April 28, 2021

USMJ ILIVYOREJESHA MADIWANI MOROGORO

Meneja Mradi wa TTCS Charles Leonard akielezea mafanikio ya mradi huo kwa wanavijiji na halmashauri za vijiji na wilaya.


Mwenyekiti wa Halmashauri ya Morogoro ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Matuli, Lucas Lemomo akieleza namna Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa (TTCS) ulivyomuwesha kutetea udiwani wake 2020.

 

NA SULEIMAN MSUYA


USIMAMIZI Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ) unaotekelezwa katika vijiji zaidi ya 30 na wilaya tatu za mkoa wa Morogoro umetajwa kuwa ni sababu kubwa kwa waliokuwa madiwani kuchaguliwa mwaka 2020.

USMJ mkoani Morogoro unatekelezwa katika Wilaya za Kilosa, Mvomero na Morogoro DC ambapo vijiji zaidi ya 30 vinanufaika kiuchumi, kijamii, maendeleo na uhifadhi.

USMJ katika vijiji hivyo inatekelezwa na Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS) kupitia Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswisi (SDC).

Ushuhuda huo umetolewa na Madiwani Lucas Lemomo wa Kata ya Matuli wilayani Morogoro na Hassan Kambenga Kata ya Kisanga wilayani Kilosa wakati wakizungumza na mwandishi wa habari hii.

Diwani Lemomo amesema Mradi wa TTCS ulifika kwenye kata katika awamu ya kwanza ya udiwani wake mwaka 2015 ambapo vijiji vitatu vya Matuli, Diguzi na Tununguo.

Lemomo ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Morogoro amesema ujio wa mradi ulihakikisha kunakuwepo na matumizi bora ya ardhi na kitambua mipaka ya misitu ndio shughuli za uzalishaji zikaanza.

"Katika kata ya Matuli, Tarafa ya Ngerengere, Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), 2015/2020 imetekelezwa kwa zaidi ya asilimia 90 kwa kupitia TTCS.

Yote ambayo tulikuwa tumeahidi wananchi, kwa mfano mimi niliahidi sekondari ambapo awali tulijenga madarasa mawili kwa miaka 10 ila fedha za misitu zimejengwa majengo mapya na shule umeanza," amesema.

Ilani ya CCM katika Ibara ya 69 (F), Sera ya Misitu ya mwaka 1998 na Sheria ya Misitu ya Mwaka 2002 kwa pamoja vinasisitiza umuhimu wa wananchi wanaozungukwa na misitu kunufaika na rasilimali hiyo.

Lemomo amesema pia wamejenga ofisi za vijiji za kisasa, wajumbe wa serikali ya kijiji na wenyeviti wanapewa posho na wananchi wamekuwa na uchumi mzuri hivyo kufanya shughuli za maendeleo.

Diwani amesema wamefanikiwa kujenga Zahanati kwenye kijiji cha Lulongwe ila wameishia njiani kutokana na vikwazo vya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)

"Niweke wazi kuwa bila TTCS sisi madiwani ambao tunatoka kwenye vijiji vyenye miradi hatungerudi kwani zaidi ya shilingi milioni 600 zimepatikana na kutekeleza miradi huku serikali ikipeleka shilingi milioni 15," amesema.

Mwenyekiti huyo wa halmashauri ameyataka mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali kuendeleza miradi hiyo kwa vijiji ambavyo vina misitu ya asili.

Amesema halmashauri ya Morogoro inatarajia kutenge fedha za kutekeleza mradi kwenye vijiji viwili kwa kuwa manufaa ya vijiji vitano vya Matuli, Diguzi, Lulongwe, Mlilingwa na Tununguo yameonekana.

Kuhusu changamoto ya TFS Lemomo amesema ipo haja kwa serikali kuangalia huu mfumo ili uwe endelevu na sio kukwamisha kama anavyodai.

Amesema vijiji vyenye USMJ uhifadhi umeongezeka kwa asilimia kubwa huku wanavijiji wakinufaika tofauti na vijiji visivyo na mradi.

Kwa upande Diwani Kambenga wa Kata ya Kisanga amesema TFCG imechochea maendeleo makubwa katika vijiji 20 vya wilaya Kilosa.

"Sisi Kisanga tuna vijiji viwili ambavyo vimenufaika na mpango wa matumizi bora ya ardhi, ujenzi wa ofisi za kijiji, madarasa yamejengwa, wananchi wamelipiwa bima ya afya  CHF.

Pia ofisi ya kijiji imejengewa choo cha kisasa, elimu ya utawala bora na uhifadhi zimetolewa hali ambayo kinawapa motisha wananchi kuilinda misitu," amesema.

Amesema kupitia miradi hiyo hakutumia nguvu kubwa kujinadi kwani wananchi wameona matunda ya utawala wake.

Kambenga amesema Serikali inapaswa kutenga bajeti kila mwaka ili kuendeleza miradi hiyo kwa vijiji vipya.

Diwani huyo amesema changamoto kubwa ni TFS kutowapa ushirikiano wavunaji wa mazao ya misitu waliopo kwenye vijiji vya USMJ hali ambayo inakatisha tamaa wanavijiji.

"Wavunaji wa mazao ya misitu yasiyo na mpango wa matumizi bora ya ardhi wanapewa huduma nzuri kuliko waliopo kwenye vijiji vya mradi," amesisitiza.

Akizungumzia mafanikio ya TTCS Meneja Mradi Charles Leonard amesema zaidi ya shilingi bilioni 3.5 zimepatikana hadi sasa.

Amesema shilingi bilioni 2 zimeelekezwa kwenye Serikali za vijiji na kutekeleza miradi ya maendeleo kama elimu, afya, maji na uhifadhi.

"Shilingi bilioni 1.5 wamepata wavunaji wa mazao ya misitu ikiwemo mkaa na mbao huku wakizingatia uhifadhi," amesema.

Meneja huyo amesema iwapo misitu itatunzwa na kutumiwa kiundelevu inamchango mkubwa kwa wananchi  na nchi kwa ujumla.

Leonard ameiomba Serikali kuweka mkazo katika USMJ kwa kuwa ina matokeo chanya kwa asilimia 80.


No comments:

Post a Comment

Pages