December 12, 2020

Wateja wa Benki ya CRDB waifurahia Kava Assurance


Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na Wakati wa Benki ya CDRB, Boma Raballa, akitoa mada wakati wa uzinduzi wa Kava Assurance.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dk. Juma Mussa, akitoa hotuba yake wakati wa uzinduzi wa Kava Assurance.
Afisa  Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Dk. Joseph Witts, akizungumza katika hafla hiyo.


 

Na Irene Mark

BAADHI ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wamepongeza ubunifu wa kuongeza thamani kwenye huduma za kibenki uliofanywa na Benki ya CRDB kwa wateja wake wote.

Mwanzoni mwa wiki hii Benki ya CRDB ilitangaza kuanza kwa huduma ya bima ambatanishi ya maisha iitwayo KAVA Assurance kwa wateja wenye akaunti katika benki hiyo kwa kushirikiana na kampuni ya bima ya Sanlam Tanzania.

Huduma hiyo inatoa mkono wa pole wa Sh. Milioni mbili hadi Sh. Milioni 15 kwa mteja wa benki ya CRDB endapo yeye au mwenza wake atafariki dunia ama atapata ulemavu wa kudumu.

Wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo, Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na Wakati wa Benki ya CDRB, Boma Raballa, alisema mteja mwenye akaunti ya akiba atapata Sh. Milioni mbili na mteja mwenye akaunti maalum atapata Sh. Milioni tano.

Ruballa alisema kuhusu mteja wa Benki ya CRDB anayeishi nje ya nchi atakapopata msiba wa mwenza wake au yeye mwenyewe benki hiyo itatoa pole ya Sh. Milioni tano na kuchangia gharama za kurejesha mwili nyumbani na tiketi ya mtu atakayesindikiza maiti kiasi cha Sh. Milioni 15.

Kwa nyakati tofauti baadhi ya wateja hao walisema huduma ya Kava Assurance imeonesha namna benki hiyo inavyowajali na kuwathani wateja wake huku wakiamini kwamba watanzania wengi zaidi watafungua akaunti kwenye benki hiyo.

Akizungumza na Habari Mseto Blog leo Disemba 10,2020 Julita Stephano mwenye akaunti ya akiba katika benki ya CDRB tawi la Tegeta Kibo, alisema huduma ya Kava Assurance imeongeza thamani ya mteja na kuongeza ubunifu kwenye biashara ya benki.

“Hakuna anayeomba kupata matatizo lakini lazima tujue yapo na yatatukuta tu sasa CRDB imeona mbali ikaamua kuwafariji wateja wake ni jambo jema na Mungu awabariki sana,” alisema Julita.

Abdallah Mpote mkazi wa Kigamboni amesema huduma hiyo itawafanya wateja wa Benki ya CRDB kuiamini na kufurahia kuweka fedha kwenye benki inayomthamini.

“Ni hulka ya binaadamu kumuamini mtu anayefikiria kwa jambo jema... hivi ulisikia wapi benki inakupa hela kwa sababu umefiwa na mumeo au mkeo, hatujazoea hii ndo mara ya kwanza tunafanyiwa mambo mazuri na Benki ya CRDB,” alisema Mpote mwenye akaunti kwenye tawi la CRDB Azikiwe.

Mwalimu Anita Nassari alisema kwa umri alionao hajawahi kisikia hiyo huduma hivyo aliipongeza Benki ya CRDB kwa kuwathamini wateja wake na kuzitaka benki nyingine kuiga mfano huo.

“Mimi mshahara wangu unapitia CRDB kwa hiyo nafurahi kuwa miongoni mwa wateja wa Benki ya CRDB waliopewa thamani kwa kupata huduma ya Kava Assurance,” alisema Mwalimu Nassari.

Wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dk. Juma Mussa alisema kuanzishwa kwa huduma hiyo ya bima kwa akaunti za wateja kutaongeza chachu ya matumizi ya huduma za kifedha na kuongeza uelewa wa huduma za bima kwa watanzania.

“Huduma hii ya Bima ambatanishi katika akaunti za wateja imekuja wakati muafaka ambapo mamlaka yetu imejikita katika kuhakikisha watanzania wote wanafikiwa na huduma za kifedha ikiwamo huduma za bima,” alisema Dk. Mussa huku akiitaka Benki ya CRDB na Sanlam kujikita katika kutoa elimu ili kuongeza uelewa zaidi kwa wateja wao.

Akielezea utayari wa Benki ya CRDB katika kusogeza huduma za bima kwa wateja, Meneja Mkuu wa Kampuni Tanzu ya Bima ya CRDB Bank Insurance, Wilson Mnzava alisema pamoja na kuanzisha kwa huduma ya KAVA Assurance, Benki ya CRDB pia ipo mbioni kuingiza huduma ya bima kidijitali ambayo itawawezesha wateja kupata huduma kupitia simu za mkononi na hivyo kuwafikia Watanzania wengi zaidi.

Nae Mkurugenzi Mkuu kampuni ya Bima ya Sanlam Afrika Masharika, Julius Magabe alisema kampuni yake inaishukuru Benki ya CRDB kwa fursa hiyo ya kutoa huduma kwa wateja wake zaidi ya milioni tatu idadi kubwa zaidi kulinganisha na idadi ya watu katika nchi za Botswana na Namibia.

“Nitoe rai kwa Watanzania wengi zaidi kuchangamkia fursa hii kwa kufungua akaunti katika Benki yao ya CRDB, kwa kufanya hivyo tutawezsha kufikia lengo la Serikali la kufikisha huduma za Bima kwa asilimia 50 ya Watazania,” alisisitiza Magabe.

No comments:

Post a Comment

Pages