WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, ameliomba Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), kupokea kwa moyo mkunjufu rasimu ya mabadiliko ya Katiba ya shirikisho hilo kwani imebeba mambo mengi mazuri.
Dk. Mwakyembe alitoa wito huo wakati akipokea rasimu hiyo kutoka kwa Katibu wa Kamati Maalumu ya mabadiliko ya Katiba ya shirikisho hilo, Henry Tandau, juzi jijini Dar es Salaam.
Waziri Mwakyembe, alisema chanzo cha kuunda Kamati hiyo ya mabadiliko ya Katiba ya RT, ni kutokana na malalamiko ya wadau wa mchezo huo kuhusiana na Katiba ya awali, mara baada ya kukutana nao wakati wa mbio za Kili Marathon mwaka huu.
Alisema kwa jinsi mambo yaliyopendekezwa na kamati hiyo yalivyo, yataleta mabadiliko chanya katika mchezo wa riadha na kuipongeza kwa kufanya kazi kwa kujitolea bila posho.
Aliwataka RT kuipokea rasimu hiyo na kuifanyia kazi, kasha kwa kushirikiana na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), waandae mkutano mkuu wa kupitisha mabadiliko hayo, kisha isajiliwe na Msajili wa Vyama na Klabu za Michezo.
Awali kabla ya kukabidhi rasimu hiyo, Tandau alieleza sehemu kubwa walizozigusa ni pamoja na muundo wa Kamati Tendaji ya RT, ambako hivi sasa itakuwa na Rais, Makamu wa Rais mmoja badala ya wawili, Katibu na Mweka Hazina wa kuajiriwa na Wajumbe sita wa Kamati Tendaji watakaotokana na kanda.
Mabadiliko mengine, Tandau alisema ni kuundwa Kamati ya Nidhamu, Kamati ya Rufaa ya Nidhamu, Kamati ya Uchaguzi na Bodi ya Wadhamini.
Aidha mabadiliko mengine ni kiwango cha elimu kwa wagombea wa nafasi ya Rais na Makamu ambapo kitakuwa ni angalau kuanzia Diploma, huku ukomo wa kugombea ni miaka 70 badala ya mihula.
Kwa upande wake, Makamu wa Pili wa Rais-Ufundi RT, Dk. Hamad Ndee, alipongeza rasimu hiyo na kumuahidi Waziri Mwakyembe wataifanyia kazi.
Wajumbe wa Kamati hiyo maalumu ni Filbert Bayi (Mwenyekiti), Henry Tandau (Katibu), huku wajumbe ni Kanali mstaafu Juma Ikangaa, Meta Petro, Mwinga Mwanjala, Mahona Milinde, Abel Odena na Tullo Chambo.
No comments:
Post a Comment