April 28, 2021

Uchakataji magogo kiteknolojia waongeza thamani kwa asilimia 60


NA SULEIMAN MSUYA

TEKNOLOJIA ya uchakataji wa mazao wa misitu hasa magogo imetajwa kuongeza thamani ya mazao hayo kwa asilimia 60 huku mapato yakiongezeka hadi kufikia asilimia 100.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mpingo na Maendeleo (MCDI), Makala Jasper (pichani) wakati akizungumza mbele ya wadau wa sekta ya misitu, mazingira na uihifadhi waliokutana jijini Dodoma.

Amesema MCDI imekuwa ikishirikiana na taasisi zingine kama Shirika la Kuhifadhi Misitu Tanzania (TFCG), Program ya Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu (FORVAC) kuhamasisha uongezaji wa thamani mazao ya misitu.

Makala amesema kwa muda mwingi uvunaji mazao ya misitu hususani magogo umekuwa ukipoteza mbao nyingi ila ujio wa teknolojia mpya imesaidia kuchochea ongezeko la mapato.

Amesema MCDI kwa kushirikiana na wadau wengine wameweza kuwesha vijiji venye misitu ya asili kupata mashine za kisasa ambazo zinaongeza thamani mazao hayo kwa asilimia 60.

Mkurugenzi huyo amesema ujio wa teknolojia umesaidia vijiji  kuuza mbao na sio magogo kama zamani ambapo walivuna kwa kutumia Sawmill.

"Kwa sasa vijiji ambavyo vilikuwa vinauza magogo vimebadilika na vinauza mbao zilichakatwa kwa teknolojia hivyo thamani ya mazao ya misitu hasa mbao imeongezeka kwa asilimia 60.

Ila kubwa zaidi ni mapato yameongezeka kati ya asilimia 60 hadi 100 jambo ambalo linachochea usimamizi na ulinzi wa rasilimali misitu," amesema.

Makala amesema pia kupitia ujio wa teknolojia umewezesha ajira zisizo za moja kwa moja 200 na ajira za moja kwa moja 5.

"Lengo la kuingiza teknolojia ni kuongeza thamani ya mazao ya misitu, mapato, ajira na uhifadhi na yote yananyika kwa ufanisi," amesisitiza.

Kwa upande wake Dk.Asha Salum kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), amesema ujio wa teknolojia umeongeza thamani na  kuchochea maendeleo kwa wanavijiji.

Dk.Salum ambaye pia ni Balozi wa Kampeni ya Mama Misitu iliyoratibiwa na Mtandao wa Usimamizi wa Misitu ya Jamii Tanzania (MJUMITA) amesema nguvu kubwa ilekezwe kwenye teknolojia ili misitu iendelee kuwa salama na endelevu.

"Ushahidi umeonesha uchakataji wa kutumia teknolojia unaongeza thamani kwa asilimia 60, uhifadhi na mapato hivyo ni vema hamasa ikajikita huko ili misitu iwe endelevu," amesema.

Mhadhiri huyo mwandamizi amesema dhana ya kuongeza thamani mazao ya misitu isambazwe kila eneo ambalo lina misitu ya asili ya vijiji.

Dk.Salum amesema uendelevu wa misitu utarahisisha wanawake kutekeleza majukumu yake kwa amani kwani atakuwa na uhakika wa kupata maji, nishati na huduma nyingine muhimu.

Ameitaka Serikali kuipa kipaumbele miradi ambayo inahusiana na Usimamizi Shirikishi wa Mazao ya Misitu kwa kuwa imekuwa na matokeo chanya.

Mwenyekiti wa Bodi ya MCDI na Shirika la Kuhifadhi Misitu Tanzania (TFCG), John Salehe amesema mafanikio ya mipango na mikakati ya kuifanya misitu kuwa endelevu itafikiwa kwa wadau wote kuwa kitu kimoja.

"Usalama na uendelevu wa rasilimali misitu ni lazima wadau wote yaani watunga sheria, Sera, wasimamizi na waibua miradi kuwa kitu kimoja kwa kuangalia Tanzania ijayo kinyume na hapo ni maumivu kwa wote," amesema.

No comments:

Post a Comment

Pages