May 25, 2021

KALEMANI ATOA MAAGIZO MAZITO KWA REA


 NA HAMIDA RAMADHANI, DODOMA


WAZIRI wa Nishati Medard Kalemani amewaagiza wakandarasi wa mradi  wa wakala wa umeme vijijini (REA) awamu ya tatu mzunguko wa pili kuhakikisha hadi kufikia 2022 vijiji vyote nchini vinapata umeme.

Aidha katika Mpango huo pia amesema hatomfumbia macho mkandarasi ambae ataleta kikwazo Cha miundo mbinu,na kubagua baadhi ya nyumba za nyasi, tembe na zile za tope.

Waziri Kalemani ameyasema hayo leo jijini hapa kwenye kikao kazi kilichowajumuisha wakandarasi mbalimbali ambapo pamoja na mambo mengine amewataka  wakawe wabunifu katika utekelezaji wa  majukumu yao.

"Kumekuwa na tabia ya mkandarasi kuruka nyumba hizi za tope ,nyasi na nyumba za tembe hivyo basi natoa maelekezo vijiji vyote vilivyo baki muende mkavipelekee Nishati hii ya umeme ndani ya miezi hiyo 18 mliosaini katika mikataba yenu na Serikali," .

Na kuongeza kusema " Tumekuwa tukipata malalamiko mengi kwamba kuna baadhi ya maeneo yamerukwa, hivyo muende mkaone ni namna gani mnaweza kufanya  Ili vijiji vyote vilivyopitwa vipate umeme kwa wakati," amesema Kalemani.

Hata hivyo amewataka wakandarasi hao waliosaini mkataba kwenda kuwasili eneo la Kazi na waende kutoa taarifa kwa Viongozi  wa eneo wanalotaka kufanyiwa Kazi.

" Hili ni muhimu sana kwani mtaondoa taharuki kwa wenyeji wenu hivyo muende mkajitambulishe kwa Mkuu wa Wilaya ,Mbunge, na hata Viongozi wa vijiji  kwani hawa ndio wawakilishi wa wananchi mnaokwenda kuwahudumia na mkawasikilize  au wawakilishi wao na mkifanya hivi hakika kazi yenu itakuwa nyepesi ," amesema Kalemani.

Amesema huo ni Mpango wa Mwisho miezi 18 ni michache hivyo amewashauri wakati wanatekeleza magenge au vituo viwe vingi angalau kila mkandarasi awe na vituo 5 ambapo ameeleza vituo hivyo vitawasaidia kukuwa kikazi.

Pia amewataka wakandarasi hao kupunguza kero kwa kuhakikisha wanatoa ajira kwa Vijana wazawa na kuachana na habari za kuja na vibarua wao ,kwa kufanya hivyo Kazi zao zitakuwa shirikishi kwa  wananchi.

Sambamba na hayo Waziri Kalemani ametoa maagizo mengine mahususi kwa wakandarasi hao na kuwaelekeza vibarua wao kuacha kuwauzia wananchi nguzo za umeme, kuwepo na stoo,kusiwepo na visingizio vya kutofikika kwa maeneo na kuondoa kero ya uunganishwaji wa umeme (wiring).

Naye Naibu Waziri wa Nishati Steven Byabato amesema ameyapokea maelekezo na sasa ni muda wa kwenda kuyafanyia Kazi ambapo amesema mikakati ya Serikali ni kwamba hadi kufikia 2022 kila mtanzania kijiji chake kiwe kimefikiwa na Nishati ya umeme.

Hata hivyo amewataka wakandarasi hao kuhakikisha wanawasili haraka iwezekanavyo katika maeneo yao ya Kazi na kuanza Kazi haraka kama walivyosaini katika mikataba yao.

No comments:

Post a Comment

Pages