December 08, 2020

NYASA YAHITAJI MICHE LAKI NANE YA MITI


Mratibu wa FORVAC Kongani ya Ruvuma, Marcel Mutunda akizungumza na waandishi wa habari katika Bustani ya Kipiki wilayani Namtumbo kuhusu mpango wao wa ugawaji miche kwa wanakijiji wa Liuli wilayani Nyasa.

 

NA SULEIMAN MSUYA, NYASA


HALMASHAURI ya Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma imesema katika kuhakikisha misitu inakuwa endelevu wanapaswa kupanda miti laki nane.

Hayo yamesemwa na Ofisa Maliasili Wilaya ya Nyasa, Bugingo Bugingo wakati akizungumza na Blog ya Habari Mseto iliyotembelea katika mashamba ya miti Liuli.

Mwandishi wa Blog ya Habari Mseto aliambatana na waandishi wengine wa vyombo vya habari katika ziara iliyoratibiwa na Program ya Mnyororo wa Thamani ya Mazao ya Misitu (FORVAC).

Program ya FORVAC imepo kwenye Idara ya Misitu na Nyuki chini ya ufadhili wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland na Wizara Maliasili na Utalii ya Tanzania.

Akizungumzia hitaji hilo Bugingo amesema wana eneo lenye ukubwa wa hekta 700 ambapo hekta moja inachukuwa miche 1,111 hivyo kwa ukubwa huo wanahitaji miche laki nane.

Amesema kwa sasa wanahitaji miche laki tatu ili kuweza kuihudumia bila shida yoyote ambayo itafanya misitu kuwa endelevu.

"Hitaji letu ni miche laki nane lakini kwa mwaka huu tunatarajia kupata miche laki tatu au mbili ambazo tutaweza kuihudumia," amesema.

Ofisa Maliasili huyo amesema upandaji wa miche hiyo utachochea uhifadhi na utunzaji wa mazingira ambayo yameanza kuharibiwa lakini pia ni miti ya biashara.

Amesema uamuzi wa FORVAC kuwapatia miche ya kwanza 150,000 na hii ta sasa 300,000 utaweza kufanikisha malengo yao kwa mwaka huu.

Amesema wamekuwa wakigawa miche kwa wanavijiji ambao wapo tayari kupanda baada ya kupata mafunzo na faida yake.

Akizungumzia kuhusu wao kutoanzisha bustani ya wilaya amesema unahitaji fedha nyingi hivyo mfumo wa kuwaga mbegu na miche ndio rafiki zaidi.

Bugingo amesema awali walianzisha bustani lakini wakatokea watu wakorofi wakaharibu.

"Mwaka 2016 tulianza kupanda miche ya mitiki kupitia Mradi wa Private Forest (PFP) uliokuwa umefadhiliwa na Serikali ya Finland. Tukaanza kupata changamoto ya kuharibiwa miche zaidi ya miche milioni 1 na wenzetu wakulima kutoka Mbinga.

Tunashukuru FORVAC walitupatia Gerhardt tukafanya vikoa vya ujirani mwema na kufikia muafaka hivyo kwa sasa tumeanza kupanda miche zaidi ya 80,000," amesema.

Naye Samweli Mawanja Mwenyekiti wa Muungano wa Chama cha Wakulima Miti (TGA) Liuli amesema mwaka 2019/2020 walipata ruzuku ya miche 81,150 sawa na hekta 72.1 na kunufaisha wakulima 80.

Mawanja amesema FORVAC wameweza kufungua fursa ambayo imepokelewa na wanavijiji wengi na kwamba hawatawaangusha.

"2020/2021 tumeomba FORVAC, miche 300,000 ambayo itapandwa katika vijiji vya Liuli, Mkalachi, Mkali A, Mkali B na Lipingo.

Huu ni mradi pekee tangu tupate Uhuru umeweza kustawi kwa kasi kubwa hali ambayo imepokelewa vizuri na wanavijiji," amesema.

Mawanja amesema miti ya misaji ambayo wamepanda itatumika kujenga mitumbwi na maboti na kuachana kukata misitu ya asili.

Mwenyekiti huyo amesema wanatarajia kuondoa umaskini kupitia miti hiyo huku uhifadhi ukiwa wa uhakika.

Joyce Nyirenda Mkulima wa Miti ya Misaji amesema ujio wa mradi huo umeweza kuibua wanakijiji wengi kushiriki shughuli za kiuchumi.

Amesema mradi huo wa kilimo ya misaji unakabiiwa na changamoto ya miundombinu hivyo kuziomba mamlaka kusika kutengeza.

Amesema anatarajia kubadilisha maisha yake kupitia mradi huo na kuomba viongozi waendeleze ushirikiano.

Nyirenda amewataka wananchi wenzake kuacha kuchoma moto na kulima milimani kwani ni uharibifu wa mazingira.

Mwenyekiti wa TGA ya Kijiji cha Nkalachi Askofu Michael Kilia amesema ameamua kujiunga na mradi huo kwa kuwa ni fursa kwa familia yake.

"Mimi nina hekta mbili na nusu miche zaidi ya 900 naamini hata kama sitakuwepo watanufaika watoto na wajukuu wangu," amesema.

Mratibu wa FORVAC Kitaifa, Emmanuel Msoffe amesema wameamua kuwekeza katika upandaji miti ya misaji ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Amesema wechagua eneo la Liuli kwa kuwa ni eneo lenye maji na rutuba hali ambayo itawezesha miti ya misaji kuota kwa haraka.

"Tunakabiliana na uharibifu wa misitu ambao ni hekta 469,000 kwa mwaka kwa kupanda miti ya misaji ambayo inaweza kutumika kwa kazi mbalimbali.

Pia niwaombe mpunguze shughuli za kibinadamu katika Milima ya Livingstone ambayo ndio inatiririsha maji," amesema.

Amesema FORVAC inafurahishwa na ushiriki wa viongozi wa ngazi zote katika uhifadhi na utunzaji mazingira.

Msoffe amewataka wanavijiji ambao wameamua kupata miti ya misaji ambayo itavunwa baada ya miaka 25 wajikite katika kilimo cha mazao kama mihogo, miembe, ndizi na mengine mengi.

"Tunahitaji kula, kusomesha watoto hivyo shughuli za ufugaji nyuki kuwa endelevu tukisuburi miaka 24 ya uvunaji," amesema.

No comments:

Post a Comment

Pages