December 02, 2020

Watanzania wakaribishwa kutembelea maonesho ya bidhaa za viwanda



WIZARA ya Viwanda na Biashara kupitia taasisi yake ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) inawakaribisha Watanzania wote kutembelea Maonesho ya Tano ya Bidhaa za Viwanda vya Tanzania yatakayoanza Desemba 3 hadi 9 mwaka huu.  

 

Katika taarifa kwa umma iliyotolewa na Tantrade kupitia Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Theresa Chilambo ameeleza kuwa uanzishwaji wa Maonesho hayo yalilenga kuhakikisha Ujenzi wa Uchumi wa Viwanda unakuwa na matokeo chanya katika uchumi na yanayoonekana.

 

Chilambo amesema kuwa maonesho hayo yanalenga kujenga jukwaa kwa Wadau wa Sekta ya Viwanda kupata fursa ya kujadiliana, kubadilishana uzoefu na kutangaza fursa zilizopo katika Sekta hiyo.

 

 

“Maonesho hayo hususan, yanalenga kutoa fursa katika Kuvitambua viwanda vya Tanzania pamoja na bidhaa zinazozalishwa nchini ili Watanzania wazitambue na kupenda kuzitumia, Kuhamasisha Watanzania kutumia bidhaa na huduma zinazozalishwa hapa nchini, Kuwaunganisha wenye Viwanda na Wazalishaji mbalimbali wa Malighafi na huduma zingine zinazotumika viwandani pamoja na kuwaunganisha wenye Viwanda na Wasambazaji wa teknolojia za viwanda,” amesema Chilambo.

 

 

Amesema Kauli Mbiu ya Maonesho hayo ni “Tumia Bidhaa za Tanzania, Jenga Tanzania” ikiwa ni kuhamasisha Watanzania waendelee kupenda, kununua na kutumia bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya Tanzania kwa lengo la kuchochea uzalishaji katika sekta mbalimbali za kiuchumi ili kukuza soko la ndani na hatimaye kuiwezesha nchi ambayo imeingia katika Uchumi wa Kati. 

 

 

Hata hivyo amesema maonesho hayo yataenda sambamba na matukio mbali mbali ikiwamo Desemba, 5 2020 kufanyika Mkutano kati ya Wizara ya Viwanda na Biashara, Wamiliki wa Viwanda nchini na Taasisi za Uthibiti.

 

Amesisitiza kuwa mkutano huu utalenga kutatua changamoto zinazowakabili wamiliki wa viwanda katika uendeshaji wa shughuli za uzalishaji wa bidhaa nchini. 

 

“Desemba 6, 2020 kutakuwa na Bonanza la Maziwa litakalo husisha matembezi ya Afya (Jogging) na michezo mbalimbali. Lengo la kuwa na Bonanza la Maziwa ni kuhamasisha unywaji wa maziwa yanayozalishwa na Viwanda vya Tanzania. Washiriki na Watembeleaji wa Maonesho watapata kuvitambua na kunywa maziwa kutoka viwanda vyetu vya ndani,” amesema.

 

Hata hivyo amesema Desemba 7, 2020 kutakuwa na kongamano la biashara lenye kuelezea fursa za biashara katika nchi za Dubai, Falme za Kiarabu na Kuwait litakaloenda sambamba na mikutano  ya biashara ya ana kwa ana (B2B Meeting).

 

“Huduma ya kliniki ya biashara itatolewa kuanzia tarehe 3 hadi 9 Desemba, 2020 ambapo taasisi zinazosimamia mnyororo wa biashara nchini zitasikiliza na kutatua kero/changamoto za wazalishaji wa bidhaa za Tanzania ana kwa ana.  

 

Mabanda yatafunguliwa saa 4 kamili asubuhi hadi saa 12 Jioni, hakuna kiingilio kwa watembeleaji. Wote mnakaribishwa,” amesema Chilambo

No comments:

Post a Comment

Pages