May 01, 2021

ZAIDI YA KILO 800 ZA DAWA ZA KULEVYA ZAKAMATWA TANZANIA

 

  

Mkurugenzi Mtendaji Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na dawa za Kulevya, Kamishna Jenerali Gerald Kusaya akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam.

 

Hussein Ndubikile, Dar es Salaam

 

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na  Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania Kamandi ya Wanamaji imefanikiwa kukamata Dawa za kulevya zenye jumla ya Kilo 859.08 katika Bahari ya Hindi upande wa maji ya Tanzania.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Kamishna Jenerali wa mamlaka hiyo, Gerald Kusaya ambapo amesema dawa hizo zilikamatwa Aprili 24 mwaka huu zikiwa zimefichwa ndani Jahazi la uvuvi lililokuwa likitokea nchini Iran.

Amebainisha kuwa katika jahazi hilo walikutwa Raia wa Iran Saba wakiwa na Dawa za heroin hydrochloride kilo 504.36 na Methamphetamine kiasi cha kilo 355.

Aliwataja majina yao kuwa ni Jan Miran (42) nahodha was jahazi jilo, Amir Kasom (35), Issa Ahmad (30), Salim Fedhmuhammad (20), Ikbal Mohammad (22), Jawid NurMohammad (19) na Mustaphar Kadirbaksh (20).


" Mamlaka kwa ushirikiano wa JWTZ tumefanikiwa kukamata Dawa za kulevya tunawaomba wananchi waendelee kutupa ushitikino tushinde vita hii ",amesema Kamishna Kusaya.

Watuhumiwa raia wa nchi hiyo wamefikishwa leo mahakamani kwa la Uhujumu Uchumi, kesi namba 02 ya mwaka 2021 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Maria Bantulanye na kusomewa mashtaka ya kusafirisha Dawa hizo.

Amesisitiza kuwa ukamataji huo ni mkubwa kuwahi kutokea tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo na kwamba huo ni mwanzo na mapambano yameanza.

Ameongeza kuwa lengo lao ni kuona nchi iliyo huru kutoka kwenye matumizi na biashara ya Dawa hizo.

Amefafanua kuwa matumizi ya dawa za kulevya husababisha magonjwa ya mbalimbali yakiwemo ya uraibu, moyo, ini na mapafu pamoja na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.

Mengine ni virusi vya homa ya ini pamoja na kifua kikuu.

Aidha, amesema matumizi yake husababisha kukithiri vitendo vya uhalifu, wizi, utapeli na uporaji kwa nia kununua Dawa hizo.

Pia amesema wafanyabiashara wa Dawa hizo huendesha magemge ya utekaji, mapigano na mauaji na kufanya jamii kuishi kwa uwoga, biashara haramu ya kusafirisha binadamu pamoja na kufadhili ugaidi.

Ametoa wito kwa jamii kuendelea kutoa taarifa za watu wrote wanaojihusisha na biashara hiyo ili wachukuliwe hatua za kisheria.


No comments:

Post a Comment

Pages