December 30, 2020

Serikali yaipatia R-Labs Sh.Milioni 45

 NA MWANDISHI WETU

 

Mkurugenzi wa Shirika la Reconstruction Labs Tanzania    (R-Labs) Yusuph Ssesanga ameishukuru serikali kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kuwapatia ruzuku ya Sh.Milioni 45.

 

Ssesanga ametoa shukrani hizo mkoani Iringa mwishoni mwa wiki wakati wa hafla fupi iliyowashikirisha viongozi wa serikali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mjini Richard Kasesera.

 

Amesema R-Labs Tanzania ni shirika linalowajengea uwezo vijana walio nje ya mfumo rasmi wa elimu ya maarifa ya kujitegemea kwa kuwafundisha stadi muhimu za maisha hivyo fedha hizo zimesaidia vijana wengi kupata mafunzo.

 

Amesema Tangu lilipoanzishwa mwaka 2013, shirika limejikita kuwafundisha vijana stadi muhimu kama vile ushonaji nguo, upambaji wa kumbi za sherehe na mikutano, ususi wa nywele, uselemara pamoja na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

 

Akizungumza kuhusiana Ufadhili waliopata kutoka COSTECH Mkurugenzi wa miradi toka R-LABS Naomi Rousse amesema ”walipokea ruzuku ya Sh. Milioni 45 ambayo imewasaidia katika kukamilisha baadhi ya mambo ukiwemo mgahawa wa “Youth Cafe”ambao utatoa huduma ya chakula kwa wananchi mbalimbali waliopo mjini Iringa

 

Amesema mradi huo utaweza kuiingizia taasisi hiyo fedha za kujiendesha huku ikitoa mafunzo kwa vijana watakaojiunga katika ukumbi uliopo ndani ya mghahawa huu.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH,Meneja wa mfuko wa MTUSATE Ntufye Mwakigonja, amesema tayari wameviwezesha vituo vya ubunifu 15 vinavyopatikana mikoa mbalimbali  na miongoni mwao ni R_Labs-Iringa

 

Amesema lengo lao ni kuhakikisha kila Taasisi ya ubunifu inafika katika viwango vya juu katika kuwawezesha vijana kujiajiri na kuleta mapinduzi katika teknolojia yatakayo saidia shughuli za kiuchumi na kuchangia katika pato la Taifa.

 

Kutokana na ruzuku hiyo ambayo pia imesaidia kutoa mafunzo kwa  vijana 700 kwa sasa wanaweza kujiajiri kwa kuanzisha miradi inayotoa fursa ya ajira kwa vijana wenzao pia.

No comments:

Post a Comment

Pages