December 11, 2020

WALENGWA WA TASAF WAONYWA KUTORIDHIKA NA MAFANIKIO WALIYOYAPATA

 Na Estom Sanga – Iringa

Wajumbe wa kamati ya taifa ya Uongozi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF –NSC-wamewahimiza Wananchi wanaonufaika na huduma zitolewazo na Serikali kupitia Mfuko huo kutobweteka na mafanikio waliyoyapata badala yake watumie fursa hiyo kuuchukia zaidi umaskini.

Ushauri huo umetolewa na Wajumbe wa Kamati ndogo ya Miradi na bajeti ya TASAF wakati wa ziara ya kikazi katika wilaya za Mufindi na Iringa Vijijini mkoani Iringa ambako wamekutana na baadhi ya Walengwa wa TASAF na kujionea namna walivyotumia fursa ya kuorodheshwa kwenye Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.

Akizungumza na Walengwa katika kijiji cha Ludilo wilayani Mufindi na Matembo katika halmashauri ya Wilaya ya Iringa Vijijini, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ndogo ya NSC inayoshughulikia miradi na bajeti Dr. Naftal Ng’ondi amebainisha kuwa azma ya Serikali ni kuona kuwa Walengwa wa Mfuko huo wanatumia kwa dhati fursa hiyo kuondokana na umaskini.

Aidha Dr. Ng’ondi amewataka Walengwa wa TASAF na wananchi wengine ambao watoto wao wamepata fursa ya kuendelea na masomo ya Sekondari hapo mwakani kuhakikisha kuwa watoto hao hawaipotezi fursa hiyo adhimu .

Wakiwa katika kijiji cha Ludilo Wilayani Mufindi Wajumbe hao wametembelea Miradi ya upandaji wa miti, matunda aina ya Miparachichi na mabwawa ya kufugia samaki ambayo imetekelezwa na Walengwa wa TASAF kupitia utaratibu wa Miradi ya Ajira ya Muda-PWP.

Wajumbe hao pia wameshuhudia namna baadhi ya Walengwa wa TASAF katika kijiji cha Matembo,  halmashauri ya wilaya ya Iringa Vijijini namna walivyoboresha makazi yao kwa kujenga nyumba na kuezeka kwa mabati baada ya kupata ruzuku kutoka TASAF.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF bwana Ladislaus Mwamanga amebainisha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dokta John Pombe Magufuli ameagiza kuwa mitaa,vijiji na shehia zote nchini zijumuishwe kwenye shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini  ili Wananchi watakaokidhi vigezo waweze kunufaika na huduma za Mpango  huo maagizo ambayo amesema  yatatekelezwa kwa ufanisi mkubwa.

Mmoja wa Walengwa wa TASAF katika kijiji cha Matembo, Iringa Vijijini (katikati)  akiwa na baadhi ya Wajumbe kamati ya Uongozi wa TASAF Taifa na Wataalamu wakiwa  mbele ya nyumba aliyoijenga kutokana na ruzuku anayopata kutoka serikalini kupitia TASAF.

Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Uongozi wa TASAF taifa wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wanafunzi   wanaotoka kwenye kaya za walengwa wa  Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika kijiji cha Matembo halmashauri ya wilaya ya Iiringa Vijijini.

 Picha ya juu na chini baadhi ya Wajumbe ya Kamati ya Uongozi wa TASAF  taifa wakikagua Shamba la miti na matunda aina ya Miparachichi ambayo imepandwa na Walengwa wa TASAF kupitia utaratibu wa Ajira ya Muda katika kijiji cha Ludilo  wilayani Mufindi mkoani Iringa.

No comments:

Post a Comment

Pages