November 21, 2020

WAZIRI MKUU AAGIZA WAKUU WA MIKOA WAFANYE UKAGUZI KWENYE VIWANDA, MAGHALA YA SARUJI

*Asema wakague mawakala, wauzaji wa kati na wadogo

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza Wakuu wa Mikoa yote nchini wafanye ukaguzi kwenye viwanda vya kuzalisha saruji, mawakala, wauzaji wa kati na wadogo wa bidhaa hiyo na wachukue hatua stahiki.

 

Ametoa agizo hilo leo jioni (Jumamosi, Novemba 21, 2020) wakati akizungumza na Wakuu wa Mikoa yote nchini kuhusu tatizo la kupanda kwa bei ya saruji nchini kwenye kikao alichokiendesha kwa njia ya video (video conferencing) kutokea ofisini kwake Mlimwa, Dodoma.

 

“Wakuu wa Mikoa na Kamati zenu za Ulinzi na Usalama fanyeni ukaguzi kwa mawakala, ukikuta wamerundika saruji kamata na kuwashtaki. Nendeni pia kwa wauzaji wa kati, nao pia chekini maghala yao,” amesema.

 

“Piteni kwa maafisa biashara na muwasimamie iwe ni kwenye Sekretarieti za Mikoa au katika Halmashauri zenu, tunataka bei irudi kama ilivyokuwa mwezi Septemba kwa sababu hakuna badiliko lolote kwenye tozo ya kodi,” amesisitiza.

 

Waziri Mkuu ambaye ameitisha kikao cha kwanza na Wakuu hao wa Mikoa tangu aapishwe, amesema: “Wakati wa uapisho, Novemba 16, mwaka huu nilitambulisha tatizo la kupatikana saruji kwa bei ya juu sana. Niliagiza kila Mkuu wa Mkoa afuatilie ni kwa nini bei imepanda kiasi hicho.”

 

“Nimepokea taarifa zenu na kuona hali halisi iliyoko kwenye mikoa yenu. Hali si nzuri, akiba iliyopo ni ndogo na bei ni ya juu sana. Nasema bei ni ya juu sababu tunaangalia bei ya mlaji kwa sasa. Awali ilikuwa kati ya sh. 14,000 hadi 15,000 lakini sasa hivi imefikia sh. 24,000 kwa mfuko mmoja,” amesema.

 

Amesema hiyo ni tofauti ya sh. 9,000 hadi 10,000 lakini kwa sasa ni lazima bei ishuke kwa sababu hakuna tozo za kodi zilizoongezeka. “Kuna watu wanatumia kigezo cha gharama za usafirishaji, hii si kweli kwani hata Septemba, walikuwa wakisafirisha bidhaa hiyo kwa njia zetu zilezile.”

 

Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya tano imekuwa ikihimiza ujenzi wa viwanda ili bidhaa zinazozalishwa nchini zipatikane kwa wingi. “Kwenye saruji malighafi ziko nchini, hazitoki nje, kwa hiyo tunataraji upatikanaji wake ungekuwa rahisi na bei ingekuwa nafuu.”

 

Amewaagiza Wakurugenzi kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara pia wakutane na wenye viwanda na kuweka ratiba ya mwaka ili kuepuka viwanda vingi kufungwa kwa matengenezo ya mwaka kwa wakati mmoja na kufanya saruji iadimike na kupandisha ghafla bei ya saruji.

 

Vilevile, amewaagiza viongozi wa Tume ya Ushindani (FCC) wafuatilie wamiliki wenye viwanda vya saruji na wafanye uchunguzi kubaini uhalali wa bei zinazopangwa na mawakala na wafanyabiashara wa saruji nchini.  Pia akawataka wawasisitizie wazingatie sheria za nchi.

 

Kwa upande wao, Wakuu hao wa Mikoa, wamesema wamepokea maelekezo na watayatekeleza.

 

Mkutano huo uliwashirikisha pia Naibu Makatibu Wakuu wa Wizara za Viwanda na Biashara; Uchukuzi na watendaji kutoka Tume ya Ushindani.

No comments:

Post a Comment

Pages