December 30, 2020

DK. Kalemani atoa miezi mitatu kwa TANESCO na REA kuwaunganishia umeme wateja


 Waziri wa Nishati,  Dkt. Medard Kalemani (kushoto), akizungumza na wafanyakazi wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) mkoa wa Mwanza  katika kikao cha pamoja juu ya mikakati ya kuwasambaza Nishati hiyo katika maeneo ambayo hayajafikiwa. (Picha na Mpiga Picha Wetu).

 

 NA MWANDISHI WETU, MWANZA


WAZIRI wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani,ametoa miezi mitatu kwa  watendaji wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) na Wakala wa Umeme Vijijini (REA), kuhakikisha wanawaunganishia umeme wateja wote waliolipia  ndani ya miezi mitatu.

Waziri Kalemani ameyasema hayo leo jijini MWANZA wakati akizungumza na wafanyakazi wa TANESCO na REA katika kikao kazi cha pamoja 

Amesema ni lazima wateja wote walioko katika maeneo ya vijijini na kando kando ya miji, wanaunganishiwa umeme kwa gharama ya Sh. 27,000 bila kujali umbali wa mita 30 kwa kuwa ni  wajibu wa TANESCO kuwafikishia wananchi nguzo za umeme ili kuwafikia wateja hao. 

"Mnataka kila mwananchi awe mita 30 ndipo muwafikishie umeme? ni  kazi yenu kupeleka nguzo hadi muwafikie wananchi hao na nimeambiwa mnasubiri sekula hii sasa ndiyo sekula nawapa ndani ya miezi mitatu nihakikishe wateja wote wanaunganishiwa umeme"Amesema Dk.Kalemani

Dk Kalemani pia ameitaka TANESCO  kuanzisha madawati ya huduma kwa wateja ili kuhakikisha wateja wanapatiwa huduma bora na kwa wakati ili kuwaondolea adha wananchi  ya kufuatilia maombi ya kuunganishiwa umeme kwenye Ofisi  za TANESCO Wilayani.

hata hivyo Dk Kalemani amewataka watendaji wa TANESCO kuwafuata wateja mahali walipo na kuepuka kutumia lugha ya kukatisha tamaa kwa wateja ili kujenga mahusiano mazuri na wateja  jambo litakalopelekea kupanua wigo wa wateja na kuongeza mapato kwa Shirika.


Aidha,  Dkt. Kalemani, amewapongeza watumishi wa TANESCO kwa utendaji mzuri na kueleza kuwa kwa zaidi ya asilimia 80 utendaji wa TANESCO ni wa Kuridhisha.

Waziri Kalemani amesifu utendaji mzuri wa Meneja wa TANESCO Kanda ya Ziwa Mhandisi Henryfried Byabato na kueleza kuwa utendaji mzuri wa kazi katika maeneo mengi aliyofanya kazi ndiyo uliopelekea Mha. Byabato kupandishwa cheo.


Akizungumza na waandishi wa habari katika kikao kazi hicho, Naibu Waziri wa Nishati Byabato, amewataka watumishi wote kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Waziri Kalemani, na atahakikisha anasimamia na kufuatilia utekelezaji wake kwa ukamilifu.

Kikao kazi baina ya Waziri  Kalemani na watumishi wa TANESCO na REA, ni kikao kazi cha pili baada ya kikao na wafanyakazi wa Mkoa wa Geita wiki moja iliyopita. Lengo la vikao hivyo ni kuweka misingi ya pamoja ya utendaji kazi unaolenga kuleta matokeo chanya na ya haraka katika Sekta ya Nishati.

 

 

 

No comments:

Post a Comment

Pages