April 30, 2021

NMB yadhamini UDSM Career Fair, yaanika mikakati kwa wasomi

Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard, akitoa mada katika kongamano la Career Fair 2021 kwa wanafunzi wa vyuo vikuu lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

 

NA MWANDISHI WETU

KATIKA kuthibitisha kwa vitendo kiu ya kuwa Mwajiri Bora Zaidi na Mtoa Huduma Bora Zaidi za Kibenki nchini, Benki ya NMB imedhamini Kongamano la Career Fair 2021 kwa wanafunzi wa vyuo vikuu mbalimbali, ililolitumia kuanika mikakati yake kwa wasomi wa Kitanzania.

Career Fair ambalo mwaka huu limefanyika kwa mara ya 20 tangu kuanzishwa kwake, ni jukwaa linalolenga kuwakutanisha wasomi wa vyuo vikuu mbalimbali, wadau wengine wa elimu ya juu na waelimishaji kutoka taasisi, mashirika na kampuni, ili kuwajuza mahitaji na changamoto za soko la ajira.

Akizungumza wakati wa kongamano hilo, lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard, alisema wasomi vijana nchini watabaki kuwa kundi muhimu na la kipaumbele kwa benki yake na kwamba wanafunzi hao wanapaswa kuongeza ushirikiano wao kihuduma na taasisi yake.

Ikidhamini kongamano hilo chini ya kaulimbiu isemayo 'The Future is Youth', Donatus alibainisha kuwa NMB itaendeleza programu zake mbalimbali kwa vijana, hasa wa elimu ya juu, na kwamba kiu yao kama taasisi ni kuwa mshirika sahihi na bora wa muda wote wa huduma za kibenki kwa kila mdau wa Sekta ya Fedha nchini Tanzania.

"Kiu yetu ya kuwa mshirika sahihi na bora zaidi kwa vijana hususani mliopo elimu ya juu na vyuo vikuu mbalimbali nchini, inatusukuma kuhakikisha tunaendeleza programu mbalimbali za vijana, zikiwemo zinazolenga kuwapa uzoefu, ujuzi na ufanisi mahali pa kazi, sambamba na kuisaidia Serikali kutatua tatizo la ajira kwa wasomi wamalizapo masomo.

"Mnapaswa kutambua kwamba mko katika vyuo bora, vinavyotoa elimu Bora kwenu na ili kuwapa nguvu, NMB inasimama kuwajengea uwezo, huku tukijipambanua kama Mwajiri Bora na Mtoa Huduma za Kibenki Bora Zaidi nchini mnayepaswa kushirikiana naye katika kutimiza ndoto zetu katika soko la ajira," alisema Donatus.

Alizitaja baadhi ya programu za NMB kwa wasomi na wanavyuo mbalimbali nchini kuwa ni pamoja na mafunzo ya uongozi (Management Trainee) na uvumbuzi wa vipaji vya wanafunzi wa chuo, ambako katika kipindi cha miaka mitano, imewawezesha vijana 50 kutoka vyuo mbalimbali nchini kupitia mchakato huo na kukuza uzoefu wa kazi.

Programu nyingine ni mikataba ya muda mfupi ya kuongeza ujuzi kwa miezi mitatu hadi 12 kwa wanachuo wanaofanya 'field' katika benki yake, aliyoitaja kama taasisi pekee ya fedha nchini inayolipa mishahara wanafunzi wa kada hiyo, na wanaofanya vema miongoni mwao kupewa mikataba rasmi ya ajira.

Kongamano la Career Fair 2021 lilizinduliwa Aprili 24 kwenye Ukumbi wa Puma uliopo Makataba Mpya ya UDSM, ambako lilifunguliwa na Amidi wa Shule Kuu ya Biashara, Ulingeta Obadia Mbamba, akimwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo (UDSM), Profesa William Anangisye. Kongamano hilo lilifungwa Jumapili ya Aprili 25.

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa kongamano hilo, Profesa Ulingeta aliwasisitiza wana vyuo walioshiriki umuhimu wa kufanya mazingatio kwa yale watayopata kutoka kwa watoa mada, na wazungumzaji waalikwa toka kwa taasisi, mashirika na Kampuni zilizodhamini ama kushiriki kwa namna moja ama nyingine.

"Changamoto katika soko la ajira ni nyingi na mahitaji nayo yamekuwa yakibadilika. Kwa mantiki hiyo, shahada, astashahada, diploma, digrii ama vyeti vyenu mnavyopata baada ya kuhitimu vyuo vinaweza visiwasaidie sana, iwapo hamtojikita kusoma alama za nyakati sokoni kabla ya kuingia. 'Connection' ya kuyajua yote hayo ni jukwaa hili la Career Fair kupitia washiriki watakaozungumza," alisema Prof. Obadia.

No comments:

Post a Comment

Pages