HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 26, 2020

Shahidi aeleza jinsi alivyokuta dawa za kulevya nyumbani kwa Kiboko

NA JANETH JOVIN

SHAHIDI wa tatu katika kesi ya dawa za kulevya inayomkabili mfanyabiashara Ayoub Kiboko, Inspekta Msaidizi wa Polisi (SSP), Emmanuel Ambilikile ameieleza mahakama jinsi walivyokamata bastola moja aina ya brown, risasi saba, vikopo vinavyodhaniwa kuwa na dawa za kulevya katika nyumba ya mtuhumiwa huyo.

SSP Ambilikile pia ameeleza jinsi walivyokuta hati za kusafiria, mafaili ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kitabu cha silaha, redio ya upepo pamoja na kadi za magari mbalimbali nyumbani kwa mfanyabiashara huyo.

Shahidi huyo ameyaeleza hayo jana katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Rushwa na Makosa ya Uhujumu Uchumi maarufu ‘Mahakama ya Mafisadi’ wakati akitoa ushahidi katika kesi inayaomkabili Kiboko na mkewe Pilly Kiboko.

Akitoa ushahidi huo, SSP Ambilikile amedai kuwa yeye ndiye alihusika katika upekuzi na ukamati wa vitu mbalimbali katika nyumba ya watuhumiwa hao na kuongeza kuwa upekuzi huo ulishuhudiwa pia na majirani wawili ambayo ni Christina Macha na Raymond Kinambo.

Akiendelea kutoa ushahidi mbele ya Jaji Lilian Mashaka, alidai kuwa upekuzi katika nyjmba hiyo aliufanya Mei 23, mwaka jana na kwamba vielelezo vyote vilivyopatikana aliviwekea alama na kwa vile vinavyodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya aliweka alama A,17, A1 na A2,21 B na 20C.

“Baada ya kufanya hivyo tulielekea ofisini kwa hatua zingine, tulipofika muda wa saa 2 usiku tuliwasiliana na mtunza vielelezo SSP Neema na alipofika tulimkabidhi, vielelezo ambavyo havihusiani na dawa za kulevya vilibaki chini yangu ikiwamo magari ambayo yalipokelewa pia kama vielelezo,” amedai shahidi huyo.

Aidha vitu vingine ambavyo shahidi huyo alidai vilikamatwa nyumbani kwa mtuhumiwa huyo ni kiboksi cha kutunza bastola, kadi nne za benki ikiwamo ya Tembo ya umoja ya kuweka na kutolea fedha, faili dogo lenye nyaraka,simu aina ya Nokia, hati nne za kusafiria na unga unaodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya ukiwa ndani ya kikopo cha plastiki.

SSP Ambilikile amedai kuwa katika upekuzi huo pia walikuta vikopo viwili vyenye unga unaodhaniwa ni dawa za kulevya, chenga chenga za unga ndani ya mfuko mweupe wa nailoni, kadi ya gari aina ya Landcruser, Prado, Toyota Hilux pamoja na Prado.

Baada ya shahidi huyo kumaliza kutoa ushahidi wake alihojiwa na wakili wa utetezi Majura Magafu ambapo alimtaka aeleze ndani ya nyumba alikuta watu wangapi.

SSP Ambilikile alijibu swali hilo alidai kuwa aliwakuta watu wawili ambao ndio washtakiwa mahakamani hapo.

Shahidi hiyo aliulizwa upekuzi ulianza muda gani ambapo alijibu kuwa ulanza saa 8 usiku na kumalizika saa moja asubuhi ambapo baada ya zoezi hilo waliwachukua watuhumiwa na kuwapeleka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) kwa mahojiano.

Aidha amedai kuwa kielelezo namba 17 alikikuta kwenye choo cha chumbani kwa washtakiwa hao huku kielelezo C alikikuta katikati ya viatu huku akidai kuwa hawezi kujua ni aina gani ya viatu vilikuwepo.

Kiboko na mkewe wanakabiliwa na shtaka moja la kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroine zenye uzito wa gramu 251.25, ambapo wanadaiwa walifanya tukio hilo Mei 23, 2018 eneo la Tegeta Nyuki, Masaiti Wilaya ya Kinondoni.

No comments:

Post a Comment

Pages