September 18, 2020

Tanzania yaruhusu ndege za Kenya kutua

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI ya Tanzania kupitia kwa Mamlaka yake ya Usafiri wa Anga Tanzania(TCAA), imeruhusu ndege zote zinazotoka Kenya ikiwamo za Shirika kuu la Kenya Airways (KQ) kuanza kutua nchini humo baada ya kuondolewa vikwazo vilivyokuwa vimewekwa.

Taarifa fupi iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari imeeleza kuwa imeondoa marufuku ya ndege hizo kutotua hapa nchini baada ya Kenya kujuimuisha Tanzania katika orodha mpya ya nchi ambazo raia wake wanaruhusiwa kuingia Kenya bila kukaa karantini kwa siku 14.

Johari amesema mbali na kuruhusu ndege za KQ, zuio hilo limeondolewa pia kwa Fly 540 Limited, Safarilink Aviation  na AirKenya Express Limited.

"Kuondolewa kwa zuio hilo kunaanza mara moja na tayari Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini Kenya imejulishwa," ilieleza taarifa hiyo.

Mgogoro wa safari za ndege kati ya Kenya na Tanzania ulianza Agosti Mosi mwaka huu Kenya ilipotoa orodha ya kwanza ya nchi zilizoruhusiwa kuingia Kenya bila karantini na kuiacha Tanzania nje ya orodha hiyo.

Baada ya taarifa hiyo Tanzania nayo ilijibu kwa kuondoa ruhusa kwa shirika la KQ kutoa katika viwanja vya ndege vya Tanzania ambapo maarufu hiyo ilidumu kwa miezi miwili.

No comments:

Post a Comment

Pages