October 12, 2020

WATENDAJI ARDHI WATAKIWA KUSHIRIKIANA

Maofisa kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Makao Makuu Dodoma wakipeana maagizo namna ya kutekeleza zoezi la
elimu ya mlipa kodi nje ya Ofisi ya Halmashauri ya Manyoni, kabla ya kuanza utekelezaji wa zoezi hilo nyumba kwa nyumba katika mtaa wa Majengo. 

 

Na Mwandishi Wetu, Manyoni


WATENDAJI  wa sekta ya Ardhi Halmashauri ya Manyoni mkoani Singida, wametakiwa kufanya kazi kwa ushirikiano na umoja ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu yao kwa urahisi zaidi.


Kauli hiyo ilitolewa juzi na Kaimu kamishna wa Ardhi msaidizi mkoa wa Singida Speratus Ruteganya, katika kampeni maalum iliyozinduliwa na Wizara ya siku ya elimu ya mlipa kodi ambayo hutekelezwa kila siku ya Ijumaa.


Akizungumza na kikosi kazi maalum kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kilichofika Wilayani Manyoni kwa lengo la kutoa elimu kwa umma kuhusu kodi ya pango la Ardhi, Ruteganya alisema umoja na ushirikiano ndiyo nguzo pekee ya kufikia malengo katika sekta ya Ardhi.


Aliongeza kwamba, wananchi wanachohitaji ni elimu tu kwani wakielimika kodi itapatikana pamoja na taarifa muhimu za umiliki.
 

Kwa upande wake kiongozi wa kikosi kazi kutoka Wizara ya Ardhi, Adam Komba alisema, lengo la Wizara hiyo ni kuanzisha siku ya elimu kwa mlipa kodi ni kuhakikisha wananchi wanapewa elimu kuhusu umuhimu wa kulipa kodi pamoja na kuboresha taarifa zao za umiliki.


Komba  alisisitiza kuwa kutokana na mabadiliko ya teknolojia hasa kwenye utoaji wa huduma, Wizara ina mpango wa kuboresha mifumo yake ya utoaji huduma  pamoja na kutoa elimu kuhusu kodi ya pango la Ardhi.


"Zoezi  pia zoezi linalenga upatikanaji wa taarifa muhimu za kila mmiliki wa kipande cha Ardhi, alisema Komba. Naye afisa Ardhi mteule wa Wilaya ya Manyoni  Zamzam Seif, aliishukuru Wizara ya Ardhi kwa hatua mathubuti iliyochukua ya kuboresha taarifa
za wamiliki Ardhi na kampeni ya siku ya elimu ya mlipa kodi.
Zam zam alisema, kitendo cha Wizara kutuma kikosi kazi Wilayani hapo na kimewapa moyo  na nguvu mpya ya kufanya kazi.


Siku ya elimu ya Mlipa kodi ni kampeni maalum iliyoanzishwa na Wizara ya Ardhi ambapo, kila siku ya Ijumaa kikosi kazi kitakuwa kinapita mitaani kutoa elimu nyumba kwa nyumba ili kuhakikisha wamiliki wa Ardhi wanajua sheria, kanuni, taratibu na miongozo inayoisimamia sekta ya Ardhi.


Pamoja na hayo, pia lengo ni kuhakikisha Wizara inajenga ukaribu zaidi na wamiliki wa Ardhi na kuona namna bora ya kutatua changamoto mbalimbali za sekta ya Ardhi kwa ujumla.


Mwisho
Captions
NO 1.
NO 2.Baadhi ya mofisa kutoka makao makuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi wakigawana ramani za upimaji (survey plan) za mtaa
wa Majengo katika Halmashauri ya Manyoni kabla ya kuanza kupita nyumba
hadi nyumba kutoa elimu kuhusu kodi ya pango la Ardhi.

No comments:

Post a Comment

Pages