December 11, 2020

JUHANI HARKONEN: TUTUNZE MISITU KAMA FAMILIA, MALI ZETU

Kiongozi wa Program ya Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu (FORVAC), Juhani Harkonen akiangalia gogo lilikatwa kwa ajili ya mbao katika Kijiji cha Sautimoja wilayani Tunduru mkoani Ruvuma.

Msitu ukiwa umependeza kutokana na utunzaji unaoafanywa na wananchi wanaouzunguka.
 

NA SULEIMAN MSUYA


WATANZANIA wameshauriwa kutunza rasilimali misitu kama wanavyotunza familia zao kwa kuwa ina faida nyingi kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Ushauri huo umetolewa na Kiongozi  wa Program ya Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu (FORVAC), Juhani Harkonen katika mahojiano maalum na mwandishi wa habari hii jijini Dar es Salaam.

FORVAC ni program inayotekelezwa kupitia Idara ya Misitu na Nyuki chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland kuhakikisha misitu inachangia huduma za kijamii, uchumi na utunzaji mazingira.

Program hiyo inatekelezwa katika wilaya 12 ambazo ni Tunduru, Namtumbo, Nyasa, Mbinga na Songea zilizopo Kongani ya Ruvuma.

Kongani ya Lindi ina wilaya za Nachingwea, Ruangwa, Liwale na Kongani ya Tanga ina wilaya za Handeni, Kilindi, Mpwapwa na Kiteto.

Harkonen amesema ili misitu iweze kuwa endelevu ni vema kila mwananchi akachukulia kwa mtazamo chanya kwa kupanda na kuilinda ili iweze kuchangia ukuaji wa uchumi na maendeleo yao.

Amesema nchini Finland misitu ina thamani sawa na nyumba, familia na vitu vingine muhimu hali ambayo inachochea uhifadhi shirikishi na kuitunza.

"Nitumie nafasi hii kuwaomba Watanzania kuchukulia misitu kwa uzito mkubwa kama wanavyofanya kwa familia na mali zao kwani ni rasilimali muhimu sana kwa jamii kiuchumi, maendeleo na mazingira," amesema.

Kiongozi huyo wa FORVAC amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau ina wajibu wa kutoa elimu kuanzia elimu ya msingi ili kila mmoja aweze kushiriki kutunza misitu.

"Jambo lolote ili lifanikiwe linahitaji elimu na sisi katika hizi wilaya 12 ambazo tupo tumeanza na elimu kwanza hali ambayo inarahisisha utekelezaji," amesema.

Harkonen amesema katika vijiji ambavyo vinashiriki program wamehakikisha kuna mpango wa matumizi bora ya ardhi ili kuepusha migogoro.

Amesema FORVAC inaamini rasilimali misitu ikitumika kwenye mfumo wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (CBFM), itakuwa salama na endelevu na kuinua maisha yao.

"Misitu ikitumiwa kwenye mfumo wa CBFM ina uwezo wa kubadilisha maisha ya wanayoizunguka na nchi kwa ujumla na uhakika wa uendelelevu utakuwepo," amesema Harkenon.

Aidha, kiongozi huyo amesema pamoja na kuhamasisha CBFM ni muhimu sheria, sera na kanuni za misitu ziendane na wakati husika kwa maslahi ya nch.

Amesema kiujumla FORVAC imeona mafanikio ya miaka miwili ya program hiyo jambo ambalo linawapa nguvu kushawishi kuendelea.

Mtaalam Kijana wa Kimataifa Anayeshughulikia Ufuatiaji na Thamini wa Mradi, Nette Korkanen amesema mwitikio wa wanavijiji ambao wanatekeleza program hiyo ni mzuri jambo linaloleta matumaini.

"Sisi kwetu Finland tumekuwa tukiamini misitu ni muhimu na ina faida hivyo kila mmoja ni balozi naamini hali hii itasambaa Tanzania nzima siku chache zijazo," amesema.

 Mtaalam huyo amesema kitendo cha kumpa matumaini mwananchi kuwa atanufaika na misitu yake baada ya miaka zaidi 80 kinahitaji elimu hivyo anaamini dhana hiyo itasambaa nchini.

Korkonen amesema Tanzania ina misitu mingi ya asili ambayo ikitunzwa  kwa mfumo wa kunufaisha wananchi itakuwa endelevu na salama.


No comments:

Post a Comment

Pages