Mratibu wa Kitaifa wa Program ya Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu (FORVAC), Emmanuel Msoffe akiwaeleza waandishi wa habari waliotembelea Bustani ya Kipiki wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma namna ya kuanda na kupanda mche wa msaji.
NA SULEIMAN MSUYA, NAMTUMBO
KATIKA
kuhakikisha uhifadhi wa misitu na utunzaji wa mazingira unakuwa
endelevu Program ya Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu (FORVAC)
inatarajia kugawa miti miche ya misaji 300,000 itakayogharimu shilingi
milioni 150.
Misaji hiyo itagawanywa kwa wananchi na vikundi vya upandaji miti katika Kijiji cha Liuli Wilaya Nyasa mkoani Ruvuma.
Programu
ya FORVAC inatekelezwa kupitia Idara ya Misitu na Nyuki chini ya Wizara
ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland.
Kupitia
programu hiyo yenye lengo la kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya
misitu inatekelezwa kwenye wilaya 12 ambazo ni Handeni, Kilindi,
Mpwapwa, Kiteto, Liwale, Nachingwea, Ruangwa, Tunduru, Namtumbo, Nyasa,
Mbinga na Songea zilizopo katika Kongani tatu za Tanga, Lindi na Ruvuma.
Akizungumza
na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali walikuwa kwenye ziara
ya kujifunza dhana nzima ya program hiyo, Mratibu wa FORVAC Kongani ya
Ruvuma, Marcel Mutunda amesema wameamua kuanzia katika upandaji miche
ili dhana nzima ya mnyororo wa thamani ieleweke.
Amesema
katika mwaka huu 2020/2021 watagawa miche ya Misaji 300,000 yenye
thamani ya shilingi milioni 150 kwa wanavijiji wenye mashamba ya miti
wilayani Nyasa.
Mutunda
amesema ugawaji wa miche hiyo inayozalishwa kwenye Bustani ya Kipiki
iliyopo Shamba Miti Mpepo ni mwendelezo wao wa kuhakikisha wananchi
wanashiriki kutunza mazingira.
"Utaratibu huu wa ununuzi wa miche umeanza mwaka jana ambapo tulinunua miche 150,000 yenye thamani ya shilingi milioni 75.
Mwaka
huu tutanunua miche 300,000 inayogharimu shilingi milioni 150 kwani
tunaamini mnyororo wa thamani unaanzia kwenye mbegu, miche na baadae
miti," amesema.
Amesema
iwapo miti hiyo 300,000 itafanikiwa kuota na baadae kuvunwa itapunguza
uharibifu wa misitu ambao unaonekana kuongezeka hasa maeneo ambayo
hayana Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ).
Mratibu
wa FORVAC Kitaifa, Emmanuel Msoffe, ambaye pia ni mtaalam wa miti
amesema miti ya Misaji ni fursa nzuri ya kibiashara inayopaswa kupewa
kipaumbele.
Amesema iwapo kila mkulima wa miti atajikita kwenye upandaji wa Misaji ukataji wa miti kama Mninga, Mkongo na mingine utapungua.
"Promosheni
tunayofanya ni kuhamasisha upandaji Misaji inatokana na ukweli kuwa
inafaa kutumika kwa ajili ya utengenezaji wa thamani, kuweka sakafu,
kutengeneza deki za meli na majahazi, kupaulia na wengine kutumia kama
kuni," amesema.
Msoffe
amesema ili miti hiyo kuvunwa inachukua muda wa miaka 25 hadi 30 kwa
Tanzania ila kwa nchi za baridi hadi kufikia miaka 60,"amesema.
Mtaribu
huyo amesema miti hiyo inakubali katika ardhi zenye kina kirefu na
rutuba na maji mengi kama Longuza Tanga, Mtibwa na Kilombero Morogoro,
Namtumbo na Nyasa Ruvuma.
Kwa
upande wake Ofisa Misitu Mkoa wa Ruvuma, Africanus Charles amesema
wamepokea kwa furaha FORVAC kwa kuwa imekuja kupambana na mabadiliko ya
tabia nchini na kukuza uchumi wa wanavijiji.
"FORVAC
wamekuja kutupa nguvu zaidi na sisi tutawaunga mkono kwa nguvu zote ili
uhifadhi uweze kuendelea kwani una faida kwa mkoa na nchi.
Tuna bustani za Misaji mbili ambazo ni hii ya Kipiki na Ndongosi ila pia kuna bustani ya miche ya Pine na Mikaratusi," amesema.
Ofisa
Misitu huyo amesema mkoa umetenga hekta 80,000 ambapo hadi sasa
wamepanda asilimia 53 ya lengo na miti ambayo wanapanda ni ya
kibiashara.
Mhifadhi Mkuu
wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Shamba la Mpepo wilayani
Namtumbo mkoani Ruvuma, Misana Manumbu amesema bustani ya Misaji katika
shamba hilo imekuwa na mafanikio.
Amesema
bustani hiyo yenye heka tano wamepanda miti ya Misaji milioni 1 ambapo
wanagawa kwa wanavijiji na kuuza kwa taasisi mbalimbali zenye uhitaji.
"Tumegawa miche zaidi ya 200,000 kwa wananchi 100, kule Mpepo tumegawa miche ya Pine 150,000," amesema.
Mhifadhi
huyo amesema zoezi hilo la uzalishaji miche linakabiliwa na changamoto
ya moto na barabara hivyo kuomba mamlaka kuchukua hatua.
Manumbu amesema uzalishaji wao unakidhi hitaji ya watu wanaotaka miche hivyo iwapo kuna watu wanahitaji wawasiliane nao.
Amesema
miti ya Misaji ina thamani kubwa katika soko hivyo kuwataka wanavijiji
na wananchi kupanda miti mingi kwa ajili ya vizazi vyao vya baadae.
Manumbu
amesema miche hiyo inaweza kupandwa 1,200 katika hekta moja na kwa
hekari miche 450 na kwamba wanatoa elimu ya upandaji kwa wanavijiji.
Amesema FORVAC wamekuwa wakipigania uhifadhi hivyo wanapaswa kuungwa mkono na wadau wengine.
No comments:
Post a Comment