NA JANETH JOVIN, Novemba 2020
“Nilikata tamaa kabisa ya maisha wakati wa janga la Covid-19
lilipoingia nchini kwetu, maana sikuweza kufanya biashara kwa
kuwa mahali nilipokuwa nafanyia ni katika shule ambazo
zilifungwa na serikali.”
Hiyo ni kauli ya Hilda Raphael mfanyabiashara ya kuuza mihogo katika Shule ya Msingi Umoja iliyopo Mabibo jijini Dar es Salaam, ambaye katika Makala hii anaeleza jinsi ambavyo ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona ulivyoweza kuleta athari katika shughuli zake za kila siku.
Hilda anasema kipindi cha corona alijiuliza maswali mengi ikiwamo janga hilo litaisha lini na atawalishaje watoto wake wawili, na kusema kuwa alikosa majibu.
Akiwa anatikisha kichwa, Hilda anasema maswali hayo yalimfanya kushindwa kumudu kukaa nyumbani kwa kuwa jambo hilo aliliona kuwa litaathiri ustawi wa familia yake na atashindwa kurejesha kwa wakati fedha za mkopo ambazo alizipata katika moja ya taasisi ya fedha hapa nchini.
“Niliamua kujiongeza nikaanza kutembeza bagia mitaani maana
niliona nisipofanya hivyo nitazidi kuchanganyikiwa kwa kuwa
nadaiwa fedha za mikopo na nilijua huenda mali zangu ambazo
niliziweka dhamana kwenye hiyo taasisi zinaweza kuchukuliwa na kupigwa mnada,” anasema.
Hata hivyo, Hilda alikuja kupata matumaini kufuatia agizo la
Serikali la kuzitaka taasisi za fedha kuongeza muda wa urejeshaji wa mikopo, na kufunguliwa kwa shule na shughuli zote ambazo zilikuwa zimesitishwa kutokana na corona kurudi kama zamani.
Hilda anasema aliporejea kijiweni kwake pale shuleni, alikutana na masharti mbalimbali ambayo yaliwekwa na viongozi wa shule, ambapo walitakiwa kila mtu kuwa na ndoo ya wanafunzi kunawa mikono kabla ya kuchukua muhogo na kula.
Vilevile anasema uongozi huo uliwataka wafanyabiashara wote wa eneo hilo la shule kupima afya zao na kupeleka majibu sehemu husika shuleni hapo.
“Tulifanya hivyo kama tulivyotakiwa na asilimia ya wafanyabiashara wote majibu yetu yalikuwa mazuri tukaruhusiwa kurejea kazini, maisha yakaendelea kama kawaida hadi hivi leo ndugu mwandishi, hakika tunaendelea kumshukuru Mungu kwa kutuepusha na janga hili,” anasema.
Hata hivyo, hali hiyo haikumtokea Hilda peke yake bali hata kwa wafanyabiashara wengine akiwamo Zakia Shaha anayefanya kazi za mama lishe katia eneo la Tangibovu kwa Komba jijini Dar es Salaam.
Zakia anafunguka na kusema kuwa kipindi cha kwanza baada ya
ugonjwa wa Covid-19 kugundulika kuwa umeingia nchini biashara kwao ilikuwa mbaya.
Anasema chakula walichokuwa wakikipika kuanzia mchana na
wakati mwingine jioni kilikuwa hakiishi kutokana na watu
kupungua mitaani na barabarani.
Zakia anaeleza kuwa wateja wao wengi walikuwa majumbani
wanaogopa kutoka kwenda makazini, hali iliyowafanya hata wao
washindwe kufanya biashara, na kusababisha hata mitaji yao
kupungua.
“Utapika chakula kingi utamuuzia nani wakati hakuna wateja,
kiukweli kipindi cha mwanzo tulipitia wakati mgumu sana ambao sitaki hata kuukumbuka,” anasema.
Hata hivyo, anasema pamoja na Serikali kusimama kidete na
kuwaondoa hofu wananchi hali ya biashara kwao bado si nzuri
kama ilivyokuwa zamani.
Vilevile anasema njia za upatikanaji wa fedha kwa upande wake
zimekuwa ngumu kwa sababu kampuni za ujenzi zimepunguza
watu ambao ndio walikuwa wakiwategemea kununua chakula chao.
Hali hiyo ilimpelekea hadi changamoto katika familia yake ambapo mtoto wa Zakia, Halfani Hamis mwenye umri wa miaka 12 anasema kuna wakati walishindwa hata kunywa chai asubuhi na kujikuta kula milo miwili kwa siku.
Hamis ambaye anasoma darasa la saba katika moja ya shule ya
msingi iliyopo Kawe, anasema kwa mara ya kwanza Serikali
iliporuhusu kufunguliwa kwa shule, alishindwa kuendelea na
masomo kutokana na mama yake kukosa fedha ya kumpatia kwa ajili ya kununua uji na chakula cha mchana.
“Maisha yalikuwa magumu sana ila kwa sasa tunamshukuru Mungu kwani hali ilivyo sio kama kipindi kile, tunakwenda shule licha ya kwamba tunapatiwa kiasi kidogo cha fedha lakini kinatutosha,” anasema Hamis.
Beng’i Issa ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji
Wananchi Kiuchumi (NEEC), anasema kipindi cha corona
kilikuwa ni kigumu kwa kuwa watu wengi, wakiwemo wajasirimali ambao wanawawezesha kiuchumi, walikuwa wakiogopa kutoka nje.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng'i Issa.
No comments:
Post a Comment