Na Magreth Kinabo na Mary Gwera, Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Mahakimu nchini kutochelewesha mashauri bila sababu za msingi ikiwemo kutumia kigezo cha kuchelewa kukamilika kwa upelelezi kama sababu mojawapo bali watumie mamlaka yao ya Kikatiba kuhakikisha kuwa mashauri yanasikilizwa na kuamuliwa kwa wakati.
Mhe. Jaji Mkuu ameyasema hayo mapema leo Novemba 27, 2020 katika hafla fupi ya kuapishwa kwa Mahakimu Wakazi wapya 39 iliyofanyika kwenye ukumbi namba moja wa Mahakama Kuu-Dar es Salaam, ambapo amesema kumekuwa na malalamiko ya ucheleweshaji bila sababu za msingi.
“Mahakama bado haizungumziwi na kutazamwa vizuri kuhusu ucheleweshaji wa maamuzi. Eneo hili wananchi wanalalamika sana, na wanayo sababu za kulalamika hasa Mahakama za Wilaya na Mahakama za Hakimu Mkazi—ni ucheleweshwaji mkubwa wa kesi kubwa kubwa za mauaji, madawa ya kulevya, nyara za serikali, uhujumu uchumi, ugaidi, utakatishaji wa fedha,” alisema Mhe. Jaji Mkuu.
Mhe. Jaji Prof. Juma aliongeza kwa kusema kuwa Mahakimu wanafanya kosa kubwa la kukubali Maahirisho yasio na kikomo na bila kupokea sababu zozote za msingi, huku akisisitiza kuwa sababu ya upelelezi unaendelea si ya msingi.
Aidha, Mhe. Jaji Mkuu alieleza kuwa wananchi wanalalamika ya kuwa, waendesha mashtaka wanatumia ucheleweshaji Mahakamani kama adhabu kabla hata kosa halijathibitishwa Mahakamani.
Aliongeza kwamba ili kuziba mwanya uliokuwa unatumiwa na Waendesha Mashtaka na Wapelelezi wa kuomba maahirisho yasio na kikomo, Mhe. Jaji Kiongozi alitoa waraka namba 5 wa mwaka 2019, kuhusu kuharakisha “Committal Proceedings, Plea Taking na Preliminary Hearing” na kuwataka Majaji na Mahakimu kuusoma waraka huo kama mwongozo wa uendeshaji wa mashauri.
Mahakama nyingi zinakiuka sheria kwa kutotekeleza masharti ya Usimamizi wa Mirathi kwakushindwa kuhakikisha kuwa majalada ya mirathi yanafungwa kwa wasimamizi kuwasilisha mahesabu.
Aidha aliwataka mahakimu hao kufuata utaratibu mwepesi wa kisheria ili Wasimamizi wa Mirathi wasitumie vibaya mali na kupora mali za marehemu.
Alisema kwa mujibu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Ibara ya 107B, imewahakikishieni nyie Mahakimu (Pamoja pia na Wasajili, Majaji) kuwa, katika kutimiza ahadi ya viapo/vithibitisho vyenu-
“Mtatekeleza mamlaka ya utoaji haki, kupitia Mahakama zitakazokuwa huru na mtalazimika kuzingatia tu, masharti ya Katiba na yale ya Sheria za Nchi,” alisema. Huku akisisitiza kuwa maana yake ni kwamba, waongozwe na Katiba, Sheria na taratibu za kimahakama katika kazi za Uhakimu. Uhakimu wako utaimarika endapo siku zote utazingatia Sheria, na kuongozwa na taratibu, kanuni na nyaraka zinazotolewa mara kwa mara na viongozi wa Mahakama.
Pia aliwataka kunzingatia maadili ya kazi zao na kujiepusha na vitendo vya rushwa.
No comments:
Post a Comment