December 13, 2020

TUMEAMUA WAOMBA SHILINGI MILIONI 15 FORVAC


Mtaalam Kijana wa Kimataifa Anayeshughulikia Ufuatiaji na Thamani wa Program ya Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu FORVAC), Nette Korkanen akipokea zawadi ya begi kutoka kwa wanachama wa Kikundi cha Tumeamua cha Kijiji cha Ukata wilayani Mbinga mkoani Ruvuma.NA SULEIMAN MSUYA, MBINGA

KIKUNDI cha Tumeamua kilichopo kijiji cha Ukata, Kata ya Ukata wilayani Mbinga mkoani Ruvuma kimeomba Program ya Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu (FORVAC) kuwasaidia shilingi milioni 15 ili kukuza mtaji wa kikundi.

Ombi hilo limetolewa na Katibu wa kikundi hicho Erasto Nchimbi wakati akisoma risala mbele ya waandishi wa habari waliotembelea kijiji hicho kuona shughuli za Program ya FORVAC wilayani Mbinga.

Amesema kikundi cha Tumeamua kimeanzishwa mwezi Machi 2020 kikiwa na wanachama 25 ambapo wanaume 19 na wanawake 6.

Nchimbi amesema baada ya miezi saba ya kujenga kikundi baadhi ya wanachama walikata tamaa na hivi sasa kikundi kina wanachama 11 ambao wanatengeneza bidhaa zitokanazo na zao la mianzi inayopatikana kwenye Msitu wa Hifadhi ya Namswea-Lilengalenga kijijini hapo.

Amesema wamelazimika kuomba msaada wa shilingi milioni 15 ili kuhakikisha kuwa lengo la FORVAC la kutaka wanavijiji kutunza na kutumia rasilimali misitu kwa njia endelevu ili kujiendeleza linatimia.

"Shilingi milioni 15 zitaweza kutusukuma mbele kwani shughuli zetu za ususi zinahitaji mtaji wa uhakika ili kufikia soko kubwa.

Baadhi ya bidhaa tunazotengeneza kutokana na mianzi kutoka msitu wa Namswea-Lilengalenga ni nyungo, majamanda, mabegi ya akina mama, fagio, viti, mikeka, chujio ya nazi, vitanda, masanduku na mapambo," amesema.

Amesema kupitia fedha hizo wanatarajia kutengeneza bidhaa za sofa, meza, kabati na nyingine kwa kutumia mianzi ambazo zitachochea ukuaji wa uchumi.

Katibu huyo ametaja changamoto wanayokabiliana nayo kuwa ni pamoja na kukosa eneo la kutengenezea bidhaa hali ambayo inachangia wakae chini ya mwembe.

Changamoto nyingine ni ukosefu wa usafiri wa kusafirishia malighafi kutoka msituni na vitendea kazi duni hivyo kukwamisha baadhi ya shughuli.

Aidha, amesema wanakabiliwa na changamoto ya elimu na masoko ya uhakika ya bidhaa zao hivyo wanaomba FORVAC waendelee kuwasaidia ili kutimiza lengo la kikundi.

Akizungumzia ombi hilo Mratibu wa FORVAC Kongani ya Ruvuma, Marcel Mutunda amesema ombi hilo linafanyiwa kazi na Program na ni matumaini yao watawapatia msaada huo wa kukuza kikundi.

Mutunda amesema matamanio yao ni kuhakikisha wanavijiji wanaozungukwa na misitu wanapata faida ya kiuchumi, kimazingira, kijamii na maendeleo huku uhifadhi endelevu ukionekana.

Amesema kikundi cha Tumeamua kimeonesha matumaini kwa muda mchache hivyo wanapaswa kuungwa mkono ili kuhakikisha msitu unakuwa salama.

"FORVAC tuliitisha maandiko ambapo Kikundi cha Tumeamua kiliomba na ombi lao wamepita hatua ya kwanza hivyo ni matumaini yangu watapata msaada huo. Ila fedha hazitakuja kabla ya kupata elimu ambapo FORVAC wameingia makubaliano na Shirika la Sedit- Vicoba  lenye makao makuu yake Jijini Dar Es Salaam ambao watatoa mafunzo kwa kikundi katika eneo la masoko.

Pia tumewasiliana na mtaalam wa ufundi kutoka Kampuni ya Emmanuel ya iliyoko Uyole, Mbeya ili aje kuwajengea uwezo kielimu," amesema.
 
Mutunda amesema ili kuhakikisha kuwa mradi unakuwa endelevu wamehamasisha wanakikundi kupanda miti ya mianzi ili baadae waweze kuitumia.

Aidha, amesema wamesukumwa kuhamasisha ususi katika Kijiji cha Ukata kwa sababu historia inaonesha tangu zamani hizo kijiji kilikuwa na wasusi na kwamba vijiji vingine vya Amani-Makolo , Kiwombi,Kindimba juu, Kindimba chini, Barabara  Ndongosi vinajishughulisha na ufugaji nyuki na uvunaji uyoga kutoka msituni.

No comments:

Post a Comment

Pages