May 25, 2021

Tutamuenzi hayati JPM kwa kutimiza ahadi zake Veta

 

Mkurugenzi Mkuu wa Veta, Dk. Bujulu akitoa maelekezo kwa Waziri Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako na Balozi wa China hapa Tanzania, Ke kuhusu  vifaa vilivyotolewa na serikali ya China kwaajili ya mafunzo ya uvuvi na uchakataji wa mazao ya samaki kwa Chuo cha Veta wilayani Chato Mkoa wa Geita.


Waziri Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako na Balozi wa China hapa nchini, Ke wakibadilishana mikataba waliyosaidi kuhusu upokeaji wa vifaa vya mafunzo ya Uvuvi na uchakataji wa mazao ya samaki, utiaji saini wa mkataba huo ulifanyika kwenye Makao Makuu ya Veta jijini Dar es Salaam leo Mei 25.2021.

 

Na Irene Mark

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amesema watatekeleza ahadi zote walizozitoa kwenye Vyuo vya Ufundistadi VETA ikiwa ni sehemu ya kumuenzi Hayati Rais John Magufuli.

Profesa Ndalichako amesema hayo Dar es Salaam leo Mei 25.2021 wakati akipokea msaada wa vifaa vya mafunzo ya uvuvi na uchakataji wa mazao ya samaki vilivyotolewa serikali ya China kwaajili ya Chuo cha Veta, Wilaya ya Chato mkoani Geita.

Akizungumza muda mfupi baada ya kuvikagua na kuvipokea, Profesa Ndalichako, amesema vifaa vilivyotolewa ni majokofu, mashine za kusindika samaki, kutengeneza soseji za samaki na boti ya uvuvi ambavyo thamani yake ni Sh. milioni 350.

“Tunaishukuru sana Serikali ya China kwa msaada huu ambao ni mwendelezo wa urafiki na undugu wetu wa siku nyingi, naomba uongozi wa VETA ukavitunze vifaa hivi ili vidumu”, alisema Profesa Ndalichako.

Kuhusu kuwepo kwa somo jipya la uvuvi na uchakataji wa mazao ya uvuvi, amesema kutawawezesha wananchi wa Chato, Kagera na mikoa ambayo wananchi wake wanategemea uvuvi kuinua kipato chao.

“Hili somo nataka sasa Veta mkalifundishe kwenye mikoa yenye maziwa kama kule kwetu Kigoma kuna Ziwa Tanganyika... hii itaboresha uchumi wa wananchi wa maeneo hayo.

Balozi wa China nchini Tanzania, Wang Ke amewapongeza watanzania kwa kuwa na rasilimali nyingi huku akiahidi kuendelea kushirikiana na VETA katika kusukuma mbele gurudumu la ujuzi kwa vijana.

“Niwatakie heri ya siku ya Afrika... Serikali ya China inafurahishwa naa juhudi zenu za kuwekeza kwenye ujuzi. Tutaendelea kushirikiana ili kuleta maendeleo ya Tanzania na Afrika,” amesema Balozi Ke.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Veta, Dk. Pancras Bujulu amesema mchakato wa upatikanaji wa vifaa hivyo ulianza Januari 6.2021 baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa China alipotemebelea Tanzania na kuzindua rasmi Chuo cha Veta wilayani Chato.

No comments:

Post a Comment

Pages