HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 15, 2021

Vyama vya siasa vyatakiwa kutii katiba na sheria za nchi

Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi.

 

NA HAMIDA RAMADHANI, DODOMA

 

Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, ametoa wito kwa vyama vya siasa nchini kuendelea kutii Katiba ya Nchi na sheria zinginezo za nchi .

Pia amevitaka vyama vya siasa viendeleze siasa za kistaarabu na kuheshimu katiba zao ikiwa ni njia ya kukuza demokrasia nchini lakini pia itachangia katika kupunguza migogoro ndani ya vyama vyao.

Jaji Mutungi ameeleza hayo leo jijini hapa kupitia taarifa yake kwa umma ambayo ni mahususi kwa ajili ya kuwatakia heri ya mwaka mpya watanzania wote, viongozi wa vyama vya siasa na wadau wa siasa za ushindani nchini. 

“Mwezi Oktoba 2020 ulifanyika Uchaguzi Mkuu wa kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge na Madiwani, na kwa upande wa Zanzibar uchaguzi ulihusisha Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Baraza la Wawakilishi na Madiwani ambapo Vyama vyote 19 vyenye usajili wa kudumu vilishiriki uchaguzi kwa kuweka wagombea katika nafasi mbalimbali,” alisema . 

Na kuongeza kuwa “Vyama 15 viliweka wagombea wa Kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku Vyama 17, vikiweka wagombea wa Kiti cha Urais Zanziba na vyama vyote 19 viliweka wagombea wa Ubunge, Baraza la Uwakilishi na Udiwani kwa idadi tofautitofauti,’’amesema Jaji Mutungi.

Aidha ametoa pongezi kwa vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu  kwa kuridhia kwao kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwezi, Oktoba 2020.

“Nanavipongeza vyama vyote vya Ssasa kwa kutilia maanani suala la utulivu na utii wa sheria za nchi ikiwemo sheria zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kwani suala hili siyo tu limedhihirisha ukomavu wa kisiasa bali limechangia mchakato mzima wa uchaguzi kumalizika kwa amani na utulivu,’’amesema . 

Na kuongeza kuwa“Ni matarajio ya mzalendo yeyote kuipenda na kuilinda nchi yake, Ni kwa dhamira hiyo hiyo sisi kama Wananchi wa Tanzania tunashukuru kwamba Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 umemalizika salama na kwa amani na kuacha nchi yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikisalia na umoja na mshikamano kama ilivyo desturi na utamaduni wetu,” amesema  Jaji Mutungi.

Hata hivyo Kwenye taarifa hiyo Jaji Mutungi ameendelea kusisitiza Watanzania kuendelea kuunga mkono maono ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliyoyatoa mara baada ya kuapishwa kwa kuwa uchaguzi sasa umekwisha badala yake wananchi wote bila kujali itikadi za vyama vyao wajikite katika harakati za kuleta maendeleo ya taifa na ustawi wa wananchi wake kwa ujumla.

“Ni kwa kuzingatia haya maono hayo aliyotoa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nimeona nito rai kuwaomba  Watanzania hususan Vyama vya Siasa kwa umoja wetu, tuzingatie na kuyatekeleza kwa vitendo maono haya ya Mhe. Rais,”

Katika hatua nyingine Jaji Mutungi ametoa pongezi kwa Vyama vya CCM, ACT – Wazalendo na ADA TADEA kwa kuonesha dhamira njema kisiasa na maendeleo kwa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar kwa maslahi ya Wanzanzibari wote.

Ameongeza kuwa ukomavu huo wa kisiasa waliouonesha uwe endelevu na mfano wa kuigwa na vyama vyote vya siasa nchini bila kujali itikadi zao pindi linapojitokeza suala linalohusu utaifa na maendeleo ya nchi kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

Pages