September 08, 2020

TMA yatabiri ukame

Na Irene Mark

HALI ya ukame inatarajiwa kuwepo kwenye maeneo mengi ya nchi hasa mikoa inayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.

Akizungumzia na waandishi wa habari Dar es Salaam leo Septmba 7, 2020; Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya  Hali ya Tanzania (TMA), Dk. Agnes Kijazi, alisema msimu wa mvua za vuli mwaka huu zinatarajiwa kuwa za chini ya wastani na wastani kwenye maeneo mengi ya nchi.

Mvua za vuli hutarajiwa kunyesha kuanzia Oktoba, Novemba na Desemba (OND) kwenye mikoa ya kaskazini mwa nchi ambayo hupata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.
 
Akitoa utabiri wa msimu wa vuli unaotarajiwa kuanza wiki ya pili ya Septemba mwaka huu hadi mwanzoni mwa Januari,2021 Dk. Kijazi alisema mifumo ya hali ya hewa inaonesha mwelekeo wa upepo na unyevunyevu kuwepo zaidi kwenye Bahari ya Pasifiki huku Bahari ya Hindi ikionekana kukosa upepo na unyevu.

“Mvua hizi za vuli zinatarajiwa kuwa chini ya wastani hadi wastani zikiambatana na vipindi virefu vya ukavu katika maeneo mengi ya nchi.

“Tunatarajia pia zitaanza kwa kuchelewa kati ya wiki ya pili na ya tatu ya Novemba, mwaka huu kwenye mikoa ya nyanda za juu kaskazini mashariki, ukanda wa pwani ya kaskazini na kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro,” alisema Dk. Kijazi.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, athari zitakazojitokeza ni upungufu wa unyevu katika udongo, maradhi ya mlipuko, malisho ya mifugo na upungufu wa maji safi na salma.

Alizishauri mamlaka zinazohusika kuchukua tahadhari ya kudhibiti majanga yanayoweza kutokea yakiwemo matukio ya moto kwenye mapori na misitu.

Aliitaja mikoa ya Kanda ya Ziwa itakayopata mvua chini ya wastani na wastani kuwa ni Kagera, Geita, Mara, Mwanza, Simiyu, Shinyanga na Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma ambako mvua zitaanza wiki ya pili ya Septemba mkoani Kagera na kusambaa.

Kwa ukanda wa pwani ya kaskazini mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Unguja, Pemba na kaskazini mwa Morogoro mvua  hizo chini ya wastani na wastani zitaanza kwa kuchelewa kati ya wiki ya pili na ya tatu ya Novemba mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

Pages