April 29, 2021

KCU YAPEWA SIKU 30 KUFUATILIA FEDHA ZA MFUKO WA MAZAO

 Naibu mrajisi wa vyama vya ushirika nchini Collins Nyakungi akizungumza na wanachama wa chama kikukuu cha ushirika cha mkoa wa Kagera KCU 1990 ltd katika mkutano mkuu wa chama hicho. (Picha na Alodia Dominick).

 

Na Alodia Dominick, Bukoba

Naibu mrajisi wa vyama vya ushirika nchini Collins Nyakunga    ametoa siku 30 kwa bodi ya chama kikuu cha ushirika cha mkoa wa Kagera KCU  1990 (limited ) kufuatilia fedha za mfuko wa mazao wa wanaushirika zaidi ya shilingi milioni  500  ili kujua fedha hizo ziko wapi.

Tamko hilo limekuja baada ya wanachama  kuleta taarifa ya kuanzisha mfuko mpya wa kuweka fedha za wakulima jambo ambalo lilikataliwa na wanachama  hao na hivyo kudai mfuko wa mazao uliokuwepo miaka ya tisini ambao ulikuwa na fedha za wakulima zaidi ya milioni 500 waelezwe fedha hizo zilipo na hatua zilizochukuliwa dhidi ya wahusika waliokuwa wanasimamia mfuko huo.

Ametoa wito huo jana katika mkutano mkuu wa chama hicho wa kuchagua viongozi wa bodi na kupitisha bei ya kununua kahawa katika msimu wa fedha wa mwaka 2021/2022 ambapo naibu mrajisi wa vyama vya ushirika nchini  Nyakunga, aliitaka bodi kufuatilia fedha ya wakulima zaidi ya shilingi 500 milioni.

“Wakulima wanataka kujua hatma ndiyo maana hawakutaka mfuko mwingine mimi nimetoa maelekezo kwamba ukaguzi ufanyike tujue hizo fedha  milioni 500 ziko kwenye akaunti na kama hazipo zimekwenda wapi nani amezitumia kwa ruhusa ya nani, hata wale watendaji na ile bodi waliokuwa wanasimamia mfuko huo wako wapi wenzetu wanaokwenda kufanya uchunguzi watatwambia” Amesema Nyakunga.

Respicius John mwanachama kutoka chama cha ushirika Nsunga wilaya ya Misenyi amesema kuwa, wao kama wanachama hawawezi kukubali kuwa na mfuko mpya wakati mfuko uliokuwepo fedha zake hazijulikani zilipo na hauna faida kwa wakulima.

John ameeleza kwamba, wamalize kwanza tatizo la mfuko wa mazao uliokuwepo ndipo waanze kushughulikia mfuko mpya.  

Hata hivyo, Katika mkutano huo wanachama wamepitisha bei ya kununua kahawa kwa msimu 2021/2022 ambapo kilo ya kahawa maganda aina ya robusta watainunua shilingi 1200 huku kahawa safi iliyokobolewa kilo moja shilingi 2,000 na imechaguliwa bodi ya watu watano ya chama hicho.

No comments:

Post a Comment

Pages