Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanza zoezi la kupanga, kupima na kumilikisha ardhi katika vitongoji 14 vilivyopo katika kata ya Chamwino mkoani Dodoma.
Zoezi hilo limeanza rasmi tarehe 24 Novemba 2020 kwa timu kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi chini ya Mkurugenzi Msaidizi wa Upimaji na Ramani Bi. Elizabeth Mrema kukutana na wananchi wa vitongoji vyote 14 vya Kata ya Chamwino ili kuangalia namna bora ya kuendesha zoezi hilo.
Akizungumza wakati wa mkutano huo, Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Usanifu Miji na Mipango Kabambe Wizara ya Ardhi Bi. Immaculate Senje aliwataka wananchi wa vitongoji vya Chamwino kuhakikisha wanamaliza tofauti za migogoro midogomidogo ya ardhi katika maeneo yao kabla ya wataalamu hawajafika uwandani ili kurahisisha kazi ya upangaji, upimaji na umilikishaji ardhi kwa wananchi.
Alisema, iwapo wananchi wa maeneo husika watashindwa kumaliza tofauti zao za migogoro ya ardhi mapema basi wataalamu watakapofika watashindwa kuendelea na zoezi mpaka pale utatuzi wa mgogoro uikapomalizika.
‘’Zoezi la upimaji katika eneo la Chamwino hapa Dodoma linalenga pia kupata maeneo ya miundombinu ikiwemo barabara na zoezi litazingatia njia za awali na kuepuka kugusa nyumba za wananchi’’ alisema Bi Senje.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Upimaji na Ramani Elizabeth Mrema aliwatoa hofu wananchi wa maeneo ya vitongoji vya Chamwino kuhusiana zoezi hilo ambapo aliwataka kuwapa ushirikiano wataalamu wa wizara ya ardhi watakaokuwa wakifanya kazi hiyo.
Alisema, hofu ya wananchi kuwa wanaweza kudhulumiwa maeneo yao kupitia zoezi hilo siyo za kweli na kusisitiza kuwa Wizara imeamua kuboresha vitongoji vya kata ya Chamwino ili kuwawezesha wananchi kuwa na nyaraka za umiliki wa maeneo yao.
Kwa mujibu wa Bi. Mrema, zoezi la kupanga, kupima na kumilikisha ardhi Chamwino litaanza na vitongoji vitano na baadaye kuendelea na vitongoji viingine hadi kufikia 14. Alivitaja vitongoji vitano ambavyo zoezi hilo litaanza kuwa ni Sokoine, Ukombozi, Kambarage, Umoja na Azimio.
Afisa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma Letare Shoo aliwaambia wananchi wa Chamwino katika mkutano huo kuwa, kazi ya upangaji, upimaji na umilikishaji maeneo katika vitongoji vya Chamwino umegawanyika katika makundi makuuu mawili aliyoyaeleza kuwa ni urasimishaji au uboreshaji maeneo yaliyojengwa bila kufuata taratibu na pili ni kupima mashamba makubwa kwa kuanisha matumizi yake ikiwemo viwanja.
Hata hivyo, Afisa Ardhi huyo wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino alisema, tofauti na maeneo menfine wananchi wa Chamwino watapata unafuu katika gharama wakati wa zoezi hilo ambapo badala ya kulipia 150,000 wao watalipia shilingi 50,000 kwa kila kiwanja.
‘’Halmashauri ya Manispaa ya Chamwino ina jumla ya vijiji 107 lakini kijiji cha Chamwino kimepata upendeleo wa kipekee kupimiwa na wataalamu wa Wizara ya Ardhi’’ alisema Shoo.
Mmoja wa wananchi wa kitongoji cha Talama katika kata ya Chamwino Dikson Mchiwa mbali na kuipongeza Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa uamuzi wa kupanga, kupima na kumilikisha maeneo Chamwino alitaka wizara kuhakikisha zoezi hilo linatakelezwa hasa ikizingatiwa kumekuwa na kugeugeua chakuelezwa upimaji utafanyika halafu haufanyiki..
No comments:
Post a Comment