December 02, 2020

Machungu ya Covid-19 kwa wajasiriamali

 NA JANETH JOVIN, Novemba 2020

“Nilikata tamaa kabisa ya maisha wakati wa janga la Covid-19
lilipoingia nchini kwetu, maana sikuweza kufanya biashara kwa
kuwa mahali nilipokuwa nafanyia ni katika shule ambazo
zilifungwa na serikali.”


Hiyo ni kauli ya Hilda Raphael mfanyabiashara ya kuuza mihogo katika Shule ya Msingi Umoja iliyopo Mabibo jijini Dar es Salaam, ambaye katika Makala hii anaeleza jinsi ambavyo ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona ulivyoweza kuleta athari katika shughuli zake za kila siku.


Hilda anasema kipindi cha corona alijiuliza maswali mengi ikiwamo janga hilo litaisha lini na atawalishaje watoto wake wawili, na kusema kuwa alikosa majibu.


Akiwa anatikisha kichwa, Hilda anasema maswali hayo yalimfanya kushindwa kumudu kukaa nyumbani kwa kuwa jambo hilo aliliona kuwa litaathiri ustawi wa familia yake na atashindwa kurejesha kwa wakati fedha za mkopo ambazo alizipata katika moja ya taasisi ya fedha hapa nchini.


“Niliamua kujiongeza nikaanza kutembeza bagia mitaani maana
niliona nisipofanya hivyo nitazidi kuchanganyikiwa kwa kuwa
nadaiwa fedha za mikopo na nilijua huenda mali zangu ambazo
niliziweka dhamana kwenye hiyo taasisi zinaweza kuchukuliwa na kupigwa mnada,” anasema.

Hata hivyo, Hilda alikuja kupata matumaini kufuatia agizo la
Serikali la kuzitaka taasisi za fedha kuongeza muda wa urejeshaji wa mikopo, na kufunguliwa kwa shule na shughuli zote ambazo zilikuwa zimesitishwa kutokana na corona kurudi kama zamani.


Hilda anasema aliporejea kijiweni kwake pale shuleni, alikutana na masharti mbalimbali ambayo yaliwekwa na viongozi wa shule, ambapo walitakiwa kila mtu kuwa na ndoo ya wanafunzi kunawa mikono kabla ya kuchukua muhogo na kula.


Vilevile anasema uongozi huo uliwataka wafanyabiashara wote wa eneo hilo la shule kupima afya zao na kupeleka majibu sehemu husika shuleni hapo.
 

“Tulifanya hivyo kama tulivyotakiwa na asilimia ya wafanyabiashara wote majibu yetu yalikuwa mazuri tukaruhusiwa kurejea kazini, maisha yakaendelea kama kawaida hadi hivi leo ndugu mwandishi, hakika tunaendelea kumshukuru Mungu kwa kutuepusha na janga hili,” anasema.


Hata hivyo, hali hiyo haikumtokea Hilda peke yake bali hata kwa wafanyabiashara wengine akiwamo Zakia Shaha anayefanya kazi za mama lishe katia eneo la Tangibovu kwa Komba jijini Dar es Salaam.


Zakia anafunguka na kusema kuwa kipindi cha kwanza baada ya
ugonjwa wa Covid-19 kugundulika kuwa umeingia nchini biashara kwao ilikuwa mbaya.


Anasema chakula walichokuwa wakikipika kuanzia mchana na
wakati mwingine jioni kilikuwa hakiishi kutokana na watu
kupungua mitaani na barabarani.

Zakia anaeleza kuwa wateja wao wengi walikuwa majumbani
wanaogopa kutoka kwenda makazini, hali iliyowafanya hata wao
washindwe kufanya biashara, na kusababisha hata mitaji yao
kupungua.
 

“Utapika chakula kingi utamuuzia nani wakati hakuna wateja,
kiukweli kipindi cha mwanzo tulipitia wakati mgumu sana ambao sitaki hata kuukumbuka,” anasema.


Hata hivyo, anasema pamoja na Serikali kusimama kidete na
kuwaondoa hofu wananchi hali ya biashara kwao bado si nzuri
kama ilivyokuwa zamani.


Vilevile anasema njia za upatikanaji wa fedha kwa upande wake
zimekuwa ngumu kwa sababu kampuni za ujenzi zimepunguza
watu ambao ndio walikuwa wakiwategemea kununua chakula chao.
 

Hali hiyo ilimpelekea hadi changamoto katika familia yake ambapo mtoto wa Zakia, Halfani Hamis mwenye umri wa miaka 12 anasema kuna wakati walishindwa hata kunywa chai asubuhi na kujikuta kula milo miwili kwa siku.


Hamis ambaye anasoma darasa la saba katika moja ya shule ya
msingi iliyopo Kawe, anasema kwa mara ya kwanza Serikali
iliporuhusu kufunguliwa kwa shule, alishindwa kuendelea na
masomo kutokana na mama yake kukosa fedha ya kumpatia kwa ajili ya kununua uji na chakula cha mchana.


“Maisha yalikuwa magumu sana ila kwa sasa tunamshukuru Mungu kwani hali ilivyo sio kama kipindi kile, tunakwenda shule licha ya kwamba tunapatiwa kiasi kidogo cha fedha lakini kinatutosha,” anasema Hamis.

Beng’i Issa ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji
Wananchi Kiuchumi (NEEC), anasema kipindi cha corona
kilikuwa ni kigumu kwa kuwa watu wengi, wakiwemo wajasirimali ambao wanawawezesha kiuchumi, walikuwa wakiogopa kutoka nje.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng'i Issa.

 

Anasema katika kipindi hicho wajasiriamali waliokuwa wakifanya biashara zilizokuwa zinahitaji mikusanyiko ya watu ndio ambao walirudi nyuma kidogo kiuchumi.


“Hata hivyo kitu kizuri katika nchi yetu kipindi hiki cha corona
kilikuwa si cha muda mrefu bali tulikuwa nacho kwa muda mfupi, lakini pamoja na hayo wapo wafanyabiashara hasa wa masuala ya kidigitali walitumia fursa hiyo kufanya biashara mitandaoni,” anasema. 

Aidha anasema baraza hilo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kwa kipindi cha miaka mitatu limefanikiwa kufakia Watanzania milioni 15 na kuwawezesha kiuchumi katika shughuli mbalimbali.


Kwa upande wake Mratibu wa Miradi ya Shirika lisilo la kiserikali la Counselling and Family Life Organization (CAFLO), Emmanuel Ngazi, anasema wakati wa corona shughuli zao za utoaji wa mafunzo kwa vijana kuhusu ujasiriamali zilisimama.


Anasema baadhi ya vijana hasa wanawake waliopo katika majukwaa ya vijana wanayoyasimamia waliwalalamikia kukosa kazi za kufanya hivyo kushindwa kuzimudu familia zao.


“Biashara zao za ujasirimali walikuwa hawafanyi na unamkuta mtu ana watoto wadogo nyumbani hivyo anakosa kabisa fedha za kulisha familia yake,” anasema.

Hata hivyo, Ngazi anasema kwa sasa maisha yameanza kurudi
kama zamani kwani wameweza kuwafikia tena vijana na kuwapatia elimu ya ujasiriamali ambayo ni muhimu katika maisha yao.


“Tunaendelea na kazi ila sio kwa spidi ile tuliyokuwa nayo kabla ya corona, hata hivyo tunaamini mambo kwa sasa yanakwenda vizuri na Serikali yetu ipo makini sana kuhakikisha kila kitu kipo sawa,” anasema.
 

Takwimu zinasemaje ?
 

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kuwa hadi kufikia Novemba 4, 2020 jumla ya nchi 219 duniani zimeripoti kuwa na wagonjwa wa Covid 19, watu Milioni 47.3 wameugua huku Milioni 1.2 wamefariki dunia.


Huku upande wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalotoa Mitaji ya Maendeleo (UNCDF) limeonyesha jinsi gani corona ilivyowaathiri wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo, huku asilimia 1.6 ndio wanaonekana kutokuathirika na changamoto hizo.

Kwa upande wa Tanzania


Kwa mujibu wa taarifa ya mwenendo wa ugonjwa wa Covid-19
iliyotolewa Aprili 29, mwaka huu na Waziri Mkuu wa Tanzania
Kassim Majaliwa, wagonjwa 167 wamepona virusi vya corona.
Hata hivyo Majaliwa alisema kuanzia tarehe 23 hadi 28 Aprili, 2020 walipatikana watu wengine wapya 196 wenye maambukizi ya corona ambapo Tanzania bara wakiwa 174 na Zanzibar 22.
Alisema wagonjwa hao walitangazwa na Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, hivyo kufanya jumla ya wenye maambukizi nchini kuwa 480.
 

Hata hivyo alisema Aprili 24, mwaka huu Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto aliwatangaza jumla ya

watu waliopona ni 37 na hivyo kufanya jumla ya waliopona kuwa 48.  Aidha alisema Aprili 29 mwaka huu idadi ya waliopona waliongezeka kutoka 48 na kufikia 167, Zanzibar wakiwa 36 na Tanzania Bara 83.


“Tunasikitika kueleza kuwa tuna ongezeko la vifo sita na kufanya jumla ya vifo sasa kuwa 16. Hata hivyo kati ya wenye maambukizi 297 waliobaki, watu 283 wanaendelea vizuri sana na watu 14 wako chini ya uangalizi maalum na tunaendelea kuwaondoa walio karibu na wagonjwa (contacts) walio karantini baada ya kumaliza siku 14,” alisema Waziri Mkuu.
 

Aidha alisema hadi tarehe 28 Aprili, 2020 watu 644 waliruhusiwa, ambao walitoka katika mikoa ya Zanzibar, Dar-es-Salaam, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Mwanza, Kagera, Dodoma, Kigoma na Songwe.

Waziri Ummy afunguka bungeni
 

Aprili 30, mwaka huu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, wakati akitoa makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2020/21 Bungeni Dodoma, alithibitisha kuwa Tanzania ni moja ya nchi zilizoathirika na janga la Covid 19.

Waziri Ummy alisema katika kudhibiti na kuhakikisha kuwa
ugonjwa huu hautoathiri watu wengi zaidi, Serikali imeendelea

kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuimarisha
ufuatiliaji wa wasafiri wanaoingia nchini kupitia viwanja vya ndege, bandari na mipaka ya nchi kavu ili kuweza kubaini wasafiri wanaoonyesha dalili za ugonjwa.


Alisema katika kuhakikisha kuwa wasafiri wote wanaoingia nchini wanapimwa joto la mwili, Serikali imenunua jumla ya vipima joto 324 (vya mkono 307 na vya kupima watu wengi kwa mpigo 17) ambavyo vimefungwa na vinatumika katika maeneo ya mipakani ikiwemo viwanja vya ndege na bandari.
 

Vilevile, Ummy alisema watumishi 120 waliajiriwa kwa muda ili
kuimarisha ufuatiliaji wa wasafiri wanaoingia nchini kupitia maeneo ya mipakani.


Ummy alisema Serikali imeandaa utaratibu maalum wa kuwaweka chini ya uangalizi wa siku 14 wasafiri wote wanaoingia nchini kwa gharama zao. 

 

Sekta ya utalii haikuachwa nyuma
 

Hata hivyo Sekta ya Utalii nayo inadaiwa kuathiri kipindi cha
Corona ambapo katika sekta hiyo ajira zilishuka kutoka 623,000
hadi kufikia 146,000 na watalii ilikadiliwa watashuka kutoka
1,867,000 waliotarajia hadi 437,000 kama janga hilo halitatulia hadi Oktoba mwaka huu.


Kauli hiyo ilitolewa Mei 7, mwaka huu na Waziri wa Maliasili na
Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla wakati akiwasilisha bungeni
makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2020/21. Alisema sekta hiyo ya utalii kabla ya madhara hayo ilikuwa inachangia asilimia 25 katika mapato yote ya kigeni inayopata nchi.

“Sekta hii imeathiriwa zaidi kutokana na ukweli kwamba
inategemea zaidi mapato ya watalii wanaotoka nje ya nchi, ambao kwa sasa kutokana na ugonjwa huu, wameshindwa kusafiri na wengi wao wamesitisha safari za kuja nchini kutalii,” alisema Dk. Kigwangalla.
 

Alisema wizara ilifanya tathmini ya awali (rapid assessment)
iliyojikita katika kipindi cha tangu ugonjwa huo uanze hadi Aprili 6, mwaka huu.
 

Dk. Kigwangalla alisema tathmini hiyo ilibaini kuwa madhara
makubwa ya corona katika sekta ya utalii yalianza kuonekana
mwanzoni mwa Machi, tofauti na Februari na Januari, mwaka huu ambapo hali ilikuwa shwari.


Hadithi hii iliungwa mkono na Kanuni ya WanaData Initiative
ya Afrika, Twaweza na Kituo cha Pulitzer juu ya Kuripoti
Majanga

No comments:

Post a Comment

Pages