Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Selemani
Jafo akiwa na viongozi wa Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro wakati
akiangalia dampo la kisasa lililojengwa manispaa hapo.
Muonekano wa dampo la kisasa lililojengwa Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
NA SULEIMAN MSUYA
WAZIRI
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Selemani Jafo
amewapongeza viongozi na watendaji wa Manispaa ya Moshi Wakiongozwa
Mstahiki Meya Wa Manispaa hiyo Juma Raibu kwa namna wanavyohifadhi taka
ngumu zinazozalishwa kila siku katika manispaa hiyo.
Jafo aliyasema hayo alipokuwa katika ziara ya Kikazi katika Manispaa ya Moshi leo Mei 22, 2021.
Katika
ziara hiyo waziri huyo alitembelea dampo la kisasa la manispaa hiyo
ambapo aliridhishwa na namna wataalamu wanavyosimamia vyema utupaji wa
taka hizo sambamba na ubadilishaji wa baadhi ya taka hizo kuwa mboji.
Jafo amezitaka halmashauri nyingine kuiga mfano wa manispaa hiyo ya Moshi katika uhifadhi bora wa taka ngumu.
Aidha,
Waziri Jafo pamoja na ukaguzi wa dampo hilo alitembelea kiwanda cha
China Paper Industry ambapo aliwataka wamiliki wa kiwanda hicho kutafuta
njia ya kutumia nishati mbadala kwani kwa sasa wanatumia magogo mengi
kwa ajili ya nishati na hivyo kusababisha uharibifu mkubwa wa
mazingira.
Amewapa mwaka mmoja wamiliki wa kiwanda hicho kuja na njia nyingine ya nishati mbadala wa magogo yanayotumika sasa.
Pia
waziri huyo amewataka wamiliki wa kiwanda cha kutengeneza nondo cha
Five Star Steel kinachotumia chuma chakavu kuepuka kununua vyuma
vinavyotoka katika miundombinu ya umma ikwemo madaraja, alama za
barabarani na kutoka kwa watu binafsi ili kutoleta hasara kwa jamii.
Hata
hivyo, Jafo amekipongeza kiwanda hicho kwa kudhibiti kusambaa kwa moshi
kutoka katika kiwanda hicho ambapo kwa siku za nyuma ulikuwa unakera
raia wanaoishi jirani ya kiwanda hicho.
No comments:
Post a Comment