ambayo haijahifadhiwa tumeendelea kuhamasisha kwa sababu  misitu ambayo haijaifadhiwa imekuwa na migogoro kwa sababu haina mpango wa matumizi bora ya ardhi, hasa kwa migororo ya mipaka wafugaji na wakulima na masuala mbalimbali ambayo maeneo yameingiliwa kutokana na kutokuwa na mpangilio rasmi,”amesema Njau.

Meneja Mradi wa Kuongeza Usimamizi wa Misitu ya Jamii katika misitu ya Pwani amesema kwa kuangalia kiwango cha misitu ambayo haijahifadhiwa mradi utawezesha jamii kwenye halmashauri ya Mtama kwa vijiji 10 kuweza kuhifadhi na hekta kati ya 2,500 hadi 5,000 mpaka kumalizika kwa mradi hiyo ni katika kupunguza hekta ambazo hazijahifdhiwa.

“Katika uhifadhi huo tumeanza kusaidia jamii kufanya shughuli nyingine ili kuwajengea utayari jamii kushiriki uhifadhi wa misitu ikiwemo ya kuanzisha mpango wa matumizi bora ya ardhi ya vijiji na tumenza katika kijiji cha Nteni,”amesema.

Yahaya alisema jamii itasaidiwa kuweza kupima ardhi yao na itawezesha kila kijiji kwenye vijiji 10 kupata hati miliki za kimila na kila kijiji kitapata hati 150 sawa na hati 1500 kwa vijiji vyote kama sehemu ya jamii kujifunza kwamba uhifadhi wa ardhi unawasaidia vyema kupata faida moja kwa moja ikiwa ni pamoja na kupanda miti mbalimbali ya asili na matunda ipatayo 20,000.

No comments:

Post a Comment

Pages