HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 18, 2020

SERIKALI YAWATAKA WASIMAMIZI WA SEKTA YA FEDHA KWENDA SAMBAMBA NA MPANGO MKUU


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Mary Maganga (katikati), akizindua Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa mwaka 2020 hadi 2030, kushoto ni Kamishna wa Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa Wizara hiyo, Dkt. Charles Mwamwaja na kulia ni Mkurugenzi Idara ya Sera za Kodi, Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar, Bw. Khamis Shibu Mwalim, katika ukumbi wa Wizara hiyo jijini Dodoma.

 

Na Farida Ramadhani na Ivona Tumsime, WFM, Dodoma

Serikali imewaagiza Wasimamizi na Waratibu wa Sekta ya Fedha kuwianisha mipango mbalimbali kuendana na Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha katika maeneo wanayosimamia ili kukabiliana na changamoto zilizopo na zinazoweza kujitokeza kwa lengo la kuhakikisha sekta hiyo inakuza kipato cha mwananchi na maendeleo ya Taifa.

Agizo hilo limetolewa jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Mary Maganga, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Doto James, katika uzinduzi wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha (Fianancial Sector Development Master plan) kwa mwaka 2020 hadi 2030.


Bi. Maganga alisema kuwa lengo la kuandaa Mpango huo ni kuongeza wigo na fursa za upatikanaji wa huduma za fedha kwa wananchi wote zikiwemo huduma za bima, mikopo, akiba, uwekezaji na kuongeza mchango wa sekta ya fedha katika ukuaji wa uchumi unaoendeshwa na sekta ya viwanda.


“Ili kuhakikisha malengo yanafikiwa, ni vema wadau wote wa Sekta ya Fedha ndani ya Serikali na nje ya Serikali kutambua kuwa uzinduzi wa Mpango huu ni mwanzo wa mambo yanayotakiwa kufanyika katika Sekta ya Fedha katika kuleta mageuzi makubwa na maendeleo katika kipindi cha miaka kumi ijayo”, alieleza Bi. Maganga.

Alisema kuwa miongoni mwa maeneo ambayo Wasimamizi na Waratibu wa Sekta ya Fedha kutakiwa kuwianisha mipango yao ili kuendana na Mpango huo uliozinduliwa ni pamoja na sekta zote ndogo zilizomo ndani ya Sekta ya Fedha kama benki, bima, masoko ya mitaji na dhamana, mifuko ya hifadhi ya jamii na Sekta ya Huduma Ndogo za Fedha.

 

Aidha Bi. Maganga, aliitaka Sekta ya Fedha kuongeza ubunifu ili kusaidia kukabiliana na changamoto zilizopo na zitakazojitokeza katika sekta hiyo muhimu ambayo inamchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi.

Aliainisha changamoto hizo kuwa ni pamoja na ukosefu wa fedha kwa ajili ya uwekezaji katika miradi mikubwa ya maendeleo, ukosefu wa mikopo kwa wajasiriamali wadogo na wa kati, ukosefu wa elimu ya fedha kwa wananchi na wananchi wengi kutofikiwa na huduma za fedha ambapo ni asilimia 8.6 tu ya wananchi waishio vijijini wanapata huduma za benki ikilinganishwa na asilimia 32.1 kwa wale wanaoishi mijini.

 

Alisema Serikali imeandaa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha 2020/2021 – 2029/2030, ili utumike kama nyenzo ya kutatua changamoto zilizopo kwa kuongeza upatikanaji wa huduma jumuishi za fedha, upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu, kulinda watumiaji wa huduma za fedha na kuimarisha uthabiti wa sekta ya fedha.

 

Bi. Maganga alisema Mpango huo pia umeandaliwa ili kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika sekta ya fedha, kudhibiti utakatishaji wa fedha haramu na kuweka mazingira wezeshi ya Sheria, kanuni, taratibu pamoja na miongozo katika sekta hiyo. 

 

Alisema ni matumaini yake kuwa kupitia Mpango huo Vyuo Vikuu, Taasisi mbalimbali za Elimu ya Juu pamoja na Utafiti vitaona fursa zilizomo na kujipanga kuboresha maeneo mbalimbali ya kitaaluma na kiutafiti ili kuhakikisha Sekta ya Fedha inaendelea kuwa juu, ya kisasa, yenye ushindani na kuweza kuhimili mabadiliko ya nyakati kwa wepesi na weledi mkubwa.

Naye Kamishna wa Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Charles Mwamwaja, alisema maendeleo ya Sekta ya Fedha ni muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini na kwa kuzingatia umuhimu huo, Serikali imefanya mageuzi kadhaa tangu miaka ya 1990 ili kuendeleza mfumo wa fedha wa uhakika unaozingatia soko kwa ajili ya kusaidia ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.

Alisema maboresho hayo yanajumuisha Awamu ya Kwanza na ya Pili ya Maboresho ya Sekta ya Fedha ambayo yalilenga kuwezesha ushiriki wa sekta binafsi katika sekta ya fedha na kuongeza upatikanaji wa huduma za fedha.

Kwa upande wa wadau walioshiriki katika uzinduzi huo wameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuandaa Mpango huo ambao wanaamini utachakia kwa kiasi kikubwa katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na wa nchi kwa ujumla.

Meneja wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA) Kanda ya Kati, Bi. Sara Lutaguza ni miongoni mwa wadau hao ambae ameahidi kuwa ofisi yake itahakikisha mikakati na mipango yote watakayoiandaa inaendana na Mpango huo.

No comments:

Post a Comment

Pages