Na Mwandishi Wetu, Tanga
MKURUGENZI Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Ladislaus Mwamanga, amesema safari ya kuondoa umaskini katika nchi hii ni ndefu inayohitaji ushirikiano kati ya watendaji wa sekta zote kwa ngazi ya halmashauri na wanahabari watakaopeleka taarifa sahihi kwa jamii.
Mwamanga alisema hayo jijini Tanga jana jioni wakati akihitimisha kikaokazi cha siku mbili kilichowakutanisha wanahabari kutoka mikoa mitano ya Tanzania na watendaji wa TASAF.
Wanahabari hao zaidi ya 40 walitoka mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Tanga, Unguja na Pemba ambapo pamoja na kupata elimu sahihi kuhusu TASAF, walipata fursa ya kuwatembelea baadhi ya walengwa wa mpango wa kunusuru kaya maskini zaidi zinazohudumiwa na mfuko huo.
Wakizungumza baada ya kuwatembelea walengwa, wanahabari hao walieleza namna walengwa wanavyopambana kujikwamua na umaskini huku wakihitaji ushauri na huduma za kitaalam jambo linalozorotesha ustawi wao kiuchumi.
Mwenyekiti wa Klabu ya Wanahabari Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC), Irene Mark alisema ipo haja sasa kwa maofisa ugani, afya na biashara kuwatembelea walengwa hao ili kuwaidia kwenye shughuli ndogondogo wanazoanzisha kutokana na ruzuku wanayopewa na TASAF.
“Tumewatembelea walengwa mengi tumeyaona huko na kujifunza kwa vitendo kikubwa kinachohuzunisha ni namna walengwa wale wanavyoshindwa kuendelea kwa haraka.
“...Wanastori nzuri za namna wanavyoanzisha miradi midogo kwa ruzuku ya TASAF lakini miradi ile inakufa. Kuna bibi wa zaidi ya miaka 70 alipopata ruzuku ya kwanza alinunua kuku wanne wa kienyeji akawafuga wakafika 50 hii ni stori nzuri lakini kuku wale walikufa kwa kideri wakabaki 10.
“Na hao pia wapo hatarini sasa hapo unaona jinsi safari ya mafanikio inavyokwama na huyu ni mmoja kati ya wengi ndio maana naiomba TASAF ishirikishe wataalam wa sekta mbalimbali kuwahudumia walengwa hawa,” alisema Mark.
Akizungumzia hilo, Mwamanga alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na kuwataka watendaji wa sekta za afya, ugani na biashara kuibeba ajenda ya TASAF kuwa sehemu ya majukumu yao ili nguvu kubwa inayofanywa na watendaji wa mfuko huo isipotee.
“Tunasema haya kila siku, lazima tushirikiane hii TASAF ni yetu sote sisi tunatoa ruzuku na namna ya kuitumia ili iwe chanzo cha mapato kwenye kaya husika sasa pale mlengwa atakapochagua biashara ya kufanya lazima apate utaalam wa kile anachofanya.
“Sasa mtu anapoteza kuku zaidi ya wengi namna hiyo kama angesema awauze unafikiri angepata kiasi gani? Hii si sawa lazima kuwasaidia kitaalam ili nao waondokane na aibu ya umaskini lakini pia tutimize lengo la serikali la kutokomeza umaskini,” alisisitiza Mwamanga.
Awali akifungua kikaokazi hicho, Katibu Tawala Mkoa wa Tanga Judika Omar, aliwapongeza TASAF kwa kutambua umuhimu wa wanahabari katika kufikisha ujumbe sahihi kwa jamii.
Kikaokazi hicho ni maandalizi ya kuanza rasmi kwa utekelezaji wa shughuli za kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya TASAF ambapo kaya maskini zaidi kutoka vijiji vyote hapa nchini zitaingizwa kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini.
No comments:
Post a Comment